Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, amesema ataanza
kuwastaafisha watumishi wa umma wasiowajibika huku akidai katika ofisi
yake ni wakuu wa idara wanne pekee ndio wanaofanya kazi vizuri kati ya
watumishi 120.
Aidha amesema kuwa daima haogopi kutumbuliwa jipu kama wengi wanavyo
muombea na kwamba yuko tayari kugombana na mtu yoyote kwa kutetea
wananchi.
Alisema tayari amewasiliana na ngazi za juu za serikali, ili kuona
uwezekano wa kuwapunguza watumishi hao ikiwa ni pamoja na kuwastaafisha
kwa manufaa ya umma.
“Watu hawawajibiki. Wanakula tu mishahara ambapo katika bajeti yetu
ya sh.bilioni 600 ni bilioni 100 tu ambazo zinaelekezwa kwenye sekta ya
maendeleo. Sh.bilioni 400 zinaishia kuwalipa mishahara na mambo
mengine, huku wananchi wakiendelea kuteseka na changamoto,”alisema
Makonda.
Alisema kuna watendaji ambao hawana ubunifu na wengi wamekuwa
wakijitetea kuwa hawana bajeti au hawajapata bajeti hizo bila kubuni
njia za kutatua changamoto za wananchi.
“Hatuwezi kwenda kwa namna hii. Tutawajibishana tu na tutatumia njia
za kuwawajibisha ikiwemo ya kuwastaafisha kwa manufaa ya umma,”alisema
Makonda.
Aliongeza “Mimi siogopi kutumbuliwa jipu na niko tayari kukosana na
kila mtu huku nikitetea wananchi wangu. Siwezi kuvumilia kuona wakuu wa
idara na watumishi wa umma wakikaa ofisini bila kuwajibika,”
Akizungumza na watumishi wa halmshauri hiyo, madiwani, wenyeviti wa
serikali za mitaa na wabunge wilayani Temeke, leo, Makonda alisema,
hayuko tayari kumvumilia mtendaji yoyote ambaye hawajibiki ipasavyo
katika kutatua kero za wananchi.
“Ninataka uwajibikaji, kuanzia serikali ya mtaa hadi idara. Kila mtu
awajibike kwa nafasi yake. Atakayeshindwa ajiondoe la sivyo
tutamstaafisha au kumpunguza. Watendaji wasiyo wajibika wajihesabie kuwa
wanabahati mbaya ya kuwa viongozi katika mkoa huu,”alisema Makonda.
Akiwasilisha ripoti ya wilaya, Mkuu wa Wilaya ya Temeke, Felix
Lyaniva, alisema wamejipanga kikamilifu hususan katika kukabiliana na
kero za wananchi, kusimamia ukusanyaji wa mapato, kumaliza changamoto ya
madawati ambapo hivi sasa wana wanashughulikia changamoto ya vyumba
vya madarasa na uhalifu.
0 MAONI YAKO:
Post a Comment