August 26, 2016

Tokeo la picha la CUF

THE CIVIC UNITED FRONT
CUF-Chama Cha Wananchi

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
WABUNGE WA CUF WAKANUSHA KUPINGA UKUTA;
Imetolewa leo tarehe 27/8/2016
Wabunge wa THE CIVIC UNITED FRONT (CUF-Chama Cha Wananchi) wanapenda kukanusha taarifa iliyoripotiwa na chombo kimoja cha habari juu ya eti wabunge wa CUF kugomea UKUTA. Operesheni UKUTA ni mpango wa shughuli za kisiasa ulioandaliwa na chama rafiki, wenzetu katika UKAWA chama cha demokrasia na maendeleo-CHADEMA. Ni Operesheni yenye madhumuni ya kupinga mfumo wa uongozi wa serikali ya awamu ya tano wenye muelekeo na taswira ya uongozi wa kiimla (udikteta). Watanzania wote wenye mapenzi na uzalendo kwa nchi yao, na wenye maono ya kutaka mabadiliko na maendeleo ya kiuchumi na kisiasa nchini kamwe hawawezi kupinga, kudharau na au kugomea juhudi hizi.
Sisi wabunge tunaotokana na chama cha CUF tunapenda kutoa taarifa rasmi za kukanusha upotoshaji huo uliotolewa na chombo hicho cha habari cha CCM, na tunawataka watanzania wote mahala popote walipo kupuuza taarifa hizo. Hakuna mbunge yeyote wa chama chetu aliyefanya mazungumzo na gazeti hilo na hakuna ukweli wowote katika kile kilichoandikwa. Aidha tunawahimiza wananchi wote kushirikiana na kuungana kwa pamoja kupinga utawala wa kiimla usiozingatia katiba na sheria za nchi yetu kwa namna na njia tofauti kadri watakavyoona inafaa kulingana na mahala na mazingira waliopo.
Kila chama kina utaratibu wake wa kuandaa ajenda, masuala na kufanya shughuli (harakati) za kisiasa kwa namna inayoridhiwa na vikao vya maamuzi vya ngazi husika. Sisi wabunge wa CUF tunatambua kuwa chama chetu cha CUF kina vipaumbele viwili kwa wakati huu. Kwanza ni kuhakikisha kuwa juhudi zinazoendelea sasa za kupigania maamuzi halali ya kidemokrasia waliyoyafanya Wazanzibar tarehe 25/10/2015 kwa kumchagua Maalim Seif Sharif Hamad kuwa Rais zinafanikiwa. Maamuzi ya kutoshiriki katika kilichoitwa uchaguzi wa marudio wa tarehe 20/3/2016 ulitokana na uwamuzi halali wa pamoja uliofikiwa na wajumbe wa Baraza Kuu la Uongozi la CUF Taifa. Sisi wabunge tunaamini kuwa uamuzi huu ni sahihi ili kulinda misingi ya haki na demokrasia nchini. Pili ni kukamilisha utaratibu wa kujaza nafasi zilizo wazi za Mwenyekiti wa Chama Taifa na Makamu wake, baada ya wajumbe wengi wa Mkutano Mkuu Maalum wa CUF uliofanyika katika ukumbi wa Blue Pearl Hotel, Dar es Salaam tarehe 21/8/2016 kukubali kujiuzuru kwa Mheshimiwa Prof Ibrahim H. Lipumba. Tunatambua kuwa kujiuzuru kwake kunatokana na haki yake ya kikatiba na kamwe mvutano uliojitokeza hautokani na sababu zozote za maana ndani au nje ya chama chetu. Hivyo si sahihi kuyahusisha na UKAWA, CHADEMA au kinachoitwa mpasuko.
Sisi wabunge wa CUF kutokana na ushiriki wetu katika chaguzi mbalimbali nchini tunaamini kuwa taasisi zilizopewa dhamana ya kusimamia uchaguzi nchini ZEC na NEC bado zina matatizo na mapungufu makubwa ya kiutendaji na kuisimamizi. Tume zetu haziko huru na hazitendi haki. Tunasimama imara kuhakikisha kuwa tunajenga mifumo ya uongozi madhubuti na taasisi imara za kidemokrasia nchini kwa kuzingatia misingi ya katiba, sheria, kanuni na taratibu tulizojiwekea katika uendeshaji wa nchi yetu. Serikali ya awamu ya tano lazima iheshimu matakwa ya kikatiba na ikubali kukosolewa na kusikiliza hoja mbadala.
Tunapenda kuwahakikishia wanachama na wapenzi wetu wote kuwa chama chetu cha CUF kipo imara na kwamba Wabunge wote wa upinzani bungeni tutaendelea kuimarisha umoja na mashirikiano baina yetu ya KUDAI HAKI SAWA KWA WOTE, DEMOKRASIA NA MABADILIKO YA KWELI kwa maslahi mapana ya Taifa letu.

IMETOLEWA NA
RIZIKI SHAHARI MNGWALI (MB)
MWENYEKITI WA WABUNGE WA CUF
Mawasiliano: 0783 054 600/0712 313159

0 MAONI YAKO:

Post a Comment

Popular Posts

WADAU

BLOG ZINGINE