Chama cha Wananchi (CUF), kimesema taarifa zinazosambazwa katika vyombo vya habari na mitandao ya kijamii, kwamba Katibu Mkuu, Maalim Seif Sharif Hamad anataka kuhama chama hicho ni za kupuuzwa kwa kuwa hazina ukweli.
Naibu Katibu Mkuu wa CUF Zanzibar, Nassor Ahmed Mazrui alisema hayo jana baada ya baadhi ya vyombo vya habari kuripoti kuwa Maalim anataka kuondoka ndani ya chama hicho cha upinzani.
Alisema tangu kuibuka kwa mgogoro ndani ya CUF na Mwenyekiti wao, Profesa Ibrahim Lipumba imekuwapo mikakati ya kuwakatisha tamaa jambo ambalo halitafanikiwa.
Mazrui alisema wanaopanga mikakati wamehangaika kila njia na wameonekana kukwama, hivyo kuibuka na mkakati wa kumzushia Katibu Mkuu kuhama chama.
“Hivi unafikiria Katibu Mkuu anaweza kuhama chama katika mazingira rahisi kiasi hicho? Hiki chama amekipigania vya kutosha wataondoka wao,” alisema.
Naibu Katibu Mkuu huyo aliwataka wana CUF kuendelea kutoa ushirikiano kwa Katibu Mkuu wao na kupuuza kauli za watu ambao wamepoteza mwelekeo kisiasa.
Alisema CUF si chama kinachotegemea mtu mmoja, na pia hakiko tayari kumpoteza Maalim kwa vibwagizo vya vibaraka wa chama tawala, ambao hawataki kupigania mabadiliko nchini.
Aidha, kuhusu chama kuwa kimya kuhusu madai yao ya ushindi katika uchaguzi wa Oktoba 25 mwaka jana, alisema bado wanaendelea na mchakato huo na watatoa taarifa hivi karibuni kuhusu hatua waliyofikia.
Mazrui alisema kila kitu kinakwenda vizuri na kutaka wana CUF kuwa na subira katika kipindi hiki, kwani mambo mazuri hayahitaji haraka.
Alisema ushirikiano wanaopata kutoka jumuiya ya kimataifa ni mzuri hali ambayo inawapa matumaini ya kuhakikisha kuwa haki inapatikana.
“Suala la madai ya ushindi wa uchaguzi linakwenda vizuri, na naamini hatima yake itapatikana kwa busara, ni vema wana CUF kuwa na subira,” alisema.
Jana katika baadhi ya magazeti ziliandikwa habari zikimhusisha Maalim na kuhama CUF na kutajwa kutarajia kuhamia vyama vya ADA-TADEA, AFP au ACT-Wazalendo, ambapo viongozi wa vyama hivyo walikanusha taarifa hizo.
Hali kadhalika Katibu Mkuu huyo alihusishwa na kutaka kujiunga na vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).
0 MAONI YAKO:
Post a Comment