March 07, 2016

Rais wa Vietnam kuzuru Tanzania kwa ziara rasmi
Rais Truong Tan Sang wa Vietnam, anatazamiwa kuwasili nchini Tanzania kwa ziara rasmi ya kiserikali hapo kesho akifuatana na ujumbe mzito katika ziara hiyo. Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Ikulu ya Dar es Salaam, Rais Tan Sang ataandamana na mawaziri watano wa serikali yake na wafanyabiashara wapatao 51.

Hii ni ziara ya kwanza ya rais wa nchi kuzuru Tanzania tangu Rais John Pombe Magufuli aingie Ikulu na ziara ya kwanza kwa rais huyo wa Vietnam kuzuru Afrika. Baada ya Tanzania Rais Truong Tan Sang ataelekea nchini Msumbiji. Akiwa jijini Dar es Salaam, rais huyo wa Vietnam mbali na kuzungumza na Rais Magufuli, atakutana na Mwenyekiti wa chama tawala CCM, rais mstaafu wa Awamu ya Nne, Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Zanzibar Dk Ali Mohamed Shein, Spika wa Bunge Job Ndugai na kushiriki dhifa ya kitaifa katika Ikulu. Imeelezwa kuwa, baada ya kuwasili jioni ya kesho Jumanne, Rais Tan Sang atafanyiwa mapokezi rasmi siku ya Jumatano Ikulu, ambapo atapigiwa mizinga 21 na kukagua gwaride rasmi la jeshi la ulinzi na usalama. Baadaye marais hao wawili wa Tanzania na Vietnam mbali na mazungumzo ya pande mbili, watatia saini mikataba kadhaa ya maendeleo. Kwa mujibu wa mikataba hiyo, wafanyabiashara wa nchi mbili hawatatozwa kodi mara mbili kwa biashara na uwekezaji watakaoufanya katika mataifa hayo.

0 MAONI YAKO:

Post a Comment

Popular Posts

WADAU

BLOG ZINGINE