Mkuu wa mkoa wa Mwanza, Magesa Mulongo, amesema watu wote waliohusika
‘kuiba’ mtoto mwenye ulemavu wa ngozi (albino) Pendo Emmanuel (4) katika
kijiji cha Ndami wilayani Kwimba, Mwanza, wamekamatwa.
Akizungumza
wakati akiwaapisha wakuu wapya wa wilaya wa mkoa huo jana, Manju
Msambya (Misungwi), Zainab Rajab (Sengerema) na Pili Moshi (Kwimba),
Mulongo alisema watu wote waliohusika wamekamatwa na hivi sasa bado
hawafahamu kama mtoto huyo yupo hai ama mfu.
“Wezi wale baada ya kumuiba mtoto Pendo walimleta katika hoteli moja
hapa jijini Mwanza, kisha kuwakabidhi watu walionekana wanunuzi, lakini
wote hao wamekamatwa akiwamo mmiliki wa hoteli hiyo,” alisema Mulongo.
Alisema serikali ipo kazini wakati wote, ndiyo maana inafanya kazi
usiku na mchana kuwasaka watu wote waovu mkoani Mwanza ambao hawawezi
kusalimika kwa kile watakachokifanya.
Hata hivyo, alisema watu hao waliofanya uhalifu huo akiwamo baba wa
mtoto huyo, Emmanuel Shilinde, wanashikiliwa na polisi huku mtu wa
mwisho aliyetoweka na mtoto huyo toka hotelini hapo akiendelea
kutafutwa.
Mulongo hata hivyo hakuweza kuitaja hotel wala mmiliki wake na
wangine waliohusika na tukio hilo lilitokea Desemba 27 mwaka jana,
lakini Shilinde akituhumiwa kuhusika zaidi na tukio hilo kutokana na
kuamua kufanya hivyo kwa sababu alikuwa ana watoto wawili albino.
Mkuu wa mkoa huyo aliwataka wakuu wa wilaya wapya, kuhakikisha
kushughulikia changamoto za wapiga ramli, kuangalia utoaji wa vibali kwa
waganga wa jadi ili kudhibiti matyukio ya utekaji na mauaji ya albino.
Hata hivyo, alishangazwa na maneno yanayotolewa na watu kuhusiana na
mauaji hayo kuwa yanatokana na masuala ya kisiasa kuelekea uchaguzi
mkuu.
Katibu wa chama cha maalbino mkoa wa Mwanza, Mashaka Tuju,
aliishutumu serikali kwa kushindwa kuchukua hatua stahili tangu mauaji
ya watu wenye ulemavu wa ngozi (albino) yalipoanza miaka tisa iliyopita.
Amesema kwa miaka tisa serikali inahangaika na kudai inachukua hatua
lakini hakuna hatua yoyote inayoonekana mpaka sasa huku albino wengi
wakiwa wanaishi vijijini katika nyumba zisizo na ulinzi thabiti, lakini
utakuta viongozi wa serikali wanaenda huko pale linapotokea tatizo la
mauaji ya watu hao.
Tuju amewashambulia mwenyekiti wa CCM mkoa wa Mwanza, Antony Diallo,
naibu waziri wa nishati na madini, Charles Kitwanga na mbunge wa Magu,
Dk. Festus Limbu, kwa kushindwa kufanya juhudi zozote za kuwalinda na
kuwatetea albino.
Katika kipindi cha miezi miwili, watoto Pendo Emmanuel wa Kwimba na
Yohana Bahati (mwaka mmoja) wa kijiji cha Ilelema Chato, walitekwa na
watu wasiojulikana.
0 MAONI YAKO:
Post a Comment