January 10, 2014


  MBUNGE wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe (CHADEMA), amesema kuanzia sasa hataki malumbano na mtu. Kauli ya Zitto, imekuja siku moja baada ya Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, kupiga marufuku chombo chochote kujadili uanachama wake. Akizungumza na MTANZANIA mjini Dar es Salaam jana, Zitto alisema ameamua kukaa kimya ili kupata muda mzuri wa kutafakari misukosuko ya kisiasa aliyokumbana nayo.

“Kuanzia sasa naomba kukwambia sitaki malumbano na mtu, natafakari misukosuko ya kisiasa niliyokumbana nayo kwanza,” alisema Zitto.

Alisema hayuko tayari kujibizana na mtu yeyote na kwamba anataendelea kufanya kazi ya kuwawakilisha wananchi wa jimbo lake.

Alisema jukumu jingine lililo mbele yake ni kutunga sheria ndani ya Bunge na kuisimamia Serikali kupitia Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC).

“Kazi kubwa iliyoko mbele yangu hivi sasa, ni kuwatumikia wapiga kura wa jimbo langu, kutunga sheria za nchi kwa manufaa ya Watanzania na kuisimamia Serikali kupitia kamati yangu,” alisema Zitto.

Zitto alitoa kauli hiyo, baada ya kutakiwa na MTANZANIA kutoa msimamo wake, baada ya CHADEMA kumtangaza kuwa yeye ni mbunge wa mahakama.

Alisema hivi sasa majukumu yaliyoko mbele yake ni makubwa, hivyo haoni kama kuna umuhimu wa kuendeleza malumbano.

Juzi Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, chini ya Jaji John Utamwa, ilitoa uamuzi wa maombi yaliyowasilishwa na Zitto kupitia wakili wake, Albert Msando, kwa hati ya dharura Januari 2, mwaka huu.

“Nakubaliana na hoja za Wakili Msando, pande mbili zinapopingana lazima shauri lao lisikilizwe mahakamani ili haki itendeke.

“Mdai akivuliwa uanachama, akapoteza nafasi yake ya ubunge, Serikali italazimika kufanya uchaguzi mdogo, kufanya uchaguzi mdogo ni hasara kwa Serikali, kwani utahusisha hadi wapiga kura, hali itakayosababisha fedha nyingi kutumika, itakuwa hasara kwa Zitto kupoteza nafasi mbili, ya ubunge na Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali kabla kesi yake ya msingi haijasikilizwa,” alisema Jaji Utamwa.

Alisema kwa kuzingatia hoja zilizowasilishwa, mahakamani ilikubaliana na maombi ya mdai, hivyo inatoa zuio kwa Chadema na chombo chochote kujadili uanachama wa Zitto hadi kesi ya msingi itakapomalizika kusikilizwa.

Kabla ya kutoa uamuzi huo, mahakama hiyo ilitupilia mbali hati kinzani iliyoapwa na mawakili wa Chadema, Tundu Lissu na Peter Kibatala, kutokana na makosa ya kisheria.

Pamoja na hati hiyo, pia mahakama iliziondoa aya tatu katika hati ya kiapo aliyoapa Wakili Kibatala kwa niaba ya Bodi ya Wadhamini wa chama hicho na Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk. Willbroad Slaa kwa sababu hakueleza alichoandika alikipata wapi.

Maombi yaliyotolewa uamuzi juzi yalikuwa dhidi ya Baraza la Wadhamini la Chadema pamoja na Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk. Slaa.

Katika kesi ya msingi iliyopo mahakamani hapo, Zitto anaiomba mahakama izuie kamati hiyo kujadili uanachama wake hadi rufaa yake itakaposikilizwa na Baraza Kuu la chama hicho na anaomba mahakama imwamuru Dk. Slaa ampe nakala za taarifa za vikao vilivyomvua uongozi ili akate rufaa.

0 MAONI YAKO:

Post a Comment

Popular Posts

WADAU

BLOG ZINGINE