Waislamu nchini Marekani, wamesema kuwa maneno ya chuki dhidi ya
dini tukufu ya Kiislamu yanayotolewa na viongozi wa chama cha
Republican, ndiyo sababu ya kuongezeka hujuma na mashambulizi dhidi ya
Waislamu nchini humo.
Taarifa iliyotolewa jana na viongozi wa jumuiya za Waislamu nchini
Marekani mbele ya waandishi wa habari mjini Washington imemtaka Donal
Trump, anayewania kuteuliwa na chama cha Republican kugombea urais
nchini Marekani, kuwaomba radhi Waislamu kutokana na matamshi yake ya
hivi karibuni yaliyojaa chuki dhidi yao. Itakumbukwa kuwa Jumatano usiku
wakati akizungumza na kanali ya televisheni ya CNN, Trump alisema kuwa
Uislamu unachafua sura ya Marekani. Nihad Awad, Mkurugenzi wa Baraza la
Mahusiano la Kiislamu nchini Marekani amesema kuwa, Trump lazima awaombe
radhi Waislamu ambao baadhi yao wanahudumu jeshini, kama ambavyo pia
kuna madaktari Waislamu wanaookoa maisha ya mamilioni ya Wamarekani na
pia kuna maafisa wa ngazi tofauti serikalini wanaowahudumia raia. Aidha
amesisitiza kuwa, mgombea huyo wa nafasi ya urais kwa tiketi ya chama
cha Republican anatakiwa kuwaomba radhi wanawake Waislamu ambao kutokana
na kuvaa kwao vazi la Kiislamu la hijabu, wananyanyasika na kutengwa
katika idara za serikali na mashuleni nchini Marekani. Kabla ya hapo pia
jumuiya za Kiislamu nchini Marekani zilikuwa zimetahadharisha kwamba,
matamshi ya kichochezi ya Donald Trump, yanawaweka hatarini Waislamu
nchini humo.
0 MAONI YAKO:
Post a Comment