Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran imelaani
mashambulizi ya kigaidi yaliyofanyika juzi jioni katika maeneo
mbalimbali ya Saudi Arabia likiwemo lile lililotokea karibu na Msikiti
wa Mtume (saw) katika mji mtakatifu wa Madina.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran Bahram Qasemi ametuma
salamu za rambirambi na mkono wa pole kwa familia za wahanga wa
mashambulizi hayo na kusema: Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inalaani ugaidi
wa aina zote na popote pale unapotokea duniani na unazitaka nchi zote
kupambana kwa nguvu zote na vyanzo, sababu na wanaofanya mashambulizi ya
kigaidi.
Qasemi amesema kuwa ugaidi hususan katika Mashariki ya Kati umeonesha kuwa, ovu hilo halitambui mipaka wala utaifa na hakuna njia nyingine ya kukabiliana nalo isipokuwa mshikamano na umoja wa kimataifa.
Magaidi wawili waliokuwa na mabomu jana jioni walijilipua karibu na Masjidu Nabawi mjini Madina na katika msikiti mwingine wa Waislamu wa madhehebu ya Shia katika mji wa Qarif huko mashariki mwa Saudia. Mashambulizi hayo yamesababisha vifo vya watu wasiopungua sita na kujeruhi wengine kadhaa.
0 MAONI YAKO:
Post a Comment