HATIMAYE bilionea Moise Katumbi Chapwe, Rais wa klabu ya TP Mazembe ya DRC amekubali mshambuliaji wa kimataifa wa Tanzania, Mbwana Ally Samatta ajiunge na KRC Genk ya Ligi Kuu ya Ubelgiji.
Na Samatta anatarajiwa kurejea Dar es Salaam kesho kwa ajili ya safari ya Ubelgiji kwenda kuanza maisha mapya katika soka ya Ulaya.
BIN ZUBEIRY SPORTS – ONLINE inafahamu Samatta tayari amekwishasaini Mkataba wa awali na Genk wa miaka minne na sasa anakwenda kukamilisha taratibu.
Samatta na Genk wanataka kukimbizana na muda ili kuwahi kabla ya dirisha dogo la usajili halijafungwa, angalau mapema Februari Mwanasoka huyo Bora Anayecheza Afrika aanze kucheza Ubelgiji.Samatta anatarajiwa kurejea kesho Dar es Salaam kwa safari ya Ubelgiji
Meneja wa Samatta, Jamal Kisongo ameiambia BIN ZUBEIRY SPORTS – ONLINE leo kwamba Katumbi ameridhia Samatta aende klabu anayopenda.
“Kama utakumbuka Samatta aliondoka hapa kwenda Lubumbashi kwa jambo moja kati ya mawili, kuruhusiwa kwenda Genk, au kubaki amalize Mkataba wake Mazembe ili aondoke kama mchezaji huru Aprili,”amesema Kisongo.
“Sasa imekuwa bahati nzuri, Katumbi ameelewa somo na kumkubalia kijana kwenda klabu anayopenda,”ameongeza.
Samatta aliondoka Dar es Salaam Januari 20, akiwa ameambatana na Ofisa mmoja wa Wizara ya Habari Utamaduni Sanaa na Michezo kwenda Lubumbashi, Jamhuri ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) kumshawishi Katumbi akubali ya Genk.
Katumbi alikuwa anataka Samatta aende Nantes ya Ufaransa, ambao walikuwa tayari kuilipa Mazembe Euro Milioni 1 na kuipa asilimia 25 ya mgawo iwapo watamuuza klabu nyingine mchezaji huyo.
BIN ZUBEIRY SPORTS – ONLINE inafahamu Genk wako tayari kutoa Euro 800,000 kumnunua Samatta kutoka Mazembe, ingawa Katumbi alikuwa anataka Euro Milioni 1.
Genk pia imekubali kuipa Mazembe asilimia 20 ya ngawo iwapo itamuuza Samatta klabu nyingine, wakati Katumbi anataka asilimia 25.
Ikumbukwe tayari Samatta amepatiwa viza na Ubalozi wa Ubelgiji kwenda kuanza maisha mapya KRC Genk.
Samatta aliyejiunga na TPM mwaka 2011 akitokea Simba SC aliyoichezea kwa nusu msimu, akitokea African Lyon, hadi sasa ameichezea klabu hiyo mechi 103 na kuifungia mabao 60.
Ndani ya mechi hizo, kijana huyo wa umri wa miaka 24, ameshinda taji la Ligi ya Mabingwa Afrika na Mazembe, huku naye akiibuka mfungaji bora wa michuano hiyo na kutwaa tuzo ya Mchezaji Bora Anayecheza Afrika.
Source: Binzubeiry
0 MAONI YAKO:
Post a Comment