Kesi ya unyang’anyi wa kutumia silaha na kujeruhi inayomkabili Salum
Njetwe maarufu ‘Scorpion’ imekwama kuendelea kusikilizwa kwa mara ya
tano mfululizo baada ya Hakimu alinayesikiliza shauri hilo kuwa mgonjwa.
Kesi hiyo iliyopo Mahakama ya Wilaya ya Ilala, imeshindwa kuendelea leo
Alhamisi baada ya Hakimu Mkazi, Flora Haule anayesikiliza shauri hilo
kuwa mgonjwa na kushindwa kufika mahakamani.
Kutokana na hali hiyo, Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Ritha Tarimo aliahirisha kesi hiyo hadi Juni 20, mwaka huu.
Mpaka sasa mashahidi wanane wa upande wa mashtaka wameshatoa ushahidi
wao dhidi ya mshtakiwa Scorpion anayekabiliwa na mashtaka mawili
likiwemo la unyang’anyi wa kutumia silaha.
Wakili wa Serikali, Chesensia Gavyole alidai mahakama hapo kuwa upande
wa mashtaka tayari ulikuwa na shahidi ambaye alipaswa kuendelea kutoa
ushahidi leo.
Itakumbukwa kuwa April 18, mwaka huu, kesi hiyo ilishindwa kuendelea
baada ya shahidi kuwa mgonjwa na kushindwa kufika mahakamani.
Mei 2, mwaka huu kesi hiyo iliahirishwa baada shahidi namba nane, ambaye
alitakiwa kuulizwa maswali na wakili wa utetezi, kuwa mgonjwa kwa mara
ya pili.
Pia, Mei 15, mwaka huu, kesi hiyo ilishindwa kuendelea baada ya upande
wa mashtaka kutokuwa na shahidi na Mei 25 kesi hiyo iliahirishwa
kutokana na wakili wa utetezi, Juma Nassoro kushindwa kufika mahakamani.
Kwa mujibu wa hati ya mashtaka, Scorpion alitenda kosa hilo Septemba 6,
2016 Buguruni Sheli wilayani Ilala, ambapo alimjeruhi Said Mrisho.
Katika shtaka la kwanza, Scorpion anadaiwa kuiba cheni moja ya shingoni
aina ya silva yenye uzito wa gramu 34 ikiwa na thamani ya Sh60,000,
bangili moja ya kiume yenye thamani ya Sh85,000 , pochi na fedha
taslimu Sh331,000 na kwamba thamani ya vitu vyote ni Sh476,000 mali ya
Mrisho.
Katika shtaka la pili, mshtakiwa alimjeruhi kwa kumchoma kisu Mrisho
sehemu ya machoni, mabegani na tumboni ili aweze kujipatia mali hizo
bila kikwazo.
0 MAONI YAKO:
Post a Comment