January 20, 2016


UTANGULIZI

Katika semina mbili tofauti za wasanii mbalimbali kutoka wilaya ya Ilala na Temeke ambapo ulikuweko mkusanyiko wa wasanii wa kike na wakiume, wakiwemo wasanii wa filamu, ngoma, muziki wa dansi, wachoraji wachongaji na kadhalika mambo mengi kuhusu hali halisi ya rushwa katika tasnia hii yalijadiliwa na hatimae kuwekwa maazimio. Hii ni moja ya semina nyingi ambazo zimetayarishwa na Chama cha Sanaa za Maonesho Tanzania(CHASAMATA). Katika semina hii mada ilikuwa Athari za rushwa katika tasnia ya Sanaa.

 

SEMINA

SEMINA ilianza kwa mtoa mada ambaye pamoja na mengine ni msanii ambae yumo katika shughuli za sanaa tangu mwaka 1975, alianza kwa kuelezea historia ya rushwa katika sanaa kwa kadri ya uelewa wake. Ni wazi kuwa rushwa katika eneo hili si ngeni hata kidogo. Baadhi ya mambo yaliyoleta rushwa katika historia ya sanaa, ni mlolongo wa vibali vilivyokuwa vikitakiwa kabla ya kila kabla ya kila onyesho. Mtindo wa vibali kwa kazi za sanaa uliingizwa nchini kutokea enzi za ukoloni katika kudhibiti kile ambacho wasanii wanakifanya. Wakati nchi ilikuwa katika enzi ya chama kimoja vibali viliendelea vikiwa na sababu ambazo hazitofautiani sana na zile za wakati wa ukoloni, hivyo ilikuwa ni makosa kufanya onyesho bila kibali kutoka kwa afisa utamaduni, kikundi kililazimika kuwa na kibali hata cha kutoka nje ya mkoa ambako kimesajiliwa. Na pia kilihitajika kibali kungia katika mkoa mwingine. Maafisa utamaduni wa mkoa na wilaya ndio waliokuwa na mamlaka ya kutoa vibali hivi, huu ulikuwa uwanja mzuri kwa kuombwa rushwa ili uweze kufanya kazi zako.

Sehemu nyingine iliyokuwa na rushwa ni redio, ambayo hapo awali ilikuwa kituo cha redio kilikuwa kimoja tu RTD, na hapo pia ndio kwa muda mrefu palikuwa sehemu peke yake ambapo wanamuziki waliweza kurekodi kazi zao. Rushwa ilianza pale ambapo ililazimi kupeleka mashahiri ya tungo za muziki kabla haujarekodiwa, kamati iliyokuwepo wakati huo, iliweza kukataa au kukubali wimbo urekodiwe kwenye studio zake bila kutoa maelezo, hivyo bendi nyingi zilidaiwa kitu kidogo ili kuhakikisha nyimbo ambazo zimefika kwenye kamati hiyo zote zinapita zilivyo, ngazi nyingine ya rushwa ilikuwa inakuja katika kuwapa motisha watangazaji husika kupiga nyimbo katika vipindi vyao, aina ya rushwa ambayo iko mpaka leo.

Rushwa nyingine ilikuwa inatolewa kwa viongozi wa serikali katika kupata kibali cha vikundi kutoka nje ya nchi, kwani taratibu zilikuwa wazi kuwa kikundi hakiwezi kutoka nje ya nchi mpaka Mkurugenzi wa Utamaduni atakapopitisha kibali hicho, Mkurugenzi mmoja ametajwa kuwa alikuwa maarufu kwa kulazimisha kipengele cha kuambatana na kikundi kwenye safari za nje, na kama hakukuwa na uwezekano huo pesa ilikuwa lazima itolewe au la hakuna kibali, wasanii wengi walikosa kwenda nje au wengine waliamua kuchukua sheria mkononi na kusafiri kwa njia za panya. Tatizo hili limedhihirika kuwa bado liko baada msani mmoja kutoa mfano wa Afisa wa Wizara ya Utamaduni kugoma kusoma na kupitisha ripoti moja ambayo ingefungua mlango wa vikundi hata 40 vya ngoma za kiasili kupata nafasi kuzuru Uchina, na kudai msanii atafute shilingi milioni moja kwa ajili ya kikao cha kuchambua ripoti hiyo, ambayo kwa sasa imerudi kwenye makabati.

Pia imedhihirika kuwa bado kuna Maafisa Utamaduni wanapenda rushwa kiasi cha kuwezesha vikundi kushinda katika mashindani mbalimbali kwa makubaliano ya kugawana zawadi. Ilitolewa mifano ambapo Afisa mmoja alidai khanga 5 kati ya 20 zilizotolewa kama zawadi kwa kikundi alichokisaidia kushinda na pia alidai kupewa wheelbarrow ambayo kikundi kilishinda katika mashindano mengine.

Katika kuchangia mada, jambo ambalo lilkuwa wazi ni kuwa rushwa ya ngono kwa wasanii wa kike ni adha wanayoipata kila mara. Katika tasnia ya filamu na michezo ya jukwaani, viongozi wa vikundi, waongozaji wa filamu, producers ndio waliotajwa kuongoza katika kuomba rushwa hiyo, na wanawake wote huombwa rushwa hiyo bila kujali umri, jambo ambalo lilimfanya mama moja mtu mzima atokwe na machozi pale alipoombwa rushwa hiyo na mvulana ambae alimuona kama mwanawe. Vikundi vidogovidogo vya mtaani vimekithiri kwa aina hii ya rushwa na hasa katika maeneo yanajulikana kama kambi au location za filamu. Kwa upande wa wanamuziki wa kike adha yao huanzia na producers, kasha watangazaji, na hata wafadhili wa kazi zao kiasi cha mtangazaji maarufu kudai aliamua kuachana na fani ya muziki kwa ajili ya adha hiyo.

Kwa ujumla makundi yote yaliyoshiriki katika semina hii yalikubaliana kuwa kuna rushwa ziko za aina mbali mbali, kuna rushwa ya fedha taslimu au vitu, rushwa ya ngono.

Rushwa ilionekana hudaiwa katika ngazi mbali mbali, watu binafsi, au vikundi.

Kati ya maeneo ambayo yalitajwa kuhusika na rushwa na katika vikundi, ambapo viongozi wa vikundi huwadaia wasanii rushwa ili waweze kupata nafasi ya kuendelea katika vikundi. Wasanii hutoa rushwa ili wawemo katika michezo mbalimbali, au katika filamu, na kama ilivyo tabia ya rushwa , ufanisi wa msanii si muhimu katika kupata nafasi husika. Katika kundi la sanaa za maigizo na filamu, rushwa ya ngono iliwakumba sana wasanii wa kike. Ambapo palikuweko na ushuhuda wa washiriki walioombwa rushwa ya ngono na waongozaji wa filamu, watayarishaji wa filamu na kadhalika. Kumekuweko na kundi jipya la waombaji wa rushwa hii ambapo wanawake huwaomba rushwa ya ngono wanawake wenzao!, hili si geni kwa upande wa wanaume, ambapo taarifa ya aina hii ya rushwa ya ngono kwa jinsia moja ni ya muda mrefu sana.

0 MAONI YAKO:

Post a Comment

Popular Posts

WADAU

BLOG ZINGINE