Makala: Andrew Carlos | Gazeti la Risasi Mchanganyiko, Toleo la Desemba 21, 2016
KWA miaka kadhaa sasa, maoni ya mashabiki wengi wa Muziki wa Kizazi Kipya ilikuwa ni kuingiza aina ya staili ya nyimbo za Afrika Magharibi, hususan Nigeria. Baadhi yao, wakatabiri mwanzo wa mwisho wa Bongo Fleva.
Wengi waliona Bongo Fleva ya zamani ni nzuri kuliko ya sasa. Ya sasa ikionekana nyimbo zao hazidumu, yaani nyepesi, pili ilionekana wanaigana mawazo ya bits, mashairi na wakati mwingine muingiliano wa video.
Diamond Platinumz, anayechukuliwa kuwa ndiye msanii mwenye mafanikio zaidi katika Bongo Fleva, hivi karibuni aliurudia wimbo wa mkongwe wa nyimbo za asili nchini, Saida Karoli anayeonekana kupotea kwenye ramani kidizaini.
Katika wimbo huo uitwao Salome, Diamond aliweka vibwagizo vya kiasili lakini vinavyoweza kuchezeka kisasa. Baada ya kibao hicho, maelfu ya mashabiki wa Bongo Fleva wameonekana kuupenda sana wimbo huo, kitu kilichowafanya wasanii wengine nao, wazitafute nyimbo za Saida Karoli na kudumbukiza vionjo hivyo.
Makala haya yanachambua baadhi ya ngoma za Bongo Fleva ambazo zimechanganywa mahadhi ya kiasili pamoja na baadhi ya mashairi yanayotokana na nyimbo za Saida;
Salome (Diamond ft Ravanny)
Septemba mwaka huu, mkali wa Bongo Fleva, Diamond Platnumz aliitoa ngoma hii kwa mara ya kwanza. Ni kama alifanya ‘kava’ kutokana na asilimia kubwa ya biti pamoja na melodi kutoka katika Ngoma ya Chambua Kama Karanga (Maria Salome).
Diamond mwenyewe alikiri kuwa, ngoma hiyo ameitoa kama kuuenzi muziki wa asili na pia kumuenzi mtunzi na mwimbaji wa ngoma hiyo, Saida Karoli.
Baadhi ya mistari inayotokana na ngoma hiyo ni;
“Hoera makulu vane, hoera ngambe
Hoera na Zari, hoera ngambe
Chambua kama karanga sasa
Chambua kama karanga
Ichambue kama karanga Salome
Chambua kama karanga.”
Tangu aachie video hiyo, katika Mtandao wa Youtube imefikisha watazamaji zaidi ya milioni 10.
Muziki ya Darassa
Katika ngoma hii ambayo ni kama wimbo wa taifa kwa sasa kutokana kukubalika kwa kila rika ndani na nje ya nchi, ukisikiliza mdundo wake ulivyo wa kuchezeka ni wazi umechanganywa na mahadhi ya nyimbo za asili.
Licha ya Darassa kutumia baadhi ya maneno yaliopo katika Ngoma ya Maria Salome kama Chambua Kama Karanga, hivi karibuni nilikuwa na Saida na nikamhoji kuhusiana na ngoma hiyo, ambapo moja kwa moja alisema, biti iliyotumika na baadhi ya vionjo vinapatikana katika wimbo wake wa Kitobero aliomshirikisha Benjamini.
Kwa sasa ngoma hiyo imetazamwa zaidi ya mara milioni 1.9 katika Mtandao wa Youtube.
Give It To Me ya Belle 9
Kama ilivyo kwa Darassa na Diamond, Belle naye ameachia Ngoma ya Give It To Me ambayo ni ya kuchezeka. Kikubwa ndani ya ngoma hii ni bit iliyokuwa na vionjo vya nyimbo za asili.
Pia katika ngoma hii, Belle ametumia upepo wa Saida katika kutengeneza kibwagizo kilichofanana na kwenye Ngoma ya Maria Salome ambapo amesikika akiimba;
“Iyooo yo yo yo
iyooo yo yo yo.”
Ndani ya siku mbili tu, ngoma hiyo imefikisha watazamaji zaidi ya laki moja.
Maneno ya Saida
Licha ya wasanii hao kuendelea kutumia biti, vionjo na baadhi ya mashairi kutoka katika nyimbo zake, mwenyewe anasema;
“Kwanza niwapongeze, sijawahi hata siku moja kumshtaki msanii eti naibiwa kazi na haitatokea. Wanavyofanya nafurahi na waendelee zaidi kwa maana wanaonyesha heshima katika muziki wetu katika kuufikisha levo za kimataifa,” alisema Saida.
0 MAONI YAKO:
Post a Comment