Sehemu za ndani ya mikoa ya Tanzania zikiwa kame.
Watanzania wanalaani hali ya hewa na kuongezeka kwa joto wakati
usambazaji wa maji mijini ukidorora na huku mabishano yakizidi kuwa
makali baina ya wakulima na wafugaji kuhusu matumizi ya vijito katika
maeneo yao.
Taarifa nyingi za kitaalam siku za nyuma zilionya kuhusu uongezekaji wa
mahitaji ya maji na viwango vya maji yanayopatikana lakini tahadhari
hizo ama zilipuuzwa au hazikutiliwa maanani ipasavyo.
Mara nyingi wanasiasa walibeza tahadhari hizo bila kufikiri pale
walipowapotosha wananchi wao kuvamia mazingira yaliyohifadhiwa ili
wakate miti, kuanzisha makazi au kulima mashamba karibu na vyanzo vya
mito.
Miji ambayo imepanuka kwa haraka katika maeneo ambayo hapo awali
yalikuwa na vijito vingi, kama vila Morogoro na Tanga katika ukanda wa
mashariki, sasa inapata adha nyingi kuanzia mazingira machafu mpaka
uhaba wa shughuli za kiuchumi kutokana na ukosefu wa maji.
Jiji kuu la biashara na viwanda, Dar es Salaam, pia limekumbwa na adha
hizo. Mamia ya wakazi wa jiji hili hutumia saa nyingi kila siku
wakitafuta maji. Matatizo yao huenda yasikomee hapo kadiri gharama za
upatikanaji maji zinavyozidi kupanda siku hadi siku.
Mameneja wa rasilimali hii pia wanasumbuka kuziba mabomba yanayovuja
huku wakipambana na wizi wa maji pale ambapo watu hujifungia mabomba
isivyo halali, wakati viwango vya maji vikishuka kule yanakotoka kabla
ya kuingizwa katika mifumo ya usambazaji.
“Uhai wetu, ustawi wetu, afya zetu na maendeleo yetu vyote hutegemea
upatikanaji maji safi na salama pale tunapoishi. Wakati umefika tuone
kila anayeharibu chanzo cha maji ni adui,” amesema Profesa Jumanne
Maghembe, Waziri wa Maji wakati wa kuzindua mradi wa maji katika
manispaa ya Moshi.
Waziri huyo aliongeza kuwaTanzania imepoteza viumbe hai na mimea kwa
wingi katika kipindi cha miaka miwili iliyopita kutokana na uharibifu wa
mazingira asili ambayo yalihifadhi vyanzo vya maji.
Hivi karibuni athari za kukauka kwa mito zimewasibu wananchi katika
sehemu mbalimbali za Tanzania. Hata hivyo hakuna juhudi thabiti
zinazofanywa na jamii au asasi za serikali kukabili athari zaidi za
kimazingira, kijamii, kiuchumi na hata za kisiasa ambazo huenda
zikasababishwa na hali hii.
Mto wa Ruaha ambao ulikuwa na maji mengi kila mwaka ni mfano dhahiri.
Viongozi wa kitaifa ambao huambaa mto huu wakiwa katika magari
wanaposafiri kwenda au kutoka mikoa ya kusini ya nchi, sana sana
hushangaa wakisema kuwa mto hauungurumi tena kama zamani.
Mto huu ulikuwa maliasili kubwa ambayo iliwezesha taa kuwaka na viwanda
kuzalisha mali kwa gharama ya chini katika miji mingi kutokana na umeme
uliofuliwa kwa maji ya Bwawa la Mtera na kituo cha umeme cha Kidatu
katika Mkoa wa Morogoro.
Bila mto huu, nini itakuwa hatima ya Hifadhi ya Taifa ya Ruaha na
shughuli za kitalii ambazo hivi karibuni zimepanuka katika eneo hilo?
Hili ni baa ambalo linaanza kujitokeza lakini linazuilika ikiwa hatua
makini zitachukuliwa kuwa na mifumo endelevu ya kilimo na kudhibiti
matumizi ya maji ya Ruaha kwa kilimo cha umwagiliaji cha mpunga.
Watu wengi huharakisha kulaumu mabadiliko ya tabia nchi kwa kila mkasa
hata kama wamekosa kuwa waangalifu wenyewe katika mwenendo wao wa maisha
katika mazingiza yao.
Majadiliano kuhusu mkataba wa kimataifa juu ya mabadiliko ya hali ya
hewa, ambao unategemewa kufikiwa na mataifa yote mwaka 2015, bado
yanasuasua kutokana na kutoaminiana baina ya nchi zilizostawi na zile
zinazoendelea.
Ili Tanzania iaminike katika jukwaa la majadiloiano hayo ya kimataifa,
watumishi wake wa umma ambao hutetea maslahi ya taifa hapana budi
wajumuike na viongozi wa jumuia za wananchi pamoja na wanasiasa
kuonyesha kuwa wanao utashi wa kisiasa kupunguza athari za mabadiliko ya
hali ya hewa katika ngazi ya taifa.
Mwandishi: Anaclet Rweyagura/DW Dar es Salaam
Mhariri: Mohammed Khelef
Mhariri: Mohammed Khelef
0 MAONI YAKO:
Post a Comment