Jumuiya
ya Madhehebu ya Dawoodi Bohra imetoa mchango wa Dola za Marekani laki
mbili na nusu (Usd. 250,000) sawa na Shilingi Milioni Mia Tano Arobaini
na Tano za Kitanzania (Ths. 545,000,000) kwa ajili ya kuwasaidia
waathirika wa tetemeko la ardhi lilitokea katika Mkoa wa Kagera tarehe
10 Septemba, 2016.
Kiongozi
Mkuu wa Madhehebu ya Bohra Duniani Dkt. Syedna Mufaddal Saifuddin
amekabidhi mchango huo kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.
John Pombe Magufuli, jana walipokutana na kufanya Mazungumzo leo tarehe
13 Oktoba, 2016 Ikulu Jijini Dar es Salaam.
Kati
ya fedha hizo Dola za Marekani laki moja (Usd. 100,000) zimetolewa na
Dkt. Syedna Mufaddal Saifuddin mwenyewe, Dola za Marekani laki moja
(Usd. 100,000) zimetolewa na Viongozi wengine wa Madhehebu ya Bohra na
Dola za Marekani Elfu Hamsini (Usd. 50,000) zimetolewa na wana Jumuiya
ya Bohra wa Tanzania.
Pamoja
na kutoa mchango huo, Dkt. Syedna Mufaddal Saifuddin ameahidi kuwa
Jumuiya hiyo ambayo inamiliki hospitali kubwa zilizopo maeneo mbalimbali
duniani ikiwemo India, itajenga hospitali hapa nchini kwa ajili ya
kutoa huduma za matibabu.
Pia
Dkt. Syedna Mufaddal Saifuddin ameahidi kuwa Jumuiya ya Bohra itatoa
udhamini wa masomo ya udaktari kwa vijana wa Tanzania na pia itadhamini
matibabu kwa wagonjwa 20 watakaopelekwa nchini India kwa ajili ya
kupatiwa matibabu.
Kwa
Upande wake Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe
Magufuli, amemshukuru Dkt. Syedna Mufaddal Saifuddin na Jumuiya nzima ya
Dawoodi Bohra kwa mchango walioutoa kwa waathirika wa tetemeko la ardhi
Mkoani Kagera na pia kwa kufanyia mkutano wao wa mwaka hapa nchini
uliowaleta wageni takribani 31,000 kutoka mataifa mbalimbali duniani.
“Dkt.
Syedna Mufaddal Saifuddin nakushukuru sana kwa kuja hapa nchini kwetu
na kutuletea mkutano huu mkubwa, ujio wenu umeimarisha uhusiano kati ya
Bohra na Tanzania na pia umechangia uchumi wa nchi yetu.
“Nakushukuru
pia kwa nia yenu ya kujenga hospitali hapa nchini, kuwasomesha
madaktari na kudhamini matibabu ya wagonjwa huko India, naomba
nikuhakikishie kuwa mchango mlioutoa utatusaidia sana na pia mkijenga
hospitali na kufundisha madaktari mtakuwa mmesaidia kuokoa fedha nyingi
ambazo Serikali ingetumia” amesema Rais Magufuli.
Aidha,
Rais Magufuli amewaalika wanajumuiya ya Dawoodi Bohra kuja kuwekeza
hapa nchini katika sekta mbalimbali zikiwemo viwanda, kilimo,
usafirishaji, madini na uvuvi na amewahakikishia kuwa Serikali itawaunga
mkono wote watakaokuwa tayari kuja kuwekeza Tanzania.
Jumuiya
ya Madhehebu ya Dawoodi Bohra Duniani imeadhimisha mwaka mpya wa
Kiislam na kumbukumbu ya kifo cha Mjukuu wa Mtume Muhammad (S.A.W)
aitwaye Imamu Hussein ambapo maadhimisho yake ya kidunia yaliyoambatana
na tamasha la zaidi ya wiki mbili yamefanyika hapa nchini kuanzia tarehe
01 Oktoba, 2016 hadi tarehe 11 Oktoba, 2016.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
13 Oktoba, 2016
0 MAONI YAKO:
Post a Comment