Kuuliwa vijana watatu wanachuo wa Kiislamu katika jimbo la
Carolina Kaskazini nchini Marekani ni kitendo kinachopaswa kulaaniwa na
ni kiashiria kingine cha hatari kubwa ya kuenea kwa vitendo vya ukatili
na uchupaji mipaka. Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran
jana alituma ujumbe na kulaani kuuliwa vijana watatu wanachuo wa
Kiislamu katika jimbo moja nchini Marekani na kueleza masikitiko yake na
kutoa mkono wa pole kwa familia za wahanga wa jinai hiyo, jamii ya
Waislamu wa Marekani na wapigania uhuru wote na watetezi wa haki za
kibinadamu. Rais wa Iran amesema kuwa inatarajiwa kuwa viongozi husika
watafanya juhudi zote za lazima kwa ajili ya kulinda haki za raia wote
ikiwemo za Waislamu.
Sehemu moja ya ujumbe wa Rais wa Iran inasema kuwa: Ni
jambo lenye kutia wasiwasi mno kutokana na ripoti za awali kuonyesha
kwamba sababu ya jinai hiyo ni chuki dhidi ya dini na uadui dhidi ya
Uislamu; lakini ukweli ni kwamba wale wanaopanda mbegu za chuki dhidi ya
dini na hofu juu ya Uislamu, kwa kutaka au kutokutaka wanaeneza vitendo
vya ukatili katika jamii.
Jinai hiyo imetokea huku vyombo vya habari vya Magharibi
vikiendelea kuonyesha mshikamano wao kwa wahanga wa jarida la kila wiki
la Charlie Hebdo la nchini Ufaransa, hata hivyo hatua hizo za kulaani
hazijaweza kufichua ukweli wa mambo; ukweli ambao utaonyesha ni nini
hasa chanzo na chimbuko la vitendo hivyo vya ukatili na uchupaji mipaka;
na ni fikra gani zilizoko nyuma ya pazia na zinazoongoza harakati ya
hofu na chuki dhidi ya Uislamu?
Baada ya tukio la kushambuliwa ofisi ya jarida la Charlie
Hebdo ambalo liliumiza hisia za Waislamu kwa kuchapisha vibonzo
vinavyomdhalilisha Mtume Mtukufu (saw); vyombo vya habari vya Magharibi
vilielekeza mashambulizi yake kwa Uislamu na Waislamu na kulitaja tukio
hilo kuwa ni nembo ya fikra za Waislamu; bila hata ya kuashiria
chimbuko la vitendo vya kufurutu ada vilivyosababisha kuenea kwa itikadi
za Kidaesh na al Qaida. Amma haukupita muda ambapo ni hivi majuzi tu
raia mmoja wa Marekani amewauwa wanachuo watatu Waislamu nchini humo,
huku duru za habari za Magharibi na za ndani ya Marekani zikiifumbia
jicho jinai hiyo kwa kutotoa radiamali yoyote ya maana. Hata hivyo
huwenda katika jami iliyojaa misuguano ya Magharibi, matukio mengi kama
haya yakafutika haraka katika fikra za waliowengi, lakini yakiendelea
kubaki katika historia. Marwa el Sherbini, mwanamke wa Kiislamu
aliyekuwa akivaa vazi la stara la hijabu raia wa Misri ni mmoja wa
wahanga hawa ambaye tarehe 8 mwezi Julai mwaka 2008 aliuliwa kwa
kucharangwa visu mara 18 na mwanaume mmoja Mjerumani katika mahakama
moja nchini Ujerumani huku mumewe na mwanae wakishuhudia hayo kwa macho
yao. Bi Sherbini alikuwemo ndani ya mahakama hiyo kama mlalamikaji ili
kuwasilisha mashtaka yake dhidi ya mwanaume huyo Mjerumani kwa kosa la
kumshambulia na kumdhalilisha. Muuaji huyo wa Kijerumani awali alikuwa
amemuita gaidi bi Marwa Sherbini katika bustani moja nchini humo na
kisha akamshambulia na kumvua hijabu yake kichwani. Mwanaume huyo
Mjerumani alihukumiwa na mahakama moja ya mwanzo ya Ujerumani kulipa
faini ya yuro 750, hata hivyo mtuhumiwa huyo alimuuwa mwanamke huyo
Mmisri aliyekuwa mjamzito kwa kumcharanga kisu mara 18, wakati wa
kusikilizwa kesi iliyokuwa ikimkabili. Kifo cha mwanamke huyo wa
Kiislamu kiliacha athari nyingi katika fikra za waliowengi na kuibua
maandamano makubwa ya kupinga ubaguzi na chuki dhidi ya dini Tukufu ya
Uislamu. Tab’an radiamali iliyoonyeshwa na vyombo vya habari vya
Magharibi ilikabiliwa na ukosoaji mkubwa wa fikra za waliowengi duniani.
Vyombo vya habari vya Magharibi viliakisi kwa upana zaidi tukio la
kushambuliwa ofisi ya jarida la Charlie Hebdo ikilinganishwa na namna
vilivyoitangaza habari ya kuuliwa vijana watatu wa Kiislamu wanachuo
huko Marekani. Wakuu wa nchi nyingi duniani hasa wa Magharibi walilaani
tukio la kushambuliwa ofisi ya gazeti la Charlie Hebdo nchini Ufaransa,
lakini hakuna yeyote kati yao aliyeashiria na kulaani jinai ya Chapel
Hill. Moja ya nukta muhimu ilikuwa hii kwamba, viongozi wengi wa nchi za
Magharibi na nyengine za kigeni ambao walionekana katika safu ya kwanza
ya maandamano ya kuonyesha mshikamano na wahanga wa mashambulizi ya
Paris, wenyewe ni miongoni mwa waungaji mkono wakubwa na waasisi wa
ugaidi. Kioja ni kwamba hata Benjamin Netanyahu, Waziri Mkuu wa utawala
mtenda jinai wa Kizayuni vile vile alikuwa katika safu ya mbele ya
viongozi walioandamana huko Paris.
Ni kwa kuzingatia undumakuwili huo wote na uhakika huu
mchungu ndipo Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran akaandika katika
ujumbe wake kwamba: Inatarajiwa kuwa viongozi watafanya jitihada zote za
lazima kwa ajili ya kulinda haki za raia wote wakiwemo Waislamu, na
akaongeza kwa kueleza kwamba: Wakati umefika sasa wa kuanzisha harakati
ya ulimwengu mzima kwa ajili ya kupambana na utumiaji mabavu na vyanzo
vya kiutamaduni vya uenezaji chuki dhidi ya dini na uhalifu unaotendwa
kutokana na chuki kwa kuwashirikisha wanafikra wote, wasanii, maulamaa
wa kidini, jumuiya za kiraia na serikali, ili kuivua jamii ya kimataifa
na aibu hii katika karne ya ishirini na moja.
0 MAONI YAKO:
Post a Comment