Mawaziri wa nje wa Umoja wa Ulaya wanakutana mjini Brussels kukiwa na
wito ushirikiano wa karibu zaidi kati ya Ulaya na ulimwengu wa Kiarabu
katika kukabiliana na makundi ya itikadi kali.
Mkuu wa Sera za Nje wa Umoja wa Ulaya, Federica Mogherini (kushoto),
akisalimiana na Waziri wa Mambo ya Nje wa Uhispania, Jose Manuel
Garcia-Margallo.
Mkuu wa sera za nje wa Umoja wa Ulaya, Federica Mogherini, amesema hivi
leo kwamba Ulaya inahitaji kuwa na muungano wa aina fulani na nchi za
Kiarabu na kuimarisha njia ambapo pande hizo mbili zinashirikiana.
Mogherini aliyazungumza hayo baada ya kukutana na Katibu Mkuu wa Jumuiya
ya Nchi za Kiarabu, Nabil el-Arabi, wakati mawaziri wa mambo ya nje wa
Umoja wa Ulaya wakiwa mjini Brussels kuandaa mkutano wa kilele wa
viongozi wa Umoja huo wanaokutana mwezi ujao kuzungumzia tatizo la siasa
kali.
Baadhi ya mawaziri hao, akiwemo Philip Hammond wa Uingereza,
wamesisitiza umuhimu wa Ulaya kushirikiana na nchi za Kiislamu badala ya
kuzilaumu kwa tatizo hilo. Hammond ameongeza kuwa Ulaya kwa ujumla wake
imejitolea kufanya kila iwezalo ili iendelee kubaki salama
"Tutaamua kufanya kile kilicho muhimu kuibakisha Ulaya salama dhidi ya
vitisho vya magaidi. Jukumu letu ni kuzungumzia changamoto ya makundi ya
siasa kali inayotukabili sasa na namna tunavyochukuwa hatua kukabiliana
nayo," alisema Hammond.
Hakuna suluhisho bila kukomesha vita Mashariki ya Kati
Waziri wa Mambo ya Nje wa Sweden, Margot Waalstrom, amesema hakuna suluhisho la haraka dhidi ya changamoto la wapiganaji wa kigeni barani Ulaya, kabla ya kwanza kumaliza vita nchini Syria na Iraq.
Mwenzake wa Ubelgiji, Didier Reynders, ambaye nchi yake ilitegua njama ya mpiganaji mmoja aliyetambuliwa kuwa Muislamu mwenye siasa kali kuwauwa polisi, ametoa wito kwa Bunge la Ulaya kukubaliana na ombi la kuanzisha rikodi ya pamoja ya abiria.
"Ninatazamia kuwa Bunge la Ulaya litabadilisha mtazamo wake na kuamuru kuanzishwa Rikodi ya Majina ya Abiria kwenye kiwango cha Ulaya na pia kwa kushirikiana na wadau wengine kama vile Marekani na Canada," alisema Reynders.
Ikiwa bunge la Ulaya litakubaliana na pendekezo hilo, wasafiri wote wanaovuuka mipaka ya upande mmoja hadi mwengine watakuwa kwenye rikodi ya pamoja kwa mataifa yote wanachama na washirika.
Sehemu ya kwanza ya mkutano huo wa mawaziri wa mambo ya nje wa Umoja wa Ulaya ilimalizika leo mjini Brussels kwa makubaliano ya kuukatia rufaani uamuzi wa Mahakama ya Umoja wa Ulaya wa hapo Disemba 17, ambao uliliondoa kundi la Hamas kwenye orodha ya makundi ya kigaidi.
Mwandishi: Mohammed Khelef/AFP/Reuters
0 MAONI YAKO:
Post a Comment