Akizungumza katika Mkutano wa Kidemokrasia uliofanyika jijini Dar es Salaam leo, Zitto alisema kuchanganyikiwa huko kwa CCM ndiko kunakosababisha serikali ya Rais John Magufuli iseme mengine na katika utekelezaji wake yafanyike mambo mengine.
“Tunatambua kuwa serikali ya Rais Magufuli imeweka mkazo katika kujenga viwanda. Hili ni jambo jema kwa kuwa likitekelezwa vizuri litachochea ukuaji wa ajira kwa vijana nchini. Hata hivyo, pamoja na nia njema, haielekei kwamba serikali ya CCM inaelewa namna ya kutelekeleza lengo hili zuri.
“Kutokana na mkanganyiko wa kifalsafa, serikali haijui ni nani hasa anapaswa kujenga viwanda kati ya serikali yenyewe na sekta binafsi. Matokeo yake imekuwa ikivizia miradi ya sekta binafsi na kukimbilia kuizindua wakati huo huo serikali ikitoa kauli ambazo zinarudisha nyuma ari ya wafanyabiashara wazalendo kuwekeza katika viwanda,” alisema Zitto ambaye pia ni Mbunge wa Kigoma Mjini.
Mkutano wa kidemokrasia ni kikao pekee rasmi cha kikatiba katika chama cha ACT- Wazalendo ambapo viongozi na wanachama wanakutana ana kwa ana na kubadilisha mawazo kuhusu chama na maendeleo ya nchi kwa ujumla. Mkutano huo wa kwanza na wa aina yake hapa nchini umehudhuriwa na wageni mbalimbali kutoka nchi na vyama marafiki kwa ajili ya kubadilisha uzoefu katika nyanja mbalimbali.
Zitto ambaye amekuwa mbunge kwa zaidi ya miaka 15, alisema nchi sasa inahitaji mwelekeo, falsafa na namna mpya ya kutatua matatizo ya Tanzania; akisema CCM kwa sasa haina mwelekeo wowote – miaka takribani 25 baada ya kuachana na siasa ya Ujamaa na Kujitegemea.
Katika mkutano huo uliofanyika katika Ukumbi wa Makumbusho, Posta, jijini Dar es Salaam, Zitto alitoa mifano ya masuala mbalimbali yahusuyo uchumi, ajira, jinsia na elimu kupitia hotuba yake iliyokuwa na maneno takribani 5000.
Kuhusu vita dhidi ya rushwa inayoendeshwa na serikali ya Rais Magufuli, Zitto alisema ACT kinaunga mkono juhudi hizo ingawa hadi sasa wanaoshughulikiwa ni mawakala wa rushwa walioko serikalini na si wala rushwa wenyewe.
Mwanasiasa huyo pia aliponda mwenendo wa serikali wa kuzuia shughuli mbalimbali za kisiasa na kusema hakuna namna ambayo nchi inaweza kupambana na ufisadi pasipo kujali misingi mingine ya haki za watu.
“Mtu yeyote anayedai kwamba anaweza kupambana na ufisadi na kuleta maedeleo kwa kukanyanga demokrasia na utawala wa sheria ni mwongo na anastahili kukataliwa na kukemewa mapema kabla hajaota pembe.
“Tunasisitiza kuwa mtu yeyote wa kawaida au kiongozi anayesema kwamba anaweza akapambana na ufisadi kwa kukanyaga misingi ya demokrasia na utawala wa sheria mtu huyo ni fisadi na anataka kujenga himaya mpya ya ufisadi. Mtu huyo, pamoja na mambo yake yote, yafaa akataliwe na kudharauliwa haraka,” alisema.
Katika hatua nyingine, Zitto alisema kwamba juhudi za kuboresha elimu hapa nchini zitakuwa na maana tu endapo walimu ndiyo watakuwa kipaumbele na si madawati wala madarasa. Alisema upatikanaji wa madawati na maabara utakuwa na maana tu endapo walimu watakuwa na motisha ya kufanya kazi.
“Tafiti zinaonyesha kwamba ili kuboresha ubora wa elimu kitu kikubwa na cha msingi kabisa kuliko vyote ni kuwekeza kwa walimu na taaluma ya ualimu. Maeneo muhimu ni mafunzo ya walimu na kuhakikisha kwamba wanakuwa na motisha wa kutosha katika kufanya kazi zao. Bahati mbaya hapa Tanzania serikali na jamii kwa ujumla hatuthamini kazi ya ualimu.
“Taaluma ya ualimu imekuwa ni daraja la kujiokoa baada ya kukosa sehemu zingine. Walimu wetu wanaofundisha katika mazingira magumu sana hatuwathamini na wakati mwingine hata tunawabeza.
Pia alitoa wito kwa asasi za kijinsia kupigia kelele suala la ajira kwa wanawake kwa vile alisema hivi sasa wanaume wanapata ajira zaidi kuliko wanawake, jambo alilosema linapaswa kurekebishwa.
Mwenyekiti huyo wa zamani wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), alitumia fursa hiyo kueleza kuhusu changamoto za ajira kwa vijana hapa nchini; akisema zaidi ya theluthi mbili ya nguvukazi iiyopo nchini haijaajiriwa katika sekta rasmi.
Mbele ya waliohudhuria mkutano huo kutoka ndani na nje ya nchi, Zitto alieleza kusikitishwa kwake na mwenendo wa nchi za Kiafrika katika siku za karibuni, aliosema unafanana na hali ilivyokuwa kwenye miaka ya 1960.
“Tunashuhudia uvunjwaji mkubwa wa haki za binadamu katika mataifa ya Burundi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Sudani ya Kusini na Ethiopia. Machafuko yote haya yanasababishwa na kupuuzwa kwa haki za kiraia na kidemokrasia.
“Tunatoa wito maalumu kwa taasisi za kiraia, taasisi za dini na vyuo vikuu katika bara la Afrika kusimama imara katika kulinda utawala wa sheria na demokrasia ya vyama vingi. Tunazitaja taasisi hizi kwa sababu kazi zao na uwepo wao unategemea sana uwepo wa demokrasia katika nchi yoyote duniani. Demokrasia ya vingi ikichezewa na hatimaye kufififshwa taasisi za kiraia, taasisi za dini na vyuo vikuu haviwezi pia kuwa na uwezo wa kufanya kazi zao kwa uhuru.
“Chama chetu kinamtaka Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo Joseph Kabila aheshimu Katiba ya nchi hiyo na kuruhusu uchaguzi kufanyika kama ilivyopangwa ili kuwezesha mpito wa kidemokrasia kwa amani kabisa. Tanzania haiwezi kuendelea kupokea wakimbizi wa kongo kwa makosa ya wanasiasa wanaong’ang’ania madaraka kinyume na Katiba,” alisema Zitto.
Mwisho
Chanzo: Ukurasa wa FB wa ZZK
0 MAONI YAKO:
Post a Comment