Luiza alizaliwa jimbo la Pernambuco, kaskazini mwa Brazil mwezi Oktoba. Ukubwa mzingo wa kichwa chake ulikuwa sentimeta 29 pekee
Mlipuko wa virusi vinavyoaminika kusababisha watoto kuzaliwa wakiwa na vichwa vidogo kuliko kawaida vimezifanya serikali Amerika Kusini kuwashauri watu kupanga uzazi.
"Tungependa kuwashauri wanawake wote wenye uwezo wa kuzaa wachukue hatua kupanga uzazi, na wazuie kushika mimba kati ya mwaka huu na mwaka ujao.”
Ushauri huu, kutoka kwa naibu waziri wa afya wa El Salvador Eduardo Espinoza, huenda ikawa hatua kali zaidi iliyochukuliwa na nchi za kanda hiyo kukabiliana na mlipuko wa ugonjwa huo ambao unaaminika kusababisha watoto kuzaliwa wakiwa na vichwa vidogo kuliko kawaida.
Virusi vya Zika, vinavyobebwa na mbu, vinadaiwa kuathiri vijusi vikiwa tumboni mwa kina mama walioambukizwa.
Virusi hivyo kwa sasa vimeathiri nchi nyingi Amerika. Umeelezwa kuwa mlipuko unaoendelea.
Kwa hivyo, kuwashauri wanawake kutoshika mimba ni jambo ambalo limeanza kuwa kawaida katika bara hilo.
Nchini Jamaica kwa mfano, wanawake wameshauriwa kuahirisha kushika mimba kwa angalau miezi sita.
Waziri wa afya Horace Dalley anasema ni muda tu kabla ya virusi hivyo kufika visiwani humo, kwa kuwa tayari kuna kisa cha maambukizi kimethibitishwa taifa jirani la Haiti.
Zika nchini Brazil
4,000
visa vya microcephaly tangu Oktoba
150 Watoto waliozaliwa na mwaka 2014
90% ya visa vimo kaskazini mashariki, maeneo maskini zaidi Brazil
1% ya watoto wote katika maeneo yaliyoathirika zaidi walizaliwa na microcephaly
Wizara ya Afya Brazil
AP
UBONGO KUDUMAA
"Ndoto yangu ni kwamba mwanangu atasoma hadi chuo kikuu. Daktari alisema hataweza, lakini ninamwamini Mungu,” anasema Erika Roque, mwenye umri wa miaka 20 nchini Brazil.
Mwanawe wa kiume wa umri wa miezi mitano alizaliwa akiwa anaugua microcephaly – ulemavu nadra sana wa kuzaliwa nao ambapo mtoto huzaliwa akiwa na kichwa kidogo. Katika visa vingi, hili huzuia ubongo kukomaa kabisa.
Mwanawe Erika ni mmoja tu kati ya watoto 4,000 waliozaliwa na microcephaly nchini Brazil, taifa lililoathirika zaidi na ugonjwa huo kanda hiyo.
Nchini humo, visa vimeongezeka mara 20 tangu Oktoba.
Wataalamu wa kimatibabu wanaamini mkurupuko wa sasa umesababishwa na virusi vya Zika.
Ingawa uhusiano wa moja kwa moja kati ya microcephaly na Zika haujathibitishwa, idadi ndogo ya watoto waliofariki walikuwa na virusi hivyo kwenye ubongo wao.
Hakuna ufafanuzi mwingine uliotolewa na wataalamu wa afya Brazil.
"Baada yake kuzaliwa, waliniambia … hakuna uchunguzi hata mmoja ulionyesha kulikuwa na kitu kilichoenda kombo akiwa tumboni,” Roque aliambia mwandishi wa BBC Brasil Camilla Costa mjini Recife, mji mkuu wa jimbo la kaskazini la Pernambuco, ambalo lina visa vingi zaidi nchini humo.
KUGUNDULIWA BAADA YA KUZALIWA
Sawa na yeye, wanawake wengi waja wazito huenda wasifahamu kwamba wameambukizwa na virusi vya Zika, kwani dalili huonekana katika asilimia 20 pekee ya visa vya maambukizi.
Ni vigumu kugundua pia ulemavu kwenye watoto, madaktari wanasema, na wengi wa kina mama wanasema waligundua ulemavu wa watoto wao baada ya kujifungua, walipogundua vichwa vya watoto wao vilikuwa vidogo sana, mzingo wa chini ya sentimeta 33.
“Ingelikuwa leo, nafikiri ningeahirisha mipango yangu ya kupata mtoto,” Mariana Botelho, mwenye umri wa miaka 33, na anayetarajia kujifungua, ameambia BBC Brasil.
Hilo ndilo baadhi ya maafisa wa afya Brazil wanawashauri wanawake kufanya.
Ingawa si sera rasmi, mkurugenzi wa idara ya kufuatilia magonjwa katika Wizara ya Afya, Claudio Maierovitch, amependekezea wanawe katika maeneo yaliyoathirika zaidi kutojaribu kushika mimba.
Maierovitch baadaye aliondoa ushauri huo, na taarifa rasmi iliyotolewa na wizara badala yake iliwashauri wanawake kushauriana na madaktari wao kuhusu hatari zilizoko.
Erika Roque na mwanawe Erick
“MSISHIKE MIMBA”
Ushauri sawa na wa afisa huyo wa Brazil umetolewa taifa jirani la Colombia, ambako Waziri wa Afya anaamini kupunguza idadi ya wanawake wenye mimba kipindi hiki cha mlipuko ndiyo njia bora zaidi.
“Ukizingatia kiwango cha sasa cha mkurupuko wa virusi vya Zika na hatari iliyopo, unapendekeza wana ndoa waahirishe kutunga mimba kipindi hiki, ambacho kinaweza kudumu hadi Julai 2016”, alisema Waziri wa Afya Alejandro Gaviria kupitia taarifa.
Tangazo hilo tata limetolewa baada ya Taasisi ya Kitaifa ya Afya kupokea habari za visa zaidi ya 11,000 za virusi vya Zika, miongoni mwa hizo, visa 500 vya wanawake waja wazito, ingawa hakuna kisa hata kimoja cha microcephaly kimethibitishwa kufikia sasa.
KUPANGA UZAZI
Jaribio la kudhibiti idadi ya mimba katika ngazi ya kitaifa imezua utata Amerika Kusini.
Baadhi ya wataalamu wanaamini sera za kudhibiti uzazi zitasaidia kudhibiti mlipuko wa virusi vya Zika.
“Ni uamuzi mgumu sana kufanya. Sitaki kuwaambia wanawake [kwamba hawawezi kushika mimba]”, anasema Jonas Schmidt-Chanasit, kutoka kwa taasisi ya matibabu ya Bernhard-Nocht na ambaye anafanya kazi na kundi la watafiti la WHO.
“Ninaweza kutahadhari sana, lakini iwapo lazima tufanye uamuzi kwa sasa basi ndio, ninaweza kupendekezea wanawake wajizuie kushika mimba ili kupunguza hatari ya kutokea kwa ugonjwa huo. Ni njia moja ya kudhibiti ugonjwa huu,” amoengeza.
Hata hivyo, ushauri huenda usitoshe, kwani wengi hawajazoea kuzaa kwa mpango.
Katika nchi zilizostawi, njia za kupanga uzazi hupatikana kwa urahisi, na karibu nusu ya mimba yote hupangiwa, takwimu zinaonyesha.
Idadi hii inashuka sana maeneo mengine ya dunia, ambapo huduma za kupanga uzazi hazipatikani na hazitumiwi sana.
“Kupendekeza watu waahirishe kushika mimba katika taifa [kama vile Colombia] ambako zaidi ya asilimia 50 ya mimba hutolewa kiholela ni kutofikiria”, amesema mwanaharakati Monica Roa, mwanachama wa shirika la Women's Link Worldwide, kama alivyonukuliwa na gazeti la Colombia la El Espectador.
copyrightAFP
MJADALA WA UTOAJI MIMBA
Huku ufahamu kuhusu ugonjwa huo ukiongezeka, wataalamu wa afya wanasema visa vya utoaji mimba nchi zilizoathirika huenda vikaongezeka.
Nchini Brazil, sheria huruhusu wanawake kutoa mimba iwapo tu imetokana na ubakaji au maisha ya mama yamo hatarini.
GETTY
0 MAONI YAKO:
Post a Comment