February 21, 2017

 

Imeandaliwa na Luqman Maloto
Weka utaratibu wa kuingiza elimu mpya kwa kila tukio unaloshuhudia katika maisha yako. Hata ukishafikia umri wa makamu uitwe mtu mzima unayetibu. Ndiyo; utu uzima dawa!
Tafsiri ya utu uzima dawa ni kwamba kadiri mtu anavyoongeza miaka, ni sawa na kuongeza dawa mpya kwenye duka lake la dawa. Duka lenyewe la dawa huwezi kuliona hivihivi. Duka la dawa la mtu mzima lipo kwenye ubongo wake.
Duka la dawa la mtu mzima halitibu maradhi kama malaria, kifua kikuu, kisukari na mengineyo. Ubongo wa mtu mzima hutibu maisha. Maana kwa umri wake anakuwa ameshakutana na changamoto nyingi, vilevile ameshaona mengi ya wengi.
Mtu mzima dawa! Ndiyo maana ukimfuata na shida yako ya kimaisha, changamoto na mitihani, yeye anafungua duka lake la dawa kutoka kwenye ubongo wake kisha anakuponya. Ubongo wa mtu mzima huhifadhi mengi.
Mpaka hapo tunaweza kuwa tumeelewana. Sasa basi, hakikisha unaishi ukijifunza ili ukiwa mtu mzima duka lako liwe na aina nyingi ya dawa. Vijana wa wakati huo wakikufuata wamekwama na majaribu ya kimaisha, duka lako la dawa ndani ya ubongo wako liwe na dawa mahsusi.
Utakuwa na dawa nyingi na mahsusi kwa kila ugonjwa wa kimaisha kama utayatumia mapito unayokutana nayo na yale ya wengine unayoyashuhudia kama elimu. Utakuwa mtu mzima hovyo kama hutakuwa na faida kwa vijana wa wakati huo.
Usiishi kama shabiki na mbea wa kusogoa vijiweni. Usiwe mtu wa kushabikia tu kama zuzu. Kila unaloliona, kabla hujashangilia au kuanza kuteta, tafakari peke yako kisha tafuta elimu ndani ya jambo husika.
Elimu huwa haiji katika sura iliyonyooka, bali hupatikana baada ya kuushughulisha ubongo kufikiri. Wakati mwingine elimu ni kama fumbo, hutaipata kama hutalifumbua fumbo.
Mwanasayansi wa Ujerumani, Albert Einstein ambaye ni mmoja kati ya zawadi kubwa na bora kuletwa na Mungu duniani, aliwahi kusema: “Education is not the learning of facts, it’s rather the training of the mind to think.”
Kiswahili: Elimu siyo kujifunza vitu kwa ukweli wake, badala yake ni mafunzo ya akili kuweza kufikiri.
Kwamba unapopata elimu, maana yake inakuwezesha kunoa ubongo kufikiri zaidi. Hivyo ndivyo kila mtu anatakiwa kuishi kila siku za maisha yake ili anapofikia kipindi cha kuitwa mtu mzima awe kweli dawa.
TUSOME NA MANJI
Mfanyabiashara Yusuf Manji kwa mapito yake ya sasa, kwa fedha zake kama alivyo. Utajiri wake mkubwa kama ulivyo. Nguvu zake kama zilivyo. Unganisha na anayopitia kisha tamka; ipo kesho.
Ndiyo; kesho ni baada ya leo. Kesho inaweza kutafsiri matendo ya jana. Kesho inaweza kuwa ni zama mpya. Kesho inaweza kustaajabisha kwa ugeni wake ambao haukupangwa wala kutarajiwa.
Siku zote unapoishi jitazame kisha usisahau kuwa ipo kesho. Ni kesho iliyomfanya Saddam Hussein ambaye ni jabali aliyeitikisa dunia, akamatwe kwenye shimo kama jalala la Uswahilini.
Ni kesho iliyombadili Valentine Strasser kutoka kuwa mtawala wa kijeshi, aliyeogopwa na kila mtu Sierra Leone, hadi kuwa raia hohehe, asiye na hadhi yeyote akihifadhiwa kwenye banda la uani katika nyumba ya mama yake.
Hiyo kesho ndiyo ilimfanya Sisera askari shupavu aliyekuwa kikwazo cha Wana wa Israel kuingia Nchi ya Ahadi kuuawa na mwanamke. Kesho iliwafanya Iddi Amin Dada na Ferdinand Marcos wafe wakiwa wakimbizi pamoja na kwamba tawala zao zilikuwa na nguvu.
Ndugu yangu usije ukaichezea kesho, inaweza kukugeuza chini juu. Ilimtoa Samuel Doe Ikulu ya Liberia akiwa Rais na kuburuzwa mitaani kama mzoga usio na thamani, akakatwa na masikio. Charles Taylor aliyemtenda hayo Doe, leo naye anatumikia kifungo cha maisha jela, Gereza la HM Frankland, Durham, Uingereza.
TUIZUNGUMZE KESHO
Kesho inaweza kukugeuka kwa kusingiziwa au kuonewa. Inaweza pia kuwa matokeo ya mbegu mbaya ambayo mtu binafsi anakuwa aliipanda, muda ukifika inaota na kutoa matunda.
Wewe jiulize, ulitarajia lini Manji angekuwa katikati ya misukosuko, kulazwa mahabusu, kutoka kupelekwa hospitali kisha kurudishwa mahabusu?
Kiongozi gani wa jeshi la polisi au uhamiaji, aliyekuwa na ubavu miaka mitatu iliyopita, kuvitangazia vyombo vya habari kuwa anamtafuta Manji ili amweke mahabusu? Nani aliyekuwa na ujasiri huo? Alikuwa anajitaka au hajitaki?
Miaka mitano iliyopita, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda alikuwa mhangaikaji tu, akipigania kesho yake ya kisiasa ndani ya Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM). Makonda hakuwa lolote wala chochote mbele ya Manji.
Hata hivyo, Februari 2017, inashuhudiwa Makonda ndiye anayemwamuru Manji kufika Kituo Kikuu cha Polisi, Dar es Salaam, halafu Manji analazwa mahabusu. Manji anaishi maisha yenye kumuumiza. Sababu ya yote eti ni Makonda. Amini kuwa ipo kesho, na ikiwadia inaweza kuwa tofauti sana na leo.
Nilishazungumza kuwa kesho inaweza kumgeuka mtu kwa kuonewa, kusingiziwa au kwa kujipandia mwenyewe mbegu mbaya. Hata mapito ya Manji leo yanabeba tafsiri hizo.
Mosi; Manji alipotimuliwa kwenye jengo la Quality Plaza, watu walipongeza. Waliona katendewa haki. Maana jengo aliliuza mwenyewe PSPF kisha akawa anaendelea kulitumia kinyume na utaratibu.
Pili; Manji tuhuma za kuuza dawa za kulevya, kuchimbwa mkwara wa kukamatwa na uhamiaji kwa sababu ya kuajiri wafanyakazi wasiokuwa na vibali, kisha kunyang’anywa hisa zake asilimia 20 alizokuwa anamiliki kwenye kampuni ya Tigo Tanzania, kwa pamoja anaonekana anaonewa.
Aliponyang’anywa Quality Plaza watu walichekelea. Sekeseke za dawa za kulevya, uhamiaji na hisa za Tigo, zinawafanya watu wabadilike, kutoka kumwona Manji mtu tishio zaidi Tanzania, sasa wanamhurumia. Watanzania wanamwona Manji anaonewa.
MASWALI YA KESHO
Kipindi ikiitwa jana, ulitegemea ungefika wakati Watanzania wangemhurumia Manji? Je, ungewaza kuwa angeweza kutokea mtu mwenye ubavu wa kufanya tukio lenye tafsiri ya kumwonea Manji?
Manji huyuhuyu aliyempeleka puta bilionea Reginald Mengi na utu uzima wake? Manji anayejikubali, anayejiamini na anayetambua nguvu ya fedha alizonazo. Ungewaza atokee mtu wa kusemwa anamwonea Manji?
Ni huyuhuyu Manji ambaye hata akihama Tanzania bado uwekezaji wake katika mataifa kama Uingereza, India, Japana, Marekani, Canada na kwingineko bado ataendelea kuwa tajiri? Leo hii watu wanashika tama kumsikitia kuwa anaonewa? Manji!
Ni hapo ndipo unaweza kuiona kesho na mabadiliko yake. Aliyeogopwa jana leo anaweza kudharauliwa au kuhurumiwa. Inategemea na jinsi ambavyo kibao kimegeuka kwa sura gani.
Anayependwa sana leo kesho ikifika anaweza kuchukiwa kwa chuki ya laana mithili ya binadamu kwa nyoka. Kesho inapowadia mwenye kupapatikiwa na watu anaweza kutengwa, tena kwa utengano wa laana kama ilivyotokea kwa ibilisi na malaika.
Mbona Goliath alikuwa mbabe wa vita asiyeshindwa lakini aliuawa kwa jiwe la mtoto mdogo, Daud, aliyerusha kwa kutumia kombeo? Kesho ni kikombe, ukishaandikiwa na Mungu ukinywe ni lazima ukinywe tu.
Nani aliyetarajia Musa angemzamisha Firauni Bahari ya Sham? Firauni amekuwa ni mfano bora zaidi wa kusimuliwa kwa mtu aliyevuna matokeo mabaya ambayo alijiandalia kwa miaka mingi kabla.
UJUMBE MAHSUSI
Je, kuna mtu anakunyanyasa kwa sababu ya fedha zake? Ongea na nafsi yako kuwa ipo kesho. Yapokee manyanyaso ya mnyanyasaji kwa tabasamu maana hajui alitendalo.
Hata uwe katika kipindi kigumu kiasi gani, elewa kuwa ipo kesho. Na itakapofika kesho haitafanana na leo. Kesho ina kawaida ya kugeuza taswira chini juu na juu chini.
Nani mlevi wa madaraka anayewanyanyasa wenzake? Mshangae na umdharau kwa maana huyo ni limbukeni. Hajui kuwa itafika kesho na hayo mamlaka hatakuwa nayo.
Unapokuwa tajiri hata uwe mkubwa wa kiasi gani, ukiwa na madaraka makubwa na yenye kukupa nguvu za kiasi gani, njia pekee ya kujiandalia kesho nzuri ni kuwa mnyenyekevu. Tambo zina mwisho wake.
Ukiwa na afya imara yenye kukupa ujasiri na jeuri ya kupambana na yeyote, hakikisha unakuwa mnyenyekevu. Usitumie afya yako vibaya. Mbabe wa ulingo, Mohammad Ali, aliyekuwa anawachakaza wababe wenzake atakavyo, alikufa akiwa hajiwezi, mwili dhaifu, akitetemeka.
Dunia haisimami, inazunguka. Ndiyo maana unaweza kunyanyaswa wewe leo na mwenye fedha halafu kesho ikifika wewe ndiye ukawa tajiri zaidi yake. Usidanganywe wala kuogopeshwa na leo. Vuta subira kesho itafika.
Dunia ina mizunguko miwili, inalizunguka jua kisha yenyewe inajizungusha kwenye mhimili wake, kwa hiyo usiogope sana anapotokea mtawala akawa anakunyanyasa, elewa kuwa inaweza kufika kesho wewe ukawa kiongozi na ukamuongoza kiongozi wa leo.
Ipo kesho ni somo la hekima kwa kila binadamu. Linafundisha subira na unyenyekevu. Linafundisha uvumilivu na kujidhibiti. Mnyonge wa leo asubiri kesho na avumilie wakati akiingoja kesho.
Aliye na nguvu leo awe mnyenyekevu maana kesho itafika. Adhibiti nguvu zake za kifedha au mamlaka, kwani ipo kesho ambayo itabisha hodi na hataweza kujua mapema kesho itakuwa na matokeo gani.
Ukiona kiongozi anastaafu vizuri na anaishi raha mustarehe nje ya madaraka aliyokuwa nayo, ujue alijidhibiti kwa ajili ya kesho yake.
Ukimwona mzee amezeeka vizuri, ujue aliuishi ujana wake kwa unyenyekevu ili kuiandaa vizuri kesho yake.
Tambo nyingi humtumbukiza mtambaji shimoni. Hivyo ishi kila siku ukijiwekea akiba ya kesho.
Ndimi Luqman MALOTO

0 MAONI YAKO:

Post a Comment

Popular Posts

WADAU

BLOG ZINGINE