Yanga iliipiga Ruvu Shooting mabao 7-0 juzi Jumamosi ikiwa ni siku
chache baada ya kuiondosha Komorozine ya Comoro kwenye Ligi ya Mabingwa
Afrika kwa jumla ya mabao 12-2.
Okwi ambaye katika ushindi dhidi ya Ruvu Shooting alipiga bao moja,
alisema: “Ninavyoona morali ya wachezaji wenzangu, sidhani kama kuna
timu inaweza kutuzuia kwa sasa, ngoja twende kambini tukajiandae na
mchezo ujao (dhidi ya Ahly wa Ligi ya Mabingwa) hatuwezi kuiogopa timu
yoyote kwani kikosi chetu kipo imara.”
Katika mchezo huo, Okwi alipiga pasi za maana zaidi ya 28. Alipiga
mashuti mawili yote yakilenga lango na kichwa kimoja huku akionyesha
uelewano mkubwa na Simon Msuva, Hamis Kiiza, Kavumbagu na Mrisho Ngassa.
Kavumbagu kwa upande wake alisema mabao hayo waliyoifunga Ruvu
Shooting, ni salamu kwa timu nyingine yoyote watakayokutana nayo,
kutokana na kikosi chao cha kwanza kuundwa na viungo washambuliaji wenye
kasi ya aina yake.
“Kurejea kwa Okwi kumeimarisha kikosi chetu katika safu ya
ushambuliaji inayoundwa na wachezaji wote wenye uwezo mkubwa ndani ya
uwanja, hali hii inanipa matumaini ya kuendelea kupata ushindi wa mabao
mengi katika kila mechi,” alisema Kavumbagu ambaye ni raia wa Burundi.
Mshambuliaji Hamis Kiiza, alisema: “Hizo ni salamu kwa wapinzani wetu
wote kuanzia kwenye Ligi Kuu na hata kimataifa, lazima waweke hofu
dhidi yetu na hilo ndilo linalotakiwa, hatutakubali kushuka kwenye
kiwango hiki kwani lengo letu ni kutwaa ubingwa wa Bara na hata kufanya
vizuri kimataifa.”
Source: Mwanaspoti
Source: Mwanaspoti
0 MAONI YAKO:
Post a Comment