Na Richard Bakana, Dar es salaam
MSHAMBULIAJI wa klabu ya Yanga na Timu ya Taifa ya Tanzania,
Taifa Stars, Mrisho Ngassa, amejutia uamuzi wake wa kukataa kujiunga na
El Merreikh ya Sudan akisema kuwa yalikuwa ni mapenzi yake makubwa
kuichezea Yanga.
Akiongea na Shaffihdauda.com
baada ya mchezo wa jana alipoibuka shujaa kwa kuifungia Yanga bao 2-0
dhidi ya Mtibwa Sugar, Ngassa alisema kuwa baada ya kugundua alifanya
makosa makubwa kuwagomea Simba na Azam FC ambao ndio walitaka kumpeleka
El Merreikh, alipofunga mabao hayo alilazimika kuwaomba msamaha
mashabiki kwa uamuzi ambao sasa anaujutia.
“Nilifanya makosa kutokwenda El
Merreikh ndio maana hata leo nilipofunga magoli ilibidi niombe msamaha
kwa sababu Simba na Azam walitaka kunipeleka El Merreikh, Nilifanya kama
kuwakosea na kwasababu nilikuwa naipenda Yanga ilibidi niichezee”
Amesema Ngassa kwa hari ya uchungu ajijuta kosa alilofanya katika maisha
yake la kukataa kwenda kucheza mpira wa kulipwa nchini Sudan.
Katika msimu wa 2013/2014 Ngassa
alijiunga na Yanga akitokea Simba alikokuwa akicheza kwa mkopo akiwa ni
mali ya Azam FC, Katika uamisho huo TFF iliamuru awalipe Simba kiasi cha
Tsh. Milioni 30 kama pesa ambayo walimsajilia kutoka Azam FC pamoja na
Tsh. Milioni 15 kama fidia baada ya kugundulika alikuwa amesajiliwa timu
mbili zaidi ya hapo TFF ilikuwa imepanga kumfungia endapo asingelipa
deni hilo.
Kufatia Yanga kuonyesha nia ya
dhati ya kutaka huduma ya kiungo huyo ambaye amewahi kufanya majaribio
kunako klabu ya West Ham ya Uingereza, Uongozi wa Mwenyekiti Manji
uliamua kumlipia deni hilo kwa makubaliano kuwa atakuwa akikatwa kiasi
cha Tsh Laki tano katika kila mshahara wake wa mwezi na ikawa hivyo
kweli.
Ngassa ambaye kwa sasa amebakiza
mkataba wa miezi mitano Jangwani, ameuambia mtandao huu kuwa makubaliano
hayo yamevunjwa na sasa anamiezi miwili hapokei mshahara kwa kuwa
wanaukata wote.
“Hadi sasa hivi nakatwa, Mshahala
wenyewe sipewi,Nacheza tu kwasababu namaliza muda wangu lakini
namshukuru Mungu yeye ndio anajua la mbele, Walisema watanikata laki
tano, wakaja wakaanza kunikata milioni na baada ya hapo wakaanza kukata
yote inamaana hadi hapa mshahara wa miezi miwili sijapewa kwahiyo siwezi
kuidai timu” Amesema Ngassa ambaye ni Mfungaji bora wa kombe la
Shirikisho barani Afrika mwaka jana.
Akizungumzia namna alivyoifunga
Mtibwa Sugar hapo jana, Ngassa anasema kuwa Kocha Hans Van De Pluijm
alimuambia asitoke katikatika ya mabeki wawili wa wapinzani wao ambao
walionekana kuwa wazito kukimbia.
“Mwalimu aliniambia kwamba wale
mabeki wa kati ni wazito ndio nikazitumia nvyema nafasi, sikuweza kutoka
pale katikati” Amesema Ngassa.
Kwa upande wake Kocha Hans Van De
Pluijm amesema kuwa udhaifu wa mabeki wa kati wa Mtibwa Sugar aliuona
katika kipindi cha kwanza ndio maana aliamua kumuingiza Ngassa mwenye
kasi kubwa.
“Kitu muhimu ni kuwa alitakiwa
kutumia fursa alizozipata kwasababu nilijua kuwa toka kipindi cha
kwanza kuwa mabeki wawili wa kati hawakuwa haraka, kwahiyo ninafurahia
matokeo tuliyopata” Amesema kocha huyo aliokuwa akiongea na
shaffihdauda.com.
0 MAONI YAKO:
Post a Comment