Pampu iliyowahi kukamatwa na mafundi wa Shirika la Majisafi na Majitaka
Jijini Dar es salaam (Dawasco) iliyokuwa ikivuta Maji kiholela kutoka
kwenye laini ya bomba kubwa
SHIRIKA la Majisafi na Majitaka jijini Dar es Salaam (Dawasco)
linawashikilia mama ntilie sita kwa madai ya kutumia huduma ya maji
kinyume cha utaratibu,anaandika Eunice Laurian.
Mama hao wanadaiwa kujiunganisha majisafi kienyeji katika Mtaa wa Kisutu, Ilala jijini Dar es Salaam.
Akizungumza katika eneo la tukio Deogratius Ng’wandu, Ofisa Biashara
wa Dawasco amesema kuwa, wamebaini wizi huo wakati wa operashani
maalum inayoendelea kwa sasa kwenye maeneo yote Dar es Salaam.
“Tumewakuta mamantilie wakiwa wanatumia huduma ya maji ambayo
imeunganishwa kinyume cha taratibu, maji hayo hayakuwa na mita
wala akaunti namba,” amesema Ng’wandu.
Subira Ngeseyani, Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa Kisutu
amewaomba wananchi kutoa ushirikianao kwa kuwataja wezi wa maji
katika mitaa yao kama ilivyoagiza na Paul Makonda, Mkuu wa Mkoa wa
Dar es Salaam.
Aziza Hassan ambaye ni mtuhumiwa amekiri kutumia huduma ya maji kinyume na taratibu za Dawasco kwa madai ya kutojua.
“Kweli tumekuwa tukitumia huduma ya maji kwenye eneo hili kwa
kutojua kutokana na hali ngumu ya maisha lakini pia kuunganisha
huduma hii ni gharama kubwa,” amesema Aziza.
Source: mwanahalisionline
0 MAONI YAKO:
Post a Comment