Naibu
Waziri waAfya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia , Wazee na Watoto, Dkt.Hamisi
Kigwangalla akifafanua jambo kuhusu uamuzi wa Serikali kuhusu Tiba
Asili na TibaMbadala katika mkutano wa waandishi uliofanyika jana
kwenye ukumbi wa mikutano wa wizara hiyo. Kushoto ni Waziri wa Wizara
hiyo, Ummy Mwalimu.
Baadhi ya Wakurugenzi waWizara hiyo wakiwa katika mkutano huo. Picha na Catherine Sungura- (WAMJW).
Katika nchi
yoyote ile uhuru usio na mipaka ni jambo la hatari; lakini pia hakuna
haki isiyo na wajibu. Vivyo hivyo, katika huduma za Tiba Asili na Tiba
Mbadala hapa nchini kuna Sheria, Kanuni na Taratibu za Maadili
zinazoweka masharti, uhuru na mipaka; pia haki na wajibu wa kila mdau.
Huduma za tiba asili na tiba mbadala ni huduma zinazotambulika na
Jamhuri yetu, watu wake na ina thamani kubwa. Aidha, ni huduma
inayotambuliwa na sayansi ya tiba ya kisasa. Hata hivyo huduma hizo
zimekumbwa na changamoto mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuwepo kwa watoa
huduma wasiozingatia Sheria, Kanuni na Miongozo mbalimbali. Kutokana na
hali hiyo na kutokana na ziara ya Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya
Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mhe. Dkt. Hamisi A. Kigwangalla (Mb) kwa
Tabibu Juma Mwaka Juma tarehe 14/12/2015 na kufuatia uchambuzi
uliofanywa na Wizara baada ya ziara hii, Wizara imebaini changamoto
zifuatazo:-
1.Huduma za tiba asili na au tiba mbadala zinatolewa na watoa huduma wasiosajiliwa na Mamlaka husika kwa mujibu wa Sheria.
2.Uwepo wa vituo vinavyotoa huduma za Tiba Asili na au Tiba Mbadala bila kusajiliwa kwa mujibu wa Sheria.
3.Kutolewa dawa kwa wagonjwa bila dawa hizo kusajiliwa na mamlaka husika.
4.Uingizaji na matumizi ya vifaa vya uchunguzi ambavyo havijasajiliwa na mamlaka zinazohusika, na
5.Utoaji
wa matangazo bila ya kufuatwa kwa matakwa ya sheria, Kanuni na Miongozo
iliyopo. Aidha baadhi ya matangazo hayo yamekuwa na taarifa zinazoweza
kuleta madhara na kupotosha Umma wa Watanzania.
Kutokana na
hali hiyo, Wizara itahakikisha kuwa huduma za tiba asili na tiba
mbadala zinatolewa kwa kuzingatia Sheria, Kanuni na Miongozo iliyopo.
Lengo ni kuwezesha huduma za tiba asili na tiba mbadala zinakuwa huduma
rafiki na salama kwa watumiaji. Tunao wajibu wa kuwalinda wananchi, vile
vile tunaowajibu wa kuweka mazingira mazuri kwa watoa huduma za tiba
asili na tiba mbadala ili kufanya shughuli zao vizuri.
Hivyo kwa upande wetu Wizara itahakikisha kuwa:-
1.Baraza na sehemu inayosimamia huduma za Tiba Asili na Tiba Mbadala inakuwa na watumishi wa kutosha kwa mujibu wa Ikama.
2.Kunakuwa na Mpango Mkakati wa muda mrefu kuwezesha kufanikisha uboreshaji wa huduma za tiba asili na tiba mbadala nchini.
3.Watoa huduma wote, vituo vyote vya kutolea huduma, dawa na vifaa na vifaa tiba vinavyotumika vinasajiliwa.
4.Utaandaliwa
mwongozo wa mafunzo kwa watoa huduma wote nchini, kuhusu namna ya
kuweka kumbukumbu za wagonjwa, kutoa rufaa kwa wagonjwa na kutengeneza
dawa zilizo bora.
5.Kunakuwa
na mawasiliano na Wizara zinazohusika na habari na mawasiliano ili
kuboresha utoaji matangazo yanayohusu Tiba Asili na Tiba Mbadala.
6.Kunakuwa
na mawasiliano na Ofisi ya Rais TAMISEMI na Taasisi za Utafiti ili
kuboresha huduma za tiba asili na tiba mbadala nchini.
7.Tutafanya
mabadiliko ya Sheria ili kuongeza kiwango cha adhabu kwa watakaokiuka,
na pia tunakusudia kuondoa Kanuni inayoruhusu matangazo kwa idhini ya
Baraza kwa sababu inaweka mianya ya matumizi mabaya ya fursa ndogo ya
matangazo inayotolewa.
Katika
kufanikisha hayo, Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na
Watoto inatoa maelekezo yafuatayo kwa watoa huduma na jamii:-
1.Hairuhusiwi
kwa mtu yeyote kutoa huduma za tiba asili na au tiba mbadala bila
kusajiliwa. Ninalielekeza Baraza la Tiba Asili na Tiba Mbadala
kuhakikisha kuwa watoaji huduma wote wanasajiliwa kwa mujibu wa Sheria:
(a) Mijini, (Majiji, Manispaa na Miji) – usajili wao ukamilike katika kipindi cha miezi mitatu; kuanzia Januari 15, 2016 na
(b) Vijijini, Halmashauri zote zilizobaki – usajili wao ukamilike katika kipindi cha miezi sita kuanzia Januari 15, 2016.
Hatua kali za kisheria zitachukuliwa kwa yeyote atakaye puuza kujisajili katika kipindi hicho
2.Hairuhusiwi
kuuza na au kugawa dawa yoyote ile ya tiba asili au tiba mbadala mpaka
iwe imesajiliwa na Baraza baada ya kuchunguzwa na Wakala wa Maabara ya
Mkemia Mkuu wa Serikali kuwa ni salama na kupewa kibali na Mamlaka ya
Chakula na Dawa (TFDA).
3.Hairuhusiwi kuendesha kituo cha kutolea huduma za tiba asili na au tiba mbadala bila kukisajili.
4.Wizara
inapiga marufuku kwa mtu binafsi au taasisi yoyote ile kutumia kifaa au
kifaa tiba chochote bila kukisajili TFDA na kupewa kibali; na
5.Matangazo
yote yanayohusu Tiba Asili na Tiba Mbadala ambayo hayajapitishwa na
Baraza yamezuiliwa kuanzia leo tarehe 15/1/2016. Wizara inavitaka vyombo
vya Habari hasa Televisheni, Radio na Magazeti kuzingatia Sheria na
Kanuni za Tiba Asili na Tiba Mbadala inayozuia matangazo ambayo
hayajachunguzwa na Baraza. Ni wajibu wa vyombo vya habari kujiridhisha
na Mamlaka husika yaani Baraza kabla ya kutoa tangazo lolote linalohusu
Tiba Asili na Tiba Mbadala. Wizara itashirikiana na Mamlaka
zinazohusika na habari na mawasiliano kutekeleza agizo hili. Vile vile,
hairuhusiwi kutoa elimu kwa umma kupitia vyombo vya habari na mikutano
ya hadhara kuhusu tiba asili na tiba mbadala.
Katika
kuwezesha ulinzi wa afya za wananchi, kila mmoja wote alinde afya yake
kwa kuhakikisha kuwa huduma anayopata ya tiba asili na tiba mbadala ni
kwa mujibu wa Sheria, Kanuni na Miongozo inayotolewa na Waziri wa Afya,
Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto. Ni uhakika uliowazi kuwa
kwa pamoja tukiboresha huduma za tiba asili siyo tu tutaboresha afya
zetu bali pia tutaweza kuuza dawa na huduma hizo nje ya nchi na kupata
fedha za kigeni kupitia na hivyo kuboresha uchumi wa mtu mmoja mmoja,
jamii na nchi kwa ujumla.
Kwa pamoja tushirikiane kuboresha huduma za tiba asili na tiba mbadala nchini. INAWEZEKANA.
Ummy A. Mwalimu (Mb)
WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII,
JINSIA, WAZEE NA WATOTO
15 Januari, 2016
0 MAONI YAKO:
Post a Comment