
KATI
ya wanawake wa Kitanzania waliopeperusha bendera yetu vizuri nje ya
nchi kielimu ni Kapteni Hilda Wendy Ringo ambaye sasa ni rubani.
Elimu
yake ya sekondari aliipata katika Shule ya Tambaza jijini Dar es Salaam
na baadaye Chuo Cha Urubani cha Progress Flight Academy cha jijini
Pretoria, Afrika Kusini.
Ni
mwanamke wa kujivunia katika nchi yetu kwa sababu amekuwa akirusha
ndege yaani rubani. Amewahi kuhojiwa na vyombo mbalimbali vya habari
nchini na kuhusu kazi yake hiyo anasema:
“Kurusha ndege ni jambo zuri linalofurahisha.”
Rubani
Hilda ni mama mwenye umri wa miaka 33, anasema alianza kurusha ndege
akiwa na umri wa miaka 22 lakini sasa anarusha ndege hapahapa nchini
katika Kampuni ya Precision Air.
Ana uzoefu mkubwa na kazi hiyo ya
urubani kwa sababu ameifanya kwa zaidi ya miaka 10 sasa na ni mwanamke
wa kwanza Mtanzania kurusha ndege aina ya Boeing Airbus.
Anasema
wazo la kuwa rubani lilimuingia katika akili yake akiwa bado mdogo
baada ya kujiuliza maswali mengi kama vile ndege ambayo ni chuma na
mabati inawezaje kupaa angani?
Anasema swali hilo lilimjia wakati
anasafiri mara kwa mara na wazazi wake akitokea Kilimanjaro kuja Dar es
Salaam akitumia Shirika la Ndege la Tanzania (Air Tanzania) lilipokuwa
linatamba katika anga ya Tanzania enzi hizo.
Kapteni Hilda akizungumzia wanawake wenzake anasema: “Tanzania ina
hazina kubwa ya wanawake si tu kupitia kwenye elimu nzuri, mtu anayoweza
kuitumia kuwa ana kipaji kama yeye na kwenda sehemu mbalimbali yeye
binafsi au kwa kupitia taalum yake.”
Ushauri wake kwa watu wote hasa wasichana anasema: “Fanya kazi yako sawasawa na taaluma yako itakulipa vyema.”
Anawataka wanawake kuacha tabia ya kukaa bila kufanya kazi, badala yake anasema wanatakiwa kufanya kazi kwa bidii.
Anaizungumziaje serikali ya awamu ya tano ya Rais Dk. John Pombe
Magufuli hasa kuhusu Shirika la Ndege la Tanzania lililokufa kifo cha
mende?
“Ushauri wangu kwa serikali ni kwamba iwaruhusu wataalam wa sekta ya
anga kutoka sehemu mbalimbali duniani kuja nchini na kufanya utafiti wa
awali utakaojikita kwenye kulifufua upya shirika letu la ndege la
taifa.”
Anafadhaika akitulinganisha na nchi ya Rwanda ambayo imekuwa katika
vita vya wenyewe kwa wenyewe kwa miaka mingi lakini sasa wametuzidi
katika kuendesha shirika la ndege na sasa wanalo lao, Air Rwanda ambalo
ndege zake husafiri hadi Dubai na kuunganisha hadi London Uingereza.
“Tanzania
katika kipindi chote tangu tupate uhuru tumekuwa na amani lakini
haiwezi kujivunia shirika lake la ndege kwa kutamba kuwa limekua,”
anasema huku akiamini kuwa kuna watu waliliua shirika letu la ndege kwa
manufaa yao binafsi.
Hata
hivyo, hivi karibuni, Rais Dk. John Magufuli alionesha tumaini la
kufufua shirika letu la ndege aliposema kwamba kutokana na ukusanyaji
mzuri wa kodi za serikali, kuna uwezekano wa kununua ndege zetu hata
kama itakuwa kwa awamu.
0 MAONI YAKO:
Post a Comment