Mawaziri wote wa baraza la mawaziri nchini Tanzania wamezuiwa kusafiri
kikazi nje ya Jiji la Dar es Salaam kutokana na kile kinachoelezwa ni
maandalizi ya kukabidhi ofisi kwa mawaziri wapya ambao wanatarajiwa
kutangazwa wakati wowote kuanzia sasa. Taarifa hizo zimekuja siku moja
tu tangu Ikulu kupitia kwa Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu,
Salvatory Rweyemamu, kuwataka Watanzania kuwa na subira kwa kuwa Rais
Jakaya Kikwete wakati wowote kuanzia sasa atatoa uamuzi dhidi ya tuhuma
zinazomkabili Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo.
Profesa Muhongo na baadhi ya viongozi wengine wa Serikali,
wanahusishwa na sakata la uchotwaji wa zaidi ya Sh bilioni 300 kwenye
akaunti ya Tegeta Escrow. Taarifa zaidi zinasema kuwa, mawaziri wote
sasa wamezuiwa kusafiri nje ya Dar es Salaam kutokana na kusubiri
mchakato huo wa kukabidhi ofisi. Vyanzo hivyo viliongeza kwamba tayari
Rais Kikwete amekwishamaliza mchakato wa uteuzi wa baraza jipya la
mawaziri, akiwa nchini Uswisi katika Mkutano wa Jukwaa la Uchumi la
Dunia. Mrengo wa upinzani nchini Tanzania umekuwa ukisisitiza juu ya
kufutwa kazi mawaziri wote waliohusika katika sakata la Escrow.
Chanzo:idhaa ya kiswahili Iran
0 MAONI YAKO:
Post a Comment