SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) imewasilisha marekebisho ya
Katiba ya Zanzibar ya 11 ya mwaka 1984, ambayo yatatoa nafasi na kumpa
uwezo Rais wa Zanzibar, kuchagua wajumbe wa Baraza la Wawakilishi bila
ya kushauriana na Kiongozi wa Upinzani ambaye kwa sasa hayupo katika
baraza hilo.
Kwa mujibu wa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Katiba, Sheria, Utumishi wa
Umma na Utawala Bora, Haroun Ali Suleiman, katika marekebisho hayo
vifungu viwili vinahitaji kufanyiwa marekebisho kikiwemo cha 66 kwa
kufanya marekebisho na kufuta maneno ya vyama na kiongozi wa upinzani.
Akifafanua katika kifungu hicho, alisema lengo lake ni kutoa nafasi kwa
Rais wa Zanzibar kuchagua nafasi mbili za wajumbe wa Baraza la
Wawakilishi bila ya kushauriana na Kiongozi wa Upinzani katika Baraza
ambaye kwa sasa hayupo, baada ya Chama cha Wananchi (CUF) kususia
Uchaguzi Mkuu wa marudio mwaka huu, na hivyo kutopata mwakilishi yeyote
na hivyo kufutika kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa ambayo Katibu Mkuu wa
CUF, Maalim Seif Shariff Hamad alikuwa Makamu wa Kwanza wa Rais.
Haroun alisema katika mazingira ya sasa katika Baraza la Wawakilishi,
hakuna kiongozi katika Baraza hilo pamoja na vyama vilivyopata wingi wa
kura, hatua ambayo imemfanya Rais kushindwa kuteua wajumbe wawili katika
Baraza la Wawakilishi.
‘Katika Baraza la Wawakilishi la sasa Rais ameshindwa kuteua wajumbe
wawili katika nafasi kumi ambapo anatakiwa ashauriane na kiongozi wa
upinzani ambaye hayupo kwa sasa,” alifafanua na kuongeza kuwa Kifungu
cha 77(2) kinafuta neno la upinzani lenye uwakilishi ndani ya Baraza la
Wawakilishi.
Akifafanua, alisema marekebisho ya Katiba yanayopendekezwa mbele ya
Baraza la Wawakilishi, lengo lake kubwa kuimarisha demokrasia na kumpa
nafasi Rais kuchagua wajumbe wa Baraza watakaofanya kazi kwa maslahi ya
taifa. Katiba ya Zanzibar imempa mamlaka Rais wa Zanzibar kuchagua
wajumbe 10 katika Baraza la Wawakilishi, ambapo nafasi mbili kwa
kushauriana na kiongozi wa upinzani ambaye hayupo kwa sasa.
Wajumbe watatu wa Baraza la Wawakilishi walioteuliwa kutoka katika vyama
vya upinzani, wanatokana na nafasi 10 kwa mujibu wa uwezo aliopewa Rais
na Katiba. Wajumbe hao watatu kutoka vyama vya upinzani ni Hamad Rashid
Mohamed, Juma Ally Khatib na Said Soud Said.
0 MAONI YAKO:
Post a Comment