Wawakilishi 35 wa bunge la nchini Iraq, ambao wanatilia shaka muungano
wa kimataifa kwa ajili ya kupambana na kundi la kitakfiri na kigaidi la
Daesh, wametaka kuundwa tume ya uchunguzi kwa ajili ya kufuatilia
mwenendo wa muungano huo. Mwaka jana magaidi wa kitakfiri wa Daesh
wanaoshirikiana na wanachama wa Kibaathi nchini humo, waliudhibiti mji
wa Mosul ulioko katika mkoa wa Nainawa, baada ya kuushambulia mji huo.
Baada ya kuudhibiti mji huo na miji mingine ya karibu, matakfiri hao
walitekeleza vitendo vya kikatili na vya kutisha dhidi ya binaadamu.
Moja ya vitendo hivyo ni ukatili dhidi ya watu wa jamii ndogo ya
Kiyazidi nchini humo.
humo. Jinai za kundi hilo la Daesh zikiwemo zile za raia wa mji wa
Kobani nchini Syria, ziliifanya Marekani ambayo mwaka 2011 iliondoa
askari wake nchini Iraq, kwa mara nyingine ipate sababu ya kurejesha
askari hao nchini humo kwa kisingizio cha eti kuwasaidia raia hao
wachache wa Yazidi. Marekani kwa kushirikiana na zaidi ya nchi 40
waungaji mkono wake, iliunda muungano huo wa kimataifa dhidi ya kundi
hilo la kitakfiri la Daesh ambalo lilianzishwa na Marekani yenyewe hapo
mwezi Septemba mwaka jana. Licha ya kwamba Washington ilitangaza kuwa
lengo la muungano huo ni kuendesha vita dhidi ya Daesh, lakini mienendo
ya muungano huo wa kimataifa katika kipindi cha miezi minne iliyopita,
inaonyesha kwamba lengo lake kuu si jingine ghairi ya kutekeleza njama
zake nchini Iraq na Syria. Kwa upande mwingine ni kwamba, kutokana na
Marekani na nchi za Magharibi kushindwa kuchukua hatua zozote za maana
kuhusiana na jinai za wazi dhidi ya binaadamu, za kivita na zilizo dhidi
ya usalama zilizotendwa na kundi hilo la kitafiri mbele ya vyombo vya
sheria, nchi hizo zimejikuta chini ya mashinikizo makubwa. Ni kwa ajili
hiyo, ndipo Marekani na waungaji mkono wake wa Kimagharibi sanjari na
misaada ya udiplomasia wa dola zinazotokana na mafuta ya baadhi ya nchi
za Kiarabu, wakaamua kuunda muungano huo wa kimaonyesho wa kimataifa
dhidi ya kundi la Daesh, ili kwa njia hiyo waweze kupunguza mashinikizo
ya walimwengu kuhusiana na kadhia hiyo. Aidha mbali na hapo ni kwamba,
kwa kipindi chote cha miaka minne iliyopita Marekani na waungaji mkono
wake wa Kimagharibi na Kiarabu, wamekuwa wakitoa uungaji mkono wa kila
upande kwa makundi ya kigaidi nchini Syria, suala ambalo limetia wasi
wasi mkubwa na kuilazimu serikali ya Rais Bashar al-Assad wa nchi hiyo
kuzidisha mapambano dhidi ya makundi hayo ya kigaidi. Wasi wasi huo
umeuondolea imani muungano huo wa kimataifa dhidi ya Daesh unaoongozwa
na Marekani na kuwafanya watu waamini kwamba, lengo lake kuu ni kujaribu
kulidhoofisha kwa muda mfupi tu kundi hilo na sio kuliangamiza kabisa.
Ni kwa kuzingatia suala hilo, ndipo viongozi wa Iraq akiwemo Haider
al-Abadi, Waziri Mkuu wa nchi hiyo wakakosoa mwenendo wa muungano
uliotajwa, na kuamini kuwa mwendo wa muungano huo wa kimataifa dhidi ya
Daesh ni kinyume na stratijia za serikali kuu ya Baghdad katika
kukabiliana na kundi hilo la kigaidi. Matukio ya kiusalama nchini Iraq
yanaonyesha kwamba, kudhoofika kwa makundi ya kigaidi nchini humo
kumetokana na ushirikiano wa serikali ya nchi hiyo na wananchi, na wala
sio mashambulizi ya muungano huo wa kimataifa unaoongozwa na Marekani.
0 MAONI YAKO:
Post a Comment