July 05, 2015

Ndugu Wanadar es salaam
Kwanza nianze kwa kutoa shukran kwa kuitikia wito wetu wa kujitokeza kwa wingi kuja kutusikiliza leo hii katika Viwanja hivi vya Mwembeyanga, TUNAWASHUKURU SANA.

Kwetu nyie mna umuhimu wa kipekee, maana mnatokea katika Jiji ambalo misingi ya ujenzi wa Taifa hili ilianzia, kuanzia kuasisiwa kwa Chama cha Tanganyika African Association mpaka harakati za Chama hicho cha Kijamii kurithiwa na Chama cha Siasa za TANU.

Siku zote historia inawaonyesha watu wa Dar es salaam kuwa ndio waasisi wa harakati hizi za siasa za kizalendo nchini. Kutokea nyakati zile za kina Mwalimu Nyerere, Bibi Titi Mohammed, kina Sykes, Dossa Aziz Ally, John Rupia na Zuberi Mtemvu mpaka leo bado wanadar es salaam mnao umuhimu wa kipekee katika siasa za nchi hii. Kwa kutambua umuhimu wenu huo, tumeona leo tufanye Mkutano huu Maalum viwanjani hapa ili kukitambulisha tena chama hiki kwenu, na pia kukikabidhi mikononi mwenu ili harakati hizi za kurudisha misingi ya Uzalendo wa Taifa hili mzishike nyie wenyewe waasisi wa harakati husika.

Na hili tunalolifanya leo si jambo geni kwenu, labda niwakumbushe tu, ni kwa huo umuhimu wenu Rais wetu wa kwanza na baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere alijenga Utamaduni wa kuzungumza na Taifa juu ya mambo yote mazito ya nchi hii kupitia wazee wetu wa Jiji hili, utamaduni ambao umeendelea kurithiwa, nasi tunaona ni utamaduni mwema wa kuuendeleza. Japo sisi tunakwenda mbele zaidi, kwamba tumekuja kwenu Vijana, Wanawake na Wazee wetu wa Dar es salaam kuzungumza nanyi juu ya jambo hili zito, kukikabidhi kwenu chama chetu cha ACT Wazalendo.

Ndugu Wanadar es salaam

Tumewaiteni leo tukiwa na mambo Machache Muhimu kwa chama chetu na Taifa kwa ujumla ambayo tungependa kuyaeleza kwenu na kwa Umma wa Watanzania wenzetu kwa ujumla.

Kama mnakumbuka Machi 29 mwaka huu tulizindua chama chetu hapa jijini Dar es salaam na baada ya uzinduzi huo tulifanya ziara katika mikoa 22 na baadhi ya majimbo nchini, pia tokea wakati huo operesheni mbali mbali za chama zimekuwa zikifanyika wakati wote huo, ikiwa ni pamoja na kuzindua Azimio la Tabora – Tamko la Kimuongozo, Kiitikadi, Kisera na Kimaadli la Chama chetu ambalo limehuisha Azimio la Arusha. Tunawashuku sana wananchi wa Mikoa mbalimbali kwa mapokezi yao makubwa waliyotupa pamoja na kulipokea kwao kwa mikono miwili Azimio la Tabora.

Ndugu Wana-Dar es salaam

Tuna uchumi unaojenga Matabaka. Hivi sasa uchumi wetu umeshikwa na watu wachache hususan wafanyabiashara ambao pia wameshika siasa au kwa wao kushiriki kwenye siasa moja kwa moja au kufadhili wanasiasa wa kutetea maslahi yao.

Tuna kansa ya ufisadi ambapo watu hutumia nafasi zao za uongozi kujilimbikizia mali. Ufisadi ni tatizo zaidi la viongozi walioshika madaraka ya umma. Tunahuisha Azimio kwa lengo la kusimika miiko ya Uongozi wa Umma ambayo itakuwa msingi mkuu wa mapambano dhidi ya ufisadi.

Azimio la Tabora kwa kiasi kikubwa linakuja kuleta Mwarobaini wa Kimaadili juu ya suala husika, kwa kuwa linahuisha Azimio la Arusha kwa kurudisha miiko ya Uongozi na Utumishi wa Umma, na pia kujenga misingi ya uchumi wa Ujamaa wa kisasa utakaojikita katika kuongeza uzalishaji mali na ugawaji sawa wa keki ya Taifa na hivyo kupunguza matabaka nchini kwetu.

Ndugu Wanadar es salaam

Mtakumbuka kuwa Mwezi Novemba mwaka 2012 Bunge lilipitisha Azimio namba Tisa la Mwaka 2012 ambalo lilielekeza Serikali kufanya uchunguzi kuhusu Watanzania na makampuni ya kitanzania waliotorosha na kuficha fedha kwenye mabenki ughaibuni. Uchunguzi pia ulikuwa uhusike na Mali za Watanzania zilizopo nje ya nchi katika juhudi za kuhakikisha kuwa fedha chafu na ufichwaji wake vinakomeshwa. Bunge lilitoa muda wa miezi sita kwa Serikali kufanya uchunguzi huo. Mwaka mzima ulipita Serikali haikutoa maelezo yeyote na baada ya kubanwa ndani ya Bunge Serikali ikaomba miezi sita zaidi. Hata hivyo mpaka leo Serikali haijatoa kauli yeyote kuhusu taarifa hiyo ya uchunguzi.

Takwimu zinazohusu fedha za Watanzania nje ya nchi bado sio za uhakika sana. Kwa mfano, Taarifa ya Serikali ya kisiwa cha Jersey kilicho chini ya himaya ya Uingereza inaonyesha kuwa Fedha na Mali za Watanzania katika mabenki kisiwani humo ni paundi za Uingereza 440 milioni ambazo kwa bei ya sasa ni sawa na shilingi za kitanzania 1.4 trilioni. Vile vile taarifa rasmi ya Benki Kuu ya Uswiss inaonesha kuwa Watanzania wenye akaunti katika mabenki ya nchi hizo imefikia dola za kimarekani 304 milioni kutoka dola 213 milioni mwaka 2012. Hatuna takwimu kwa nchi nyingine duniani.

Fedha hizi zaweza kuwa halali ama haramu. Kuna watu ama ni Watanzania wanaishi ughaibuni na kufanya kazi huko ni lazima wawe na akaunti za benki. Pia kuna Watanzania ambao ni wafanyabiashara na masharti ya biashara zao ni lazima wawe na akaunti katika mabenki ya nje. Hata hivyo mfumo mzima wa ufunguaji na ufungaji wa akaunti katika mabenki ya nje umewekewa masharti ya kisheria na kibali cha Benki Kuu kinahitajika. Kuna Watanzania wenye kuficha fedha ambazo zimepatikana kwa rushwa na biashara haramu mbalimbali kama vile madawa ya kulevya na biashara ya nje ambayo haingii kwenye rekodi za Benki Kuu. Iwapo Serikali ingefanya uchunguzi na kuukamilisha tungeweza kujua kwa hakika katika orodha ya watu wenye akaunti nje ni wepi wana fedha zao halali na wepi wana fedha haramu. Serikali imetunyima haki hiyo kwa zaidi ya miaka miwili na nusu sasa. Bunge la Kumi linavunjwa mnamo tarehe 9 Julai mwaka huu na hakuna dalili yeyote ya Serikali kutoa taarifa ya uchunguzi ndani ya bunge kama ilivyoagizwa na Bunge.

Ndugu Wanadar es salaam

Mara baada ya Azimio la Bunge kutolewa mwaka 2012 nilipata mialiko kutoka sehemu mbalimbali za dunia kwenda kushirikiana nao katika jambo hili. Jambo hili sio changamoto ya Tanzania peke yake. Nchi mbalimbali duniani kama Marekani, India, Nigeria, Ujerumani nk zinahangaika na jambo hili. Kila nchi ilichukua hatua inavyoona yenyewe inafaa ili kukabiliana na suala hili. Hatua ya Tanzania kufanya uchunguzi kufuatia agizo la Bunge ilikuwa ni ya kipekee na wachunguzi wengi wa kimataifa wakashawishika kuwa Tanzania itakuwa nchi ya mfano katika kupambana na tatizo la utoroshwaji wa fedha na ukwepaji wa kodi.

Katika safari hizo mbalimbali nilizofanya duniani nilipata taarifa ambazo niliziwasilisha Serikalini kwa ajili ya kusaidia uchunguzi wetu. Jaji mmoja wa Mahakama ya Ufaransa ambaye anafanya uchunguzi dhidi ya Benki ya HSBC alinipa ushirikiano wa kutosha na taarifa muhimu ambazo niliziwasilisha Serikalini ili waweze kuchukua hatua. Serikali haijafanya kitu. Miongoni mwa taarifa hizo ni orodha ya Watanzania 99 wenye akaunti 288 katika tawi moja la Benki ya HSBC nchini Switzerland. Orodha hiyo niliiwasilisha kwa Gavana wa Benki Kuu, Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania kwa ajili ya uchunguzi. Serikali mpaka sasa ninapozungumza nanyi haijatoa Taarifa licha ya kupewa kila aina ya ushirikiano.

Nimeamua leo kuiweka orodha hii wazi kama shinikizo kwa Serikali kutoa taarifa ya uchunguzi kabla ya Bunge kuvunjwa wiki ijayo. Kila mwandishi wa habari aliyepo kwenye mkutano huu nimempatia bahasha yenye majina 99 ya Watanzania au watu wenye mahusiano na Tanzania ambao wana akaunti HSBC ya Uswiss. Jumla ya akiba katika akaunti Benki hii pekee ni dola za kimarekani 114 milioni.

Narejea kusema kuwa sisi hatuna uhakika kama fedha hizi ni halali au haramu. Kuna ambazo zinahusiana na washirika 2 wa kashfa ya rada ambao ni Sailesh Vithlani aliyetuhumiwa kumhonga Andrew Chenge, Mbunge wa Bariadi na mmiliki wa kampuni ya Shivacom. Hizi zaweza kuhusishwa na ufisadi wa rada. Hata hivyo nyingine ni ngumu sana kusema zinatokana na nini kama vyombo vyetu vya uchunguzi vikiendelea kukalia kimya taarifa ya uchunguzi. Wito wangu ni kwa Serikali kuwasilisha taarifa ile Bungeni ili wenye fedha halali watofautishwe na wenye fedha haramu na wale wenye haramu wachukuliwe hatua kali za kisheria ikiwemo fedha hizo kurejeshwa nchini.

Ndugu Wanadar es salaam

Suala hili ni tone tu ya namna tatizo la kimaadili lilivyo kubwa nchini, na pia namna lilivyo na athari kisiasa na kiuchumi, ni suala ambalo kama Taifa tunapaswa kulitafutia dawa, Chama cha ACT Wazalendo tumewaletea dawa ya tatizo – Miiko ya Uongozi kama ilivyoainishwa katika katika Azimio la Tabora.

Ahsanteni sana.


Majina ya wenye mahela Uswisi.





SehemuHotuba hiyo
           

0 MAONI YAKO:

Post a Comment

Popular Posts

WADAU

BLOG ZINGINE