June 20, 2015

 Mwenyekiti wa maofisa watendaji wakuu wa makampuni, Ali Mufuruki (Kushoto) akiangalia kitabu cha Azimio la Tabora alilokabidhiwa na kiongozi wa Chama cha ACT Wazalendo, Zitto Kabwe (wa pili kushoto) baada ya kumalizika kwa mdahalo kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2015. Wengine ni Mwenyekiti wa NLD, Emmanuel Makaidi na Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahimu Lipumba
Dar es Salaam. Viongozi wa vyama vya siasa vya CUF, NCCR-Mageuzi, NLD na ACT-Wazalendo wameitupia lawama Serikali kwa kushindwa kutekeleza maagizo yanayotolewa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).
Wakizungumza kwenye mdahalo wa Uchaguzi Mkuu mwaka 2015 kuhusu masuala ya Sera juzi jijini Dar Es Salaam viongozi hao Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba, Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia, Mwenyetiki wa NLD, Dk Emmanuel Makaidi na Kiongozi wa ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe walisema kuwepo kwa mfumo mbovu serikalini na kukithiri kwa rushwa ndiyo chanjo cha kupuuzwa kwa ripoti za CAG.
Kwa mujibu wa ripoti ya ukaguzi maalumu wa miaka mitano ya ufuatiliaji wa utekelezaji wa mapendekezo ya CAG, imeeleza bayana kumekuwepo na ufisadi wa takribani Sh600 bilioni zilizochotwa katika matumizi mbalimbali ambayo hayana maelezo ya kutosha.
Ripoti hiyo maalumu inaonyesha kuwa uovu huo umekuwa ukiwezekana kutokana na mapendekezo ya CAG ya kuziba mianya ya upotevu wa fedha, kutofanyiwa kazi.
Akifungua mdahalo huo, Mwenyekiti wa Umoja wa Maofisa Watendaji Wakuu wa Kampuni Binafsi nchini (CEOrt), Ali Mufuruki alisema kuwa awali mdahalo huo uliwalenga wagombea kiti cha urais, lakini kwa kuwa wengi walishindwa kushiriki kwa sababu mbalimbali, sasa utaitwa mdahalo wa uchaguzi mkuu kuhusu sera.
“Ni matumaini yetu kuwa kushiriki mdahalo kwa njia hii kutaleta ujumbe ule ule tuliokuwa tumeukusudia kutoka kwa waliotangaza nia, ambapo masuala ya uchumi, utawala bora na utawala wa sheria yatakuwa msingi wa mazungumzo,” alisema Mufuruki.
Akijibu swali kuhusu kupuuzwa kwa ripoti za CAG, Zitto alisema kuwa ili kazi ya CAG iwe bora ni vyema idara za Polisi, Mwendesha Mashtaka wa Serikali (DPP) na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) zishirikishwe katika kuchukua hatua zinazostahili.
“Kuijadili ripoti ya CAG pekee yake haitoshi. Tatizo hili linatokana na kuwepo kwa mfumo wa kuiwajibisha Serikali, wananchi wanahitaji wafahamu wabunge wanatakiwa kuunda kamati nzuri ya kukagua hesabu za serikali,”alisema Zitto.
Kwa upande wake Mbatia alisema ripoti za CAG zimekuwa zikiibua madudu yanayofanya Serikalini lakini hakuna mhusika anayechukuliwa hatua yoyote. Akitolea mfano, alisema kuwa fedha zilizotajwa na CAG kupotea mwaka zikigawanywa kila mstaafu anayeidai Serikali angelipwa Sh800, 000.
Mbatia alisema ‘dawa’ ya kuidhibiti serikalini bungeni ni kwa kuhakikisha kuwa hakuna chama kinachokuwa na zaidi ya asilimia 40 ya wabunge wote. Alisema kwa kufanya hivyo, wabunge watakuwa na nguvu ya kutoa maamuzi ya pamoja.
“Jiulize kwanini mapato yasiyo ya kodi yanazidi kushuka wakati bajeti inazidi kuongezeka. Hakuna nidhamu ya matumizi, hii ya kutengeneza bajeti ni kuwadanganya Watanzania,” alisema Mbatia.
“Nafikiria kwa hali ilivyosasa tuweke watu ambao si wala rushwa na kupunguza nguvu ya CCM. Ndani ya Bunge watu wanapokea rushwa hawawezi kutekeleza ripoti ya CAG,” alisema Makaidi na kuongeza kuwa hata bajeti zinazoandaliwa bungeni huanza ‘kutafununwa’ siku ya pili baada ya kupitishwa kutokana na kukithiri kwa rushwa.

0 MAONI YAKO:

Post a Comment

Popular Posts

WADAU

BLOG ZINGINE