Balozi Seif
akizungumza na baadhi ya Wananchi mara ya kukabidhiwa Vijana Sita
walioamua kuachana na matumizi ya Dawa za kulevya waliokuwa wakipata
mafunzo kwenye Kituo cha Mombasa nje kidogo ya Mji wa Zanzibar. Kushoto
ya Balozi Seif ni Sheha wa Shehia ya Fujoni Bwana Said Mgeni Bakari na
wa kwanza kutoka kushoto ni Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Kaskazini “ B “
Nd. Hilika Khamis na Mke wa Mbunge wa Jimbo la Kitope Mama Asha Suleiman
Iddi.
Na Mwandishi Wetu.
Wazazi wameaswa kuwa tayari
kuwapokea Vijana au watoto wao walioamua kuacha matumizi ya dawa za
kulevya ili kuwalinda na vishawishi vinavyoweza kutoa nafasi ya
kuwarejesha tena kwenye matumizi ya Dawa hizo pamoja pombe haramu.
Mbunge wa Jimbo la Kitope Balozi
Seif Ali Iddi ametoa wosia huo wakati wa kuwapokea Vijana Sita wa Kijiji
cha Fujoni walioamua kuacha kutumia Dawa za kulevya na kupata mafunzo
watakayoyatumia kuwasomesha wenzao kuachana na Dawa hizo hapo katika
Skuli ya Fujoni Wilaya ya Kaskazini “ B “.
Balozi Seif ambae pia ni Makamu
wa Pili wa Rais wa Zanzibar alisema wapo Wazazi na Familia Nchini ambao
bado wanaendelea na tabia ya kuwatenga Vijana wao walioathirika na
Dawa za kulevya kwa kuchelea kufanyiwa matendo ya maudhi kama wizi.
Alisema tabia hiyo inafaa kuachwa
kwa vile kama haikutafutiwa ufumbuzi inaweza kuzalisha zaidi Vijana
wanaotumbukia katika matumizi ya Dawa za kulevya na hatimae kuwa na
kundi kubwa la walevi ndani ya Jamii ambao ni nguvu kazi ya Taifa.
Balozi Seif alionyesha furaha
yake kutokana na ujasiri mkubwa ulioonyeshwa na vijana hao wa kuamuwa
kuacha matumizi ya Dawa za kulevya na kujitolea kuwa mfano kwa wenzao
wenye tabia hiyo.
Wakati huo huo Mbunge huyo wa
Jimbo la Kitope Balozi Seif ameukabidhi Uongozi wa Mamlaka ya Maji
Zanzibar { ZAWA } shilingi Milioni 5,000,000/- kwa ajili ya kukamilisha
ujenzi wa Kibanda cha Maji katika Kijiji cha Kinduni.
Ujenzi wa Kibanda hicho una lengo
la kuimarisha miundo mbinu ya upatikanaji wa huduma za Maji safi na
Salama ndani ya Kijiji hicho chenye changamaoto ya upatikanaji wa huduma
hiyo muhimu.
Mbunge wa
Jimbo la Kitope ambae pia ni Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi
Seif akisalimiana na mmoja kati ya Vijana sita walioamua kuachana na
matumizi ya Dawa za Kulevya katika Kijiji cha Fujano hapo katika Viunga
vya vya Skuli ya Fujoni. Kati kati yao ni Mwakilishi wa Umoja wa
kusaidia mapambano dhidi ya matumizi ya Dawa za kulevya na Pombe
Tanzania Bwana Abdulrahman Mohammed Abdulla.
Mwakilishi
wa Umoja wa kusaidia mapambano dhidi ya matumizi ya Dawa za kulevya na
Pombe Tanzania Bwana Abdulrahman Mohammed Abdulla akielezea mikakati ya
taasisi yake katika mapambano dhidi ya Dawa za kulevya hapa Nchini.
Chanzo Mo Blog
0 MAONI YAKO:
Post a Comment