January 23, 2016

KATIBU Mkuu wa Yanga SC, Dk. Jonas Tiboroha (pichani kushoto) amejiuzulu leo na tayari amewasilisha barua kwa Mwenyekiti, Yussuf Mehboob Manji.
Tiboroha ameiambia BIN ZUBEIRY SPORTS – ONLINE kwamba amechukua uamuzi huo ilia pate muda zaidi wa kufanya shughuli zake za Uhadhiri katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).
“Mimi ni Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kitivo cha Elimu ya Viungo (PE), na kwa kuondoka Yanga SC maana yake napata wasaa mzuri wa kumtumikia mwajiri wangu, UDSM,”amesema.
Pamoja na Tiboroha kutozama ndani sana juu ya kujiuzulu kwake, lakini inaelezwa alikuwa hana maelewano na Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano ya klabu, Isaac Chanji ambaye kwa sasa ndiye mtu anayesikilizwa na kuaminiwa zaidi na Manji.
Juhudi za kumpata Chanji kuzungumzia kujiuzulu kwa Tiboroha hazikufanikiwa hadi tunapandisha habari hii, ingawa zinaendelea ili kupata maoni yake.Isaac Chanji (kushoto) akiwa na Mwenyekiti Yussuf Manji (kulia) na Makamu Mwenyekiti, Clement Sanga (katikati)
Kwa upande wake, Tiboroha alipoulizwa kuhusu mahusiano yake na Chanji alisema; “Nilichoandika katika barua yangu ya kujiuzulu ndiyo sababu za msingi, kikubwa ninawapisha watu ambao wanaweza kuiongoza vizuri Yanga SC kuliko mimi,”amesema.
Tiboroha aliingia Yanga SC Desemba mwaka 2014 akichukua nafasi ya Benno Njovu aliyeondolewa kwa tuhuma mbalimbali. Aliingia Yanga SC akitokea Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kama Ofisa Maendelezo ya Ufundi.


Source:Binzubeiry

0 MAONI YAKO:

Post a Comment

Popular Posts

WADAU

BLOG ZINGINE