August 24, 2016



MKE wa bilionea Erasto Msuya, Miriam Elisaria Msuya (41) amefikishwa mahakamani kwa tuhuma za mauaji ya dada wa wa bilionea huyo, Aneth Msuya.

Mshtakiwa huyo alifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jana jijini Dar es Salaam na kusomewa mashtaka na Wakili wa Serikali, Diana Lukondo mbele ya Hakimu Mkazi, Margareth Bankika.

Akisoma mashtaka hayo, Lukondo alidai mshtakiwa huyo ambaye ni mkazi wa maeneo ya Sakina kwa Iddi, jijini Arusha anadaiwa Mei 25, mwaka huu katika maeneo ya Kibada Kigamboni jijini Dar es Salaam alimuua Aneth Elisaria Msuya.

Mshtakiwa hakutakiwa kujibu lolote kwa sababu mahakama hiyo haina uwezo wa kusikiliza kesi za mauaji, mbapo Jamhuri ilidai upelelezi haujakamilika na kuomba kesi hiyo ipangwe tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa.

Hakimu Bankika, alikubali kuahirisha kesi hiyo hadi Septemba 9, mwaka huu kwa ajili ya kutajwa na mshtakiwa alirudishwa rumande.

Habari zilizopatikana baada ya tukio hilo zilidai kwamba, marehemu Aneth aliuawa kwa kuchinjwa na watu wasiojulikana usiku wa kuamkia Mei 25, mwaka huu Dar es Salaam.

Mauaji hayo yalitokea nyumbani kwake eneo la Kibada block 16, Kigamboni ambako inaelezwa wauaji hao hawakuchukua kitu chochote ndani ya nyumba yake.

Marehemu Erasto Msuya, aliyekuwa mfanyabiashara wa madini ya Tanzanite aliuawa kwa kufyatuliwa risasi Julai 7, mwaka 2013 katika eneo la Mijohoroni,  kando ya barabara ya Arusha – Moshi wilayani Hai mkoani Kilimanjaro, akiwa ameitika wito wa kwenda kununua madini ya Tanzanite baada ya kupigiwa simu na vijana wawili  waliomtaka wakutane maeneo hayo.

Inaelezwa kuwa alifika katika eneo hilo akiwa na gari lake aina ya Range Rover T 800 CKF na kuwakuta vijana hao wakimsubiri, baada ya kuteremka Msuya alielekea kumsalimia mmoja wa vijana hao.

Hata hivyo kabla hajamfikia kijana huyo aliitoa bunduki ya SMG namba KJ 10520 aliyokuwa ameificha kwenye koti na kumfyatulia risasi takribani 22 mwilini.

0 MAONI YAKO:

Post a Comment

Popular Posts

WADAU

BLOG ZINGINE