Serikali
kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto
imesikitishwa na kukemea vikali tukio la mzazi kumbaka na kumlawiti
mtoto wake wa kufikia mwenye umri wa mwaka mmoja na nusu, kitendo
kilichofanywa na John Donald (35) mkazi wa Kiyangu, Manispaa ya
Mikindani mkoani Mtwara.
Tukio
hili la kubaka na kulawitiwa ni ukatili wa hali ya juu dhidi ya mtoto
maana husababisha maumivu makali ikiwa ni pamoja na kumdhuru mtoto
kimwili, kisaikolojia, kijamii na kihisia. Aidha, vitendo hivi, vinaacha
kovu la kudumu kimwilini, kiakili, kimaadili, kijamii, ulemavu,
maumivu, na wakati mwingine husababisha kifo; jambo ambalo linahitaji
ulinzi thabiti katika kuhakikisha watoto wanaishi mazingira salama na
rafiki.
Ukatili
alilofanyiwa mtoto eneo la Kinyangu, manispaa ya Mikindani, ni
ukiukwaji mkubwa wa haki za mtoto ambao huchangia kurudisha nyuma ustawi
na maendeleo ya Mtoto na ni kinyume cha Sheria ya Mtoto Na. 21 ya mwaka
2009.
Wizara
inatoa pongezi kwa Jeshi la Polisi mkoani Mtwara kwa kumkamata
mtuhumiwa na kumfikisha mahakamani ili hatua za kisheria zichukuliwe.
Vile vile, Wizara inaipongeza Mahakama ya Wilaya ya Ilala, mkoani Dar es
salaam dhidi ya Omary hamisi (25), mkazi wa Gongo la Mboto, Dar es
salaam, ya kutumikia kifungo cha maisha jela, baada ya kupatikana na
hatia ya kumlawiti mtoto wa miaka tisa mwenye ulemavu wa kusikia na
kuongea. Uamuzi huu ni kielelezo kuwa, wananchi wakitoa ushahidi wa
matukio ya ukatili dhidi ya watoto, watuhumiwa watachukuliwa hatua kali
ili kuwa fundisho kwa wananchi wanaowanyanysa watoto.
Wizara
inamwelekeza Afisa Ustawi wa Jamii na Afisa Maendeleo ya Jamii wa Mkoa
wa Mtwara kuwasiliana na wadau wengine katika ngazi zote kuhakikisha
mama na mtoto wanapata huduma ya afya na ushauri na kufuatilia mwenendo
wa shauri hili.
Imetolewa na
Erasto Ching’oro
Msemaji wa Wizara
Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto
0 MAONI YAKO:
Post a Comment