August 18, 2017

Wafuasi wa upinzani wamekusanyika katika barabara za kuelekea majengo ya Mahakama ya Juu
Muungano wa upinzani nchini Kenya National Super Alliance leo unatarajiwa kuwasilisha kesi ya kupinga ushindi wa Rais Uhuru Kenyatta katika uchaguzi mkuu uliofanyika tarehe 8 Agosti.
Mawakili wa muungano huo wanatarajiwa kuwasilisha kesi hiyo katika majengo ya Mahakama ya Juu mjini Nairobi.
Kesi ya kupinga matokeo ya uchaguzi wa urais yaliyotangazwa Ijumaa wiki iliyopita yanafaa kuwasilishwa kabla ya leo saa sita usiku, kabla ya kumalizika kwa siku saba tangu kutangazwa kwa matokeo.
Mgombea urais wa chama hicho waziri mkuu wa zamani Raila Odinga alikuwa ameapa kutopinga matokeo ya urais tena kortini kabla ya uchaguzi kufanyika na baada ya matokeo kutangazwa.
Lakini alibadilisha uamuzi huo na kutangazwa Jumatano wiki hii kwamba muungano wake ungefika kortini kupinga matokeo hayo.
Bw Odinga alisema ingawa muungano huo ulikuwa umeapa kutowasilisha kesi kortini wakati huu, waliona ni heri kufanya hivyo "kufichua uovu uliotokea wakati wa uchaguzi mkuu."
"Tumeamua kwenda kortini kufichua jinsi uongozi wa kompyuta ulivyofanikishwa...Hawa ni viongozi wa kompyuta. Kompyuta ndiyo iliwataga, kompyuta iliangulia, kompyuta iliwatoa. Vifaranga vya kompyuta."


Bw Odinga alisema mitambo ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi IEBC ilidukuliwa na matokeo kuvurugwa kumfaa Bw Kenyatta ambapo kulikuwa na pengo kiasi fulani kati yake yeye na Bw Kenyatta muda wote wa kutangazwa kwa matokeo.
Aidha, kiongozi huyo aliishutumu tume ya uchaguzi akisema ilikuwa ikitangaza matokeo ya uchaguzi bila kutoa Fomu 34A za kuonyesha matokeo yalivyokuwa katika vituo vya kupigia kura.
Jamii ya kimataifa ilikuwa imehimiza upinzani, pamoja na wagombea wengine ambao hawakuwa wameridhishwa na uchaguzi, kutumia mifumo iliyowekwa kikatiba kutafuta haki.
Kwa mujibu wa matokeo ya IEBC, Rais Kenyatta alipata kura 8,203,290 huku naye Raila Odinga akipata kura 6,762,224.

Chanzo: IEBC

Tarehe muhimu kesi ya kupinga uchaguzi wa rais

  • Agosti 18: Siku ya mwisho ya kuwasilsiha kesi
  • Agosti 20: Siku ya mwisho ya kuwasilisha nyaraka za kesi kwa wanaofaa kujibu kesi
  • Agosti 24: Siku ya mwisho kwa wanaofaa kujibu kesi kuwasilisha majibu
  • Septemba 1: Siku ya mwisho kwa Mahakama ya Juu kutoa uamuzi.
Uamuzi wa Mahakama ya Juu kuhusu kesi hiyo ni wa mwisho. kwa mujibu wa Katiba ya kenya, iwapo mahakama hiyo itaidhinisha ushindi wa Bw Kenyatta kiongozi huyo ataapishwa kuongoza kwa muhula mwingine tarehe 12 Septemba, siku saba baada ya kutolewa kwa uamuzi.
Iwapo mahakama hiyo itakubali malalamiko ya upinzani na kubatilisha ushindi wa Bw Kenyatta, basi uchaguzi mpya utafanyika katika kipindi cha siku 60 baada ya uamuzi kutolewa, kufikia tarehe 31 Oktoba.
Takwimu kutoka IEBC

0 MAONI YAKO:

Post a Comment

Popular Posts

WADAU

BLOG ZINGINE