Wafanyakazi watatu wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) mkoani Morogoro,
wanashikiliwa na Polisi wakihojiwa kutokana na kifo cha mfanyakazi
mwenzao, Deo Elias (30), mkazi wa Mazimbu, Manispaa ya Morogoro kwa
kunaswa na umeme juu ya nguzo.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa
Morogoro, Ulrich Matei akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake
jana, alisema tukio hilo lilitokea juzi saa 5.30 asubuhi maeneo ya
Mafiga, wakati Elias akiwa na wafanyakazi wenzake katika eneo la kazi.
Kamanda Matei alisema Elias alipokuwa na wenzake katika eneo hilo wakirekebisha umeme, alinaswa na kufa papo hapo.
Meneja
wa Tanesco Mkoa wa Morogoro, Mhandisi John Bandiye akizungumzia tukio
hilo ofisini kwake jana, alisema Elias alikuwa katika kazi za kawaida kama
fundi na tukio hilo limetokea kwa bahati mbaya.
Mhandisi
Bandiye alisema mfanyakazi huyo alikuwa akirekebisha njia ya umeme ya
Ngazengwa iliyopo eneo la Mafiga na ilikuwa imezimwa, lakini cha
kushangazwa ilikuwa na umeme uliosababisha kifo chake.
“Kwa sasa
shirika lina wafanyakzi wa muda wanaosaidiana na mafundi wakuu na
hupatiwa mafunzo na wanatambulika, tofauti na maneno yaliyozagaa mitaani
kuwa marehemu hakuwa mfanyakazi,” alisema.
Alisema mwili wake umesafirishwa kwenda kwao mkoani Mbeya kwa ajili ya maziko.
0 MAONI YAKO:
Post a Comment