September 22, 2015

 
  Utafiti uliofanywa na taasisi ya utafiti ya TWAWEZA umeonesha kuwa endapo uchaguzi ungefanyika mwezi mmoja uliopita, mgombea urais wa CCM John Magufuli angepata ushindi kwa asilimia 65.
 Matokeo ya utafiti huo yametolewa leo jijini Dar es salaam ambapo yameonesha pia kuwa wagombea wa CCM katika ngazi zote ikiwa ni pamoja na ubunge na udiwani CCM inaongoza.
Asilimia 62 ya wananchi wanasema kwamba wanajisikia wapo karibu zaidi na chama cha CCM kuliko vyama vingine. Aidha, walipoulizwa watawachagua wagombea wa chama gani – bila kutajiwa majina ya wagombea – wananchi 6 kati ya 10 walisema kwamba watawachagua wagombea wa CCM kwa Urais (66%), Ubunge (60%) na Udiwani (60%). Takwimu hizi zinatoa picha kwamba CCM inaungwa mkono, kama ilivyokuwa mwaka 2012.

 

Chadema ni chama cha pili kinachopendwa kushinda vyama vingine vya upinzani. Lakini wananchi wanaosema kwamba watawachagua wagombea wa Chadema kwa Urais, Ubunge na Udiwani wamepungua kidogo. Ikumbukwe kuwa, inawezekana wananchi wanaopenda zaidi mseto wa Ukawa waliunga mkono vyama vya CUF, NCCR-Mageuzi au NLD.
Mbali ya CCM na vyama vinavyounda Ukawa, chama cha ACT-Wazalendo kilitajwa na zaidi ya asilimia moja ya wananchi.

Walipoombwa kutaja moja kwa moja jina la mgombea Urais ambaye wangemchagua, asilimia 65 ya wananchi walimtaja mgombea wa CCM, John Magufuli. Asilimia 25 walimtaja mgombea wa Chadema (na Ukawa), Edward Lowassa. Asilimia 10 iliyosalia iligawanyika kati ya wale waliomtaja mmoja miongoni mwa wagombea urais wengine, waliokataa kujibu na waliokuwa bado hawana mgombea waliyempendelea. Hata hivyo, takwimu zilikusanywa kabla vyama vingine, kikiwemo ACT-Wazalendo, kuteua wagombea wao wa Urais. Takwimu hizi (zilizokusanywa kati ya Agosti na Septemba) sio utabiri wa matokeo ya uchaguzi. Zinaonyesha tu kwamba mwanzoni mwa kipindi cha kampeni, mgombea Urais wa CCM, John Magufuli, alikuwa anaongoza katika kura za maoni.
Hata hivyo, wananchi hawana taarifa sahihi juu ya nafasi rasmi ya Ukawa kama mseto. Asilimia 49 ya wananchi wanafikiri kwamba Ukawa ni chama cha siasa kilichosajiliwa, kinyume na hali halisi. Asilimia 57 wanafikiri kwamba neno ‘Ukawa’ litakuwepo kwenye karatasi zao za kupigia kura. Hii pia, sio kweli. Bila kampeni na juhudi za kuwaelimisha wapiga kura ili wawe na taarifa sahihi kuhusu jambo hili, hali hii inaweza kuleta wasiwasi siku ya uchaguzi.

Matokeo haya yalitolewa na Twaweza katika muhutasari wa utafiti mwenye jina la Waache Sema mwananchi, sema | Maoni ya wananchi kuhusu uongozi wa kisiasa. Muhtasari huu umetumia takwimu kutoka Sauti za Wananchi, utafiti wa kwanza barani Afrika unaotumia simu za mkononi na wenye uwakilishi wa taifa zima. Matokeo yanatokana na Awamu ya 1 ya kuwapigia simu wahojiwa wapya 1,848 iliyoendeshwa kati ya Agosti na Septemba 2015. Wahojiwa waliteuliwa kwa kutumia njia kama zinavyotumika na asasi za utafiti duniani kote. Unasibu (sampling) huu ulifanyika katika mikoa yote ya Tanzania Bara. Takwimu hizi zimelinganishwa na zile za awamu za utafiti katika miaka ya nyuma, zikiwemo:
  • Utafiti wa awali wa kwanza wa Sauti za Wananchi 2012
  • Sauti za Wananchi Awamu ya 10 ya Octoba 2013
  • Sauti za Wananchi Awamu ya 24 ya Septemba 2014
  • Awamu za utafiti za Sauti za Wananchi Aprili-Julai 2015
  • Utafiti mpya wa awali ulioendeshwa kati ya Julai na Agosti 2015

Related Posts:

0 MAONI YAKO:

Post a Comment

Popular Posts

WADAU

BLOG ZINGINE