April 29, 2017

Image may contain: 1 person 

Good News zilizotufikia ni hii ya mwanamuziki toka nchini Tanzania Dayna Nyange hit maker wa nyimbo za Angejua na Komela, Amechaguliwa kushiriki katika tuzo hizi za nchini Nigeria. Taarifa iliyoufikia uongozi wa Dayna na Dayna Nyange ni kwamba mwanamuziki huyo amechaguliwa kushiriki katika tuzo za BAE kipengele cha Best African ACT Vocal Perfomance Femail  na Best African Act

“Best Vocal Performance Female”
ARAMIDE-              “Fun Mi Lowo”
NGOWARI-             “Ebasitam”
ROCKNANA-         “Sweetie Potato”
DAYNA NYANGE-   “Angelua”

Na kipengele kingine ni Best African Act akiwa na 

Best African Act”
EDDY KENZO.             “Uganda”
RABBIT KIKI KAKA.     “Kenya”
STONEBWOY.              “Ghana”
DAYNA NYANGE.        “Tanzania”
JAH VINCI.                  “Jamaica”

Tuzo hizo zinazotarajiwa kutolewa hivi karibuni nchini humo.kumpigia kura Dayna Nyange tembelea tovuti ya www.baeawards.com Tunatoa pongezi kwa Dayna na Timu yake kwa kuchaguliwa kushiriki katika tuzo hizi na tunamtakia kila la kheri 

January 22, 2017


Ni kundi jipya kabisa kutoka mkoani Morogoro, wanaitwa Mokomoko Movement, humu wamekutana wasanii zaidi ya saba na wakafanya huu wimbo unaitwa Movement zangu. Wasanii hao ni pamoja na Tea -Sigwer, Gonga, Lotta Komba, Medy Botion, Rajlam, Vennt Skillz, Mash J pamoja na Makunga

Song - Movement Zangu

Crew - Mokomoko Movement

Producer - Vennt Skillz

Production - Kwanza Records

Contacts:0653 36 10 70 Vennt Skillz

Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif  Sharif Hamad, amemwandikia barua Gavana wa Benki ya Tanzania (BoT), Profesa Beno Ndulu ili achukue hatua za kulishughulikia sakata la fedha za ruzuku zinazodaiwa kukwapuliwa na CUF upande wa Mwenyekiti anaetambuliwa na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, Profesa Ibrahim Lipumba.

Maalim Seif ameandika barua hiyo yenye kumbukumbu namba CUF/HQ/AKM/003/017/01 na nakala zingine kuzituma kwa mamlaka mbalimbali.

Katika barua hiyo kwa Profesa Ndulu, Maalim ameamabatanisha kumbukumbu ya miamala ya fedha ilivyofanyika, pia amesema kuwa chama hicho kinaendelea na taratibu za kukamilisha hatua za kisheria ili kuwafikisha mahakamani wahusika wote walioshiriki  katika kuchukua fedha hizo, akiwapo Msajili wa Vyama vya Siasa Jaji Francis Mutungi.

Amesema kuwa, Mutungi atakuwa na kesi ya pili na atashtakiwa kutokana na madai ya kushirikiana na walalamikiwa wale wale wa kufungua akaunti mpya ili wapewe ruzuku.

Aidha, amesema Jaji Mutungi amefanya hivyo huku akifahamu fika kuwa kuna kesi ya msingi iliyopangwa kusikilizwa Februari 2, 2017 mbele ya Jaji Kihiyo.

“Gavana baada ya Muhtasari huo, kwa masikitiko makubwa leo nakuandikia barua hii kukujulisha kuwa njama za kuiba fedha za ruzuku  ya CUF Chama cha Wananchi zimefanikiwa  kwa kufanya muamala wa jumla ya shilingi 369,378,502.64 toka kwa Msajili wa Vyama vya Siasa nchini kwenda akaunti namba 2072300456 ya NMB tawi la Temeke januari 5 mwaka huu,”amesema Maalim.

Hata hivyo, hivi karibuni CUF upande wa Maalim Seif ulilalamikia hatua iliyochukuliwa na Jaji Mutungi kuwapa CUF upande wa Profesa Lipumba zaidi ya shilingi milioni 360 za ruzuku

Barua ya Maalim Seif Sharif Hamad kwa Gavana wa Benki Kuu Tanzania.
------------------------------------------------------------------------------------
Napenda kuchukua fursa hii kwa niaba ya Katibu Mkuu Maalim seif Sharif Hamad kukutumia nakala ya barua ambayo alimuandikia Gavana wa Benki Kuu kuhusiana na kadhia ya wizi wa fedha za ruzuku ya CUF kama hatua za awali katika kulishughulikia suala hili.
Chama chetu kinaendelea na taratibu za kukamilisha hatua za kisheria ili kuwafikisha mahakamani wahusika wote walioshiriki katika wizi huu akiwemo Jaji Francis Mutungi.
itakumbukwa kuwa kwa barua ya tarehe 10/10/2016 ambayo tuliisambaza katika press confernce yetu tuliyoifanya peacock hotel wiki iliyopita na hata katika mitandao ya kijamii Jaji Mutungi alimjulisha KATIBU MKUU kuwa amesitisha kutoa ruzuku kutokana na mgogoro uliokuwepo CUF.
Jaji Francis Mutungi ni Mlalamikiwa namba moja, wakiwemo pia Mwanasheria mkuu wa serikali na Lipumba na wenzake katika shauri la madai namba 23/2016 lililopo mahakama kuu mbele ya Jaji Kihiyo.
Jaji Francis Mutungi ameshirikiana na walalamikiwa wenzake kutaka kujaribu kufungua akaunti mpya ya CUF hapo awali ili awape ruzuku kwa matarajio ya kupata mgawo wake kutokana na fedha hizo kwa njia haramu. Jaribio ambalo tulifanikiwa kulidhibiti.
Jaji Francis Mutungi ameshiriki kitendo haramu cha wizi na kutakatisha fedha kinyume na katiba ya CUF na muongozo uliotolewa na ofisi yake. Lakini Tamaa ya fedha imemtia Upofu juu ya haki na uadilifu.
hali akijua kuwa kesi ya msingi imepangwa kusikilizwa tarehe 21/2/2017 mbele ya Jaji KIhiyo. Leo Jaji Mutungi eti anasema ametoa fedha hizo kwa uongozi halali na kwamba ndani ya CUF hakuna mgogoro wowote wa kiuongozi.
Ni mataraji yetu kuwa tutashirikiana kuhakikisha misingi ya demokrasia na haki inajengwa katika nchi yetu.
Mbarala Maharagande
K/Naibu Mkurugenzi wa Habari, Uenezi na Mahusiano na Umma CUF Taifa.
0784001408/ 0715 062 577
THE CIVIC UNITED FRONT
(CUF – Chama cha Wananchi)
OFFICE OF SECRETARY GENERAL
P.O.BOX 3637, Zanzibar, Tanzania
Our Ref: CUF/HQ/AKM/003/017/01 Date: 11/01/2017
Mhe.Gavana,
Benki Kuu ya Tanzania (BOT),
2 Mirambo Street,
11884 Dar es salaam,
S.L.P. 2939,
DAR ES SALAAM.
YAHUSU: WIZI WA FEDHA SHILINGI 369,378,502.64 MALI YA
THE CIVIC UNITED FRONT (CUF-CHAMA CHA WANANCHI)
Tafadhali husika na mada tajwa hapo juu na rejea barua ya Bodi ya Wadhamini kwako Kumb.Na.CUF/HQ/BRT/005/016/12 ya tarehe 10/10/2016.
Barua ya Bodi ya Wadhamini ya CUF-Chama cha Wananchi iliandikwa kwako kukujulisha juu ya njama zilizokuwa zikifanywa kwa ushirikiano kati ya Msajili wa Vyama vya Siasa nchini na Prof.Ibrahim Haruna Lipumba kutaka kufungua akaunti katika benki ya NMB tawi la Ilala kwa minajili ya kuitumia kuiba fedha za ruzuku ya CUF-Chama cha Wananchi. Bodi ilifanya hivyo baada ya kupata taarifa za uhakika, ikiwemo muhtasari wa kugushi wa kikao cha Bodi kilichoketi tarehe isiyojulikana, uliotiwa sahihi na Bwana Thomas Malima na ambao ulipata baraka za Msajili wa vyama vya siasa nchini kwa barua yake yenye Kumb. Na.322/362/14/104 ya tarehe 6/10/2016. Barua ya Bodi ilinakiliwa kwa Msajili wa Hazina, Wizara ya Fedha na Wakurugenzi Watendaji wa benki zote kwa ajili ya taarifa na tahadhari. Aidha pamoja na hatua hiyo ya Bodi ya Wadhamini, nilimwandikia Msajili wa Vyama vya Siasa nchini barua Kumb.Na.CUF/HQ/AKM/003/016/023 ya tarehe 7/10/2016 kumtahadhalisha juu ya hatua yake ya kushirikiana na Prof.Ibrahim Haruna Lipumba (ambaye si mwanachama wa CUF) kuingilia masuala ya fedha za Chama ambayo kwa mujibu wa Katiba ya Chama ya 1992 (Toleo la 2014) vifungu 93(1) na 98(3) yako chini ya dhamana ya Katibu Mkuu wa Chama na Bodi ya Wadhamini. Barua hiyo niliinakili kwa Mkurugenzi Mtendaji wa benki ya NMB kwa taarifa na tahadhali na kwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa lolote linaloweza kutokea kutokana na njama hizo za Msajili wa Vyama vya Siasa nchini na mshirika wake Prof.Ibrahim Haruna Lipumba.
Baada ya hatua hizo Msajili wa Vyama vya Siasa nchini alighadhabika na kuamua bila sababu yoyote ya msingi kusitisha ruzuku ya Chama kupitia barua yake Kumb.Na.HA.322/362/14/17 ya tarehe 10/10/2016 ambayo nanukuu haya ya mwisho .... “Kwa kuwa fedha za ruzuku ni fedha za umma ambazo zinahitaji usimamizi mzuri katika matumizi yake, na kwa kuwa ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa ina dhamana ya kugawa fedha za ruzuku kwa Vyama vya Siasa vinavyostahili na kusimamia uwajibikaji katika matumizi ya fedha hizo, hivyo baada ya tafakuri ya kina nimeona ni busara kwanza kusimamisha kwa muda mgao wa ruzuku kwa chama chenu mpaka hapo chama chenu kitakaporejea katika hali shwari kiutendaji inayowezesha viongozi husika kusimamia matumizi ya fedha hizo ipasavyo.”…mwisho wa kunukuu. Sina barua nyingine toka Msajili wa Vyama vya Siasa nchini inayoelekeza vinginevyo na hata kama Msajili angeliamua kuniandikia Barua nyingine kuwa anaanza kutoa tena ruzuku ya CUF kwa vyovyote vile angeliingiza kwenye akaunti ya Chama iliyoidhinishwa na Bodi ya Wadhamini kufuatia barua Kumb. Na. CUF/HQ/AKM/003/016/024 ya tarehe 14/10/2016.
Mheshimiwa Gavana, baada ya muhtasari huo wa utangulizi, kwa masikitiko makubwa leo nakuandikia barua hii kukujulisha kuwa njama za kuiba fedha za ruzuku ya CUF-Chama cha Wananchi zimefanikiwa kwa kufanya muamala wa jumla ya Tshs.369,378,502.64 toka kwa Msajili wa Vyama vya Siasa nchini kwenda akaunti Na.2072300456 ya benki ya NMB tawi la Temeke tarehe 5/1/2017. Akaunti ambayo imetumika katika wizi wa fedha hizo ilifunguliwa tarehe 01/08/2002 na viongozi wa CUF wilaya ya Temeke kwa ajili ya kupokelea fedha zinazopangwa na Kamati ya Utendaji ya Taifa ya CUF. Ifahamike kuwa kila wilaya ya Kichama ya CUF inayo akaunti ya wilaya ambayo inatumika kupokelea fedha zinazopangwa na Kamati ya Utendaji ya Taifa. Akaunti za namna hii (za wilaya) hata siku moja hazikuwahi kupangiwa matumizi ya kupokea ruzuku kutoka Serikali Kuu. Katibu Mkuu wa CUF na Bodi ya Wadhamini ya CUF, hawakuwahi kuielekeza mamlaka yoyote ya serikali na au Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa kwamba ianze kuweka fedha za ruzuku ya CUF kwenye akaunti yoyote ya CUF ya ngazi ya wilaya.
Tumejiridhisha na wizi huo na utaratibu uliotumika ni huu ufuatao;
1. Kati ya tarehe 02/01/2016 na 05/01/2017 akaunti Na. 2072300456 ilibadilisha watia sahihi kwa kuongezwa majina ya Magdalena Hamis Sakaya, Thomas Malima na Zainab Mndolwa ili watumike kuidhinisha miamala ya fedha,
2. Alhamisi ya tarehe 5/1/2017 Msajili wa Vyama vya Siasa nchini alifanya muamala wa Tshs.369,378,502.64 kwenda akaunti Na.2072300456 na watia saini wapya walikwenda kuthibitisha muamala huo kupitia tawi la NMB Mandela.
3. Ijumaa ya tarehe 6/1/2017 watia saini hao wakiongozwa na Thomas Malima walikwenda NMB tawi la Temeke na kutoa Tshs.69,000,000/= fedha taslimu na kuhamisha Tshs.300,000,000/= kwenda akaunti ya mtu binafsi Na.41401600207 ya NMB Handeni yenye jina la Mhina Masoud Omary.
4. Jumatatu ya tarehe 9/1/2017 asubuhi, Mhina Masoud Omary aliyetumika katika utakatishaji wa fedha hiyo iliyoibiwa, alikwenda tawi la NMB Magomeni na kuchukua fedha taslimu Tshs.150,000,000/= (katika mikupuo miwili ya Tshs.100,000,000/= na Tshs.50,000,000/=),
5. Siku hiyo hiyo ya Jumatatu tarehe 9/1/2017 majira ya mchana Mhina Masoud Omary alikwenda tawi la NMB Kariakoo akachukua tena Tshs.149,500,000/= (katika mikupuo miwili ya Tshs.100,000,000/= na Tshs.49,500,000/=) na akaunti yake kubaki na bakaa ya Tshs.207,907/=.
Mhe.Gavana, nyaraka za kufanyika miamala hiyo zimeambatanishwa pamoja na barua hii kwa ushuhuda na kwa hatua zako.
Tumejiridhisha kuwa huu ni wizi, utakatishaji wa fedha na ufisadi uliohusisha viongozi wa umma ikizingatiwa mambo haya yafuatayo;
a) Imekuwaje Msajili wa Vyama vya Siasa nchini asitishe ruzuku ya CUF-Chama cha Wananchi kwa barua Kumb.Na.HA.322/362/14/17 ya tarehe 10/1//2016 yenye nukuu .... “Kwa kuwa fedha za ruzuku ni fedha za umma ambazo zinahitaji usimamizi mzuri katika matumizi yake, na kwa kuwa ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa ina dhamana ya kugawa fedha za ruzuku kwa Vyama vya Siasa vinavyostahili na kusimamia uwajibikaji katika matumizi ya fedha hizo, hivyo baada ya tafakuri ya kina nimeona ni busara kwanza kusimamisha kwa muda mgao wa ruzuku kwa chama chenu mpaka hapo chama chenu kitakaporejea katika hali shwari kiutendaji inayowezesha viongozi husika kusimamia matumizi ya fedha hizo ipasavyo.” halafu atengue uamuzi huo bila taarifa kwa mamlaka ya Chama kikatiba kujulishwa rasmi? Inawezekanaje Msajili wa Vyama vya Siasa nchini aamue kuipa CUF ruzuku kupitia kwenye akaunti ya ngazi ya wilaya huku akiikwepa kwa makusudi, akaunti ya Chama iliyoidhinishwa na Bodi ya Wadhamini kupitia barua Kumb. Na. CUF/HQ/AKM/003/016/024 ya tarehe 14/10/2016.
b) Kama Msajili wa Vyama vya Siasa nchini alisitisha ruzuku ya CUF-Chama cha Wananchi kwa kutomwamini Katibu Mkuu, Kamati ya Utendaji ya Taifa, Baraza Kuu la Uongozi la Taifa na Bodi ya Wadhamini katika kusimamia fedha hiyo, iweje akamwamini Prof.Ibrahim Haruna Lipumba na genge lake ambao anafahamu fika sio wanachama wa CUF baada ya maamuzi halali ya kikao cha Baraza Kuu la Uongozi Taifa kumfukuzwa uanachama tarehe 27/9/2016 na kwamba shauri Na.23/2016 la Bodi ya Wadhamini dhidi Prof.Ibrahim Haruna Lipumba lililopo Mahakama Kuu bado halijahitimishwa? Je katika mazingira hayo, ushwari aliokusudia katika barua yake ya kusitisha ruzuku uko wapi?
c) Tarehe 10/10/2016 Msajili wa Vyama vya Siasa nchini alimwandikia barua Katibu Mkuu wa CUF-Chama cha Wananchi yenye Kumb.Na.AB.111/368/01/77 akimtaka atenge akaunti maalum kwa ajili ya fedha ya ruzuku toka serikalini na akajibiwa kwa barua Kumb.Na.CUF/HQ/AKM/003/016/024 ya tarehe 14/10/2016 iliyoambatanishwa na muhtasari wa kikao cha Bodi ya Wadhamini kilichomjulisha kuwa akaunti maalum kwa ajili ya ruzuku ni Na. 021101002699 ya NBC Zanzibar. Kwa nini Msajili huyo huyo akafanya muamala wa fedha ya ruzuku ya Chama kwenye akaunti nyingine (akaunti Na.2072300456 ya benki ya NMB tawi la Temeke)? Nani alitengua maamuzi ya Bodi ya Wadhamini ambayo ndiyo inasimamia mali na rasilimali za Chama kikatiba?
d) Kama ilikuwa bahati mbaya, kwa nini fedha hiyo haikuelekeza kwenye akaunti Na. 011103005079 ya NBC tawi la Corporate iliyokuwa ikitumika kabla ya mabadiliko ya tarehe 14/10/2016? Lakini bahati mbaya hiyo ya kufanya muamala kwenye akaunti Na.2072300456 ya benki ya NMB tawi la Temeke, ilikuwaje ikatanguliwa na mabadiliko ya haraka ya watia saini na kuingiza majina ya watu waliokaribu na Prof.Ibrahim Haruna Lipumba kinyume na Katiba ya Chama ya 1992(Toleo la 2014) na maamuzi ya vikao halali vya Chama? Benki ya NMB imekuwaje ikasimamia na kuruhusu miamala ya viwango hivyo vikubwa vya fedha katika muda mfupi na ikizingatiwa kuwa akaunti ya Na.41401600207 ya NMB Handeni ya Mhina Masoud Omary ni ya mtu binafsi ambayo haikuwa na fedha zozote kwa muda mrefu?
e) Kitengo cha usalama cha benki ya NMB ilikuwaje kishindwe kuzingatia taratibu za kazi yao na kuzuia miamala hii ya harakaharaka mithiri ya fedha za akaunti ya ESCROW?
f) Inawezekanaje fedha za umma ambazo zinasimamiwa ugawaji na uwajibikaji katika matumizi yake kwa mujibu wa sheria za fedha za nchi na sheria ya vyama vya siasa nchini zikachezewa kwa kiwango hiki cha watu kugawana na kutolewa katika taasisi ya fedha kwa kutumia mifuko ya sandarusi bila kuchukuliwa kwa tahadhari yeyote mbali na taasisi zote za fedha nchini kujulishwa njama za Msajili wa Vyama vya Siasa nchini na Prof.Ibrahim Haruna Lipumba dhidi ya fedha na rasilimali za CUF-Chama cha Wananchi kupitia barua Kumb. Na.CUF/HQ/BRT/005/016/12 ya tarehe 10/10/2016 ?
g) Baada ya fedha hizo za CUF kuhamishiwa kwenye akunti ya mtu binafsi(Na.41401600207 ya NMB Handeni ya Mhina Masoud Omary) isiyotambulika kwa Katibu Mkuu wa CUF; ambaye ndiye muwajibikaji mkuu wa masuala ya fedha kwa mujibu wa kifungu cha 93(1) cha Katiba ya CUF ya mwaka 1992(Toleo la 2014), isiyotambulika kwa Kamati ya Utendaji ya Taifa ya CUF ambayo inawajibika kupanga bajeti mbalimbali na isiyotambulika kwa Baraza Kuu la Uongozi la Taifa la CUF ambalo ndilo lina mamlaka ya usimamizi wa jumla wa Chama; Je Kurugenzi ya Fedha ya CUF, Wakaguzi wa Ndani wa Fedha za Chama na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) watakaguaje na kujiridhisha juu matumizi yake?
Mhe.Gavana nimekuandikia kueleza masikitiko yangu binafsi, Bodi ya Wadhamini na ya CUF-Chama cha Wananchi kwa ujumla wake kwa kitendo cha Hazina ya Wizara ya Fedha na Msajili wa Vyama vya Siasa nchini ambaye ni Jaji wa Mahakama Kuu na hivyo ni mjuzi katika tasnia ya sheria kwa makusudi kuacha kabisa maadili ya kazi zao na kushiriki katika utoroshaji wa fedha za Chama, kilichosajiliwa kwa mujibu wa Katiba na Sheria za nchi huku wakitambua bila ya shaka yoyote kwamba kufanya hivyo ni kwenda kinyume na kanuni na taratibu za masuala ya fedha na sheria za nchi. Hii ni aibu kubwa sana katika sekta ya fedha katika nchi yetu, ikizingatiwa taswira iliyoanza kujengwa na serikali ya awamu ya tano. Kama benki ya NMB inaweza kutumika katika wizi wa fedha tena za taasisi kubwa kama CUF, usalama wa fedha za serikali na za mtu mmoja mmoja zinazopitia benki hiyo ukoje? Ni nani katika Hazina ya Wizara ya Fedha anayeruhusu fedha za umma zipelekwe kokote kule bila kuzingatia taratibu, kanuni na sheria za nchi? Je Msajili wa Vyama vya Siasa ni juu ya maelekezo na maagizo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kusimamia rasilimali za nchi? Ukaguzi wa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali(CAG) kwa fedha inayochotwa na kugawanya kwa mtindo huu unafanyikaje? Je Mamlaka ya Mapato(TRA) ilikusanya kodi kwa mnufaika Mhina Masoud Omary?
Ni maswali mengi yasiyokuwa na majibu na yenye kutia shaka juu ya uadilifu wa Msajili wa Vyama vya Siasa nchini Jaji Francis S.K.Mtungi. Tunazo taarifa za Jaji Francis S.K.Mtungi kushawishi ofisi na taasisi kadhaa za serikali kugushi nyaraka ili kumnufaisha Prof.Ibrahim Haruna Lipumba na genge lake. Mwenendo huo ni hatari sio tu kwa CUF-Chama cha Wananchi bali kwa mustakabali wa siasa za vyama vingi nchini, demokrasia na utengamano wa Taifa.
Mhe.Gavana nihitimishe kwa kukuomba kwa mamlaka uliyonayo, ufuatilie na kuchukua hatua stahiki ili kuhakikisha kuwa fedha hiyo iliyoibiwa inarejeshwa na wahusika wote wa wizi huo, ikiwemo watendaji wa benki ya NMB waliohusika na kadhia hii wanachukuliwa hatua stahiki ili kuzuia michezo hiyo michafu inayoipotezea nchi mapato kwa vitendo viovu na ubinafsi wa watumishi wa umma wasiokuwa na maadili ya kazi zao. Kwa mamlaka yako nikuombe kuchukua hatua za makusudi kuhakikisha kuwa fedha ya ruzuku ya CUF-Chama cha Wananchi iliyozuiliwa ambayo ni takriban Tshs.635,000,000/= inakuwa salama, na pale itakapohitajika kutolewa kwa Chama ipelekwe kwenye akaunti rasmi ya Chama iliyopitishwa na Bodi ya Wadhamini na ambayo inakaguliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali(CAG) ambayo ni A/C Na. 021101002699 ya NBC Zanzibar.
Ni matarajio yangu na Chama Chetu kuwa utazingatia taarifa hii, na maombi yetu utayapa uzito unaostahiki.
Namaliza kwa salaam za Chama chetu,
HAKI SAWA KWA WOTE

Seif Sharif Hamad
KATIBU MKUU
Nakala:
1. Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa hesabu za Serikali(CAG),
Makao makuu, Dar es Salaam.
2. Mkurugenzi Mtendaji National Microfinance Bank(NMB),
Makao makuu, Dar es Salaam.
3. Mkurugenzi wa Kuzuia na Kupambana na Rushwa TAKUKURU,
Makao makuu, Dar es Salaam.
4. Wanasheria na Mawakili wa CUF-Chama cha Wananchi.
5. Mamlaka ya Mapato Tanzania(TRA) Makao Makuu.

Viambatanisho:
1. Barua kwa Gavana Bank Kuu, kuhusu njama za ufunguaji akaunti Kumb.Na.CUF/HQ/BRT/005/016/12 ya tarehe 10/10/2016.
2. Barua ya ufunguaji wa akaunti kwa Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, Kumb. Na. CUF/HQ/AKM/003/016/023 ya terehe 7/10/2016.
3. Barua kwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali Kumb. Na. CUF/AKM/003/016/051 ya tarehe 14/10/2016.

4. Barua ya kufukuzwa uanachama Prof.Ibrahim Haruna Lipumba Kumb. Na. CUF/HQ/OKM/WM/2016/Vol.1/50 ya tarehe 28/9/2016.
5. Barua ya kusitishwa ruzuku Kumb. Na. HA.322/362/14/17 ya tarehe 10/10/2016

Taarifa kuhusu ziara ya Rais wa Uturuki nchini
Rais wa Jamhuri ya Uturuki, Mheshimiwa Recep Tayyip Erdogan anatarajiwa kufanya ziara ya kitaifa ya siku mbili nchini tarehe 22 na 23 Januari 2017 kwa mwaliko wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli.

Mhe. Rais Erdogan ambaye ataambatana na Mkewe, na kuongoza ujumbe wa watu 150 wakiwemo Mawaziri, Wabunge, Maafisa kutoka Serikalini na Wafanyabiashara anatarajiwa kuwasili kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere tarehe 22 Januari, 2017 jioni  na atapokelewa na Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Madhumuni ya ziara hiyo ni kukuza mahusiano mazuri yaliyopo baina ya Uturuki na Tanzania pamoja ‎na kupanua fursa za uwekezaji hususan katika maeneo ya biashara  na uwekezaji.

Wakati wa ziara hiyo, Mhe. Erdogan  atakutana na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kwa mazungumzo ya faragha yatakayofuatiwa  na mazungumzo rasmi yatakayowahusisha wajumbe wa pande mbili na baadaye Marais hao watashuhudia uwekwaji saini wa mikataba ya ushirikiano kwenye maeneo mbalimbali.

Siku hiyo ya tarehe 23 Januari, 2017, kutakuwa na Kongamano la Biashara kati ya Uturuki na Tanzania litakalowakutanisha Wafanyabiashara kutoka nchi hizi mbili. Kongamano hilolitahutubiwa na viongozi wa Tanzania na Uturuki.

Mhe. Rais Erdogan na ujumbe wake watashiriki Dhifa ya Chakula cha jioni kilichoandaliwa Ikulu kwa heshima yake na Mhe. Rais Magufuli.
 
Mahusiano ya Uturuki na Tanzania‎
Mahusiano ya Tanzania na Uturuki ni mazuri. Ikumbukwe kuwa, kufunguliwa kwa mara nyingine kwa Ubalozi wa Uturuki hapa nchini mnamo Mei 2009 kuliongeza kasi ya mahusiano baina ya nchi hizi mbili. Katika hatua nyingine Tanzania imetangaza kufungua Ubalozi wake nchini Uturuki na hivi leo Mhe. Rais atamwapisha Balozi Mteule, Prof. Elizabeth Kiondo atakayetuwakilisha Uturuki.
 
Pia kumekuwa na ziara za viongozi wakuu wa kitaifa wa nchi hizi mbili ikiwemo ziara ya Rais mstaafu wa Uturuki, Mhe. Abdullah Gul  nchini mwaka 2009 ; ziara ya Rais wa Awamu ya Nne wa Tanzania, Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete nchini Uturuki mwaka 2010 na ziara ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Ali Mohamed Shein mwaka 2011.
 
Tume ya Pamoja ya Biashara
Tanzania na Uturuki zinashirikiana pia kupitia Tume ya Pamoja ya Biashara ambayo ilianzishwa baada ya kusainiwa kwa Mkataba wa Ushirikiano kwenye masuala ya Biashara mwaka 2010. Kikao cha kwanza cha Tume hiyo kilifanyika Jijini Dar es Salaam mwezi Novemba 2012. Katika kikao hicho pande zote zilikubaliana kushirikiana kwenye maeneo mbalimbali hususan biashara na uwekezaji, elimu, Kilimo, Nishati na Madini, Maendeleo ya viwanda na mawasiliano ya simu.

Kikao cha Pili cha Tume ya Pamoja ya Biashara kati ya Tanzania na Uturuki kilifanyika tarehe 11 – 12 Januari 2017, Uturuki kwa lengo la kujadili utekelezaji wa Makubaliano ya Kikao cha Kwanza na kuibua maeneo mapya ya ushirikiano kati ya pande hizi mbili. Aidha, Mkutano huu pia ulikuwa na umuhimu wa kipekee kwa kuwa ulifanyika ikiwa ni maandalizi ya ziara ya Kiserikali ya Mheshimiwa Recep Tayyip Erdoğan, Rais wa Jamhuri ya Uturuki inayotarajiwa kufanyika tarehe 23 Januari, 2017.

Pande zote mbili zimekubaliana kuongeza nguvu katika kuhamasisha uwekezaji kwenye nchi zetu. Katika kutekeleza hili, Uturuki imepanga kuandaa Mkutano wa Uwekezaji kati ya Tanzania na Uturuki ndani ya robo ya pili ya mwaka huu jijini Istanbul. Vile vile, nchi zote mbili zimekubaliana kubadilishana taarifa za fursa za uwekezaji kupitia Balozi zetu na Baraza la Biashara la Tanzania na Uturuki.

Aidha, Taasisi zetu za Uwekezaji zimeelekezwa kuanza majadiliano ya kuingia Mkataba wa Ushirikiano ili kuhamasisha uwekezaji nchini. Hali kadhalika, Uturuki imemchagua Mwambata wa Biashara katika Ubalozi wao wa Dar es Salaam na Tanzania imeahidi kuteua Afisa Maalum ndani ya mwezi mmoja kushughulikia uhamasishaji wa uwekezaji na biashara kati ya nchi hizi mbili.

Mafanikio yaliyopatikana kutokana na ushirikiano kati ya Tanzania na Uturuki

Tangu kuanzishwa kwa Tume ya pamoja ya ushirikiano ya kiuchumi mafanikio ya ushirikiano baina ya nchi hizi mbili yameonekana ikiwemo:- Kuimarishwa kwa ushirikiano katika masuala ya Usafiri wa Anga ambapo Shirika la Ndege la Uturuki lilianzisha safari tatu  za moja kwa moja kutoka Istanbul hadi Dar es Salaam, Kilimanjaro na hivi karibuni Zanzibar. Kuanzishwa kwa safari hizi kumekuza biashara kati ya Uturuki na Tanzania  ambapo mwaka 2009  ukubwa wa biashara ulikuwa Dola za Marekani milioni 66 sawa na shilingi bilioni 145.2 lakini hadi kufikia Februari 2016 biashara kati  ya nchi hizi mbili iliongezeka kwa Dola za Kimarekani milioni 160 sawa na shilingi bilioni 352.

Aidha, kuzinduliwa kwa Baraza la Biashara kati ya Tanzania na Uturuki mwaka 2013 ambalo kumewezesha kuimarisha ushirikiano wa sekta binafsi za nchi hizi mbili na  Kuongezeka kwa Makampuni ya Uturuki yaliyowekeza nchini ambapo hadi sasa ni Kampuni 30 zimefanya uwekezaji wenye thamani ya Dola za Kimarekani milioni 305.08 na zinatarajiwa kutengeneza ajira 2,959.


Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, 
Dar es Salaam
20 Januari, 2017

January 21, 2017

Rais na Mkurugenzi Mtendaji wa Makampuni ya Mohammed Enterprises Tanzania Limited (MeTL Group), Mohammed Dewji ametangazwa na Jarida la African Leadership kuwa mshindi wa tuzo ya African Leadership Magazine Person of the year 2016 baada ya kuibuka mshindi katika kinyang’anyiro kilishohusisha watu nane.
MO Dewji ambaye ni Mtanzania anayejihusisha na biashara kupitia kampuni yake ya MeTL Group na kusaidia jamii kupitia Taasisi ya MO Dewji ameibuka mshindi kwa kupata asilimia 60.8 ya kura zote zilizopigwa akifuatiwa na Rais mstaafu wa Ghana, Dramani Mahama ambaye alipata asilimia 30.2.
Wengine waliowania tuzo hiyo ni Strive Masiyiwa, Chris Kirubi, Akinwumi Adesina, Cyril Ramaphosa, Atiku Abubakar na Aisha Mohammed.
Akizungumza kuhusu MO Dewji, Mjumbe wa Bodi ya Ushauri wa Jarida la African Leadership, Joe Beasley amemtaja MO Dewji kama mtu ambaye anaumuhimu mkubwa kutokana na dhamira yake ya kusaidia bara la Afrika kupunguza tatizo la ukosefu wa ajira kwa kutoa nafasi nyingi za kazi.
“Dhamira ya Dewji ni kutengeneza ajira jambo ambalo ni kiini cha tatizo kubwa linalokabili Afrika la ukosefu wa ajira … kupitia biashara zake amesaidia kupunguza ukosefu wa ajira, kupata utajiri na kutoa ajira kwa vijana ambao hawana ajira barani [Afrika],” alisema Beasley.
Mohammed Dewji anakuwa mshindi wa tuzo hiyo kwa mwaka 2016 ambapo kwa mwaka 2015 ilichukuliwa na Rais Mstaafu wa Nigeria, Goodluck Jonathan.

January 19, 2017

ABOUTRIKA AORODHESHWA KAMA GAIDI MISRIMohamed Aboutrika
0
Kiungo mshambuliaji wa zamani wa klabu ya Al Ahly na Misri, Mohamed Aboutrika ameongezwa kwenye orodha ya magaidi nchini Misri kufuatia kutuhumiwa kuwa na uhusiano na kikundi cha Muslim Brotherhood kilichopigwa marufuku.
Aboutrika anatuhumiwa kukifadhili kikundi cha Brotherhood kinachotafsiriwa kama kundi la kigaidi nchini Misri. Katika uchaguzi wa mwaka 2012, Aboutrika alimpendekeza mgombea wa Brotherhood, Mohamed Morsi ambaye alishinda  urais na kudumu kwa kipindi cha mwaka mmoja kabla ya kung’olewa madarakani na kuorodheshwa kwenye orodha ya magaidi nchini humo.
Aboutrika pia amekuwa akiunga mkono nchi ya Palestina na kuvaa fulana za kuwaunga mkono raia wa nchi hio katika vuguvugu dhidi ya Israel

Aboutrika akionesha fulana ya kuwaunga mkono raia wa Gaza 

Wakili wa Aboutrika, Mohamed Osman amesema Aboutrika ameorodheshwa kama gaidi licha ya kutofikishwa mahakamani wala kujulishwa kutuhumiwa.
”  Tutakataa rufaa kupinga haya maamuzi,” Amenukuliwa Osman huku Aboutrika mwenyewe akikana tuhuma hizo.
SOURCE: SOKA 360

Popular Posts

WADAU

BLOG ZINGINE