Naibu
Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi Vijana na Ajira ambaye pia ni Mbunge wa
Jimbo la Dodoma Anthony Mavunde (wa pili kushoto) akizungumza katika
mkutano na Wafanyabiashara wa eneo la Jamatini Manispaa ya Dodoma baada
ya Vibanda vyao kubomolewa Kampuni Hodhi ya Rasilimali za Reli (RAHCO)
kupisha mradi wa ujenzi wa Reli kisasa. Kulia ni Naibu Meya wa Manispaa
ya Dodoma Jumanne Ngede na wa pili kulia ni Mkurugenzi wa Halmashauri
hiyo Godwin Kunambi. Kushoto ni Katibu wa Wafanyabiashara hao John
Banda.
Mkurugenzi
wa Halmashauri ya Manispaa ya Dodoma Godwin Kunambi (wa pili kushoto)
akiteta jambo na wafanyabiashara wakati akitoka katika eneo la Stendi ya
Jamatini Mjini Dodoma baada ya kuzungumza na wafanyabiashara
waliovunjiwa vibanda vyao kupisha mradi wa ujenzi wa Reli ya Kisasa.
Baadhi
ya wafanyabiashara wa eneo la Jamatini Manispaa ya Dodoma wakifuatilia
mkutano wao na Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi Vijana na Ajira
ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Dodoma Anthony Mavunde, Naibu Meya wa
Manispaa ya Dodoma Jumanne Ngede na Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo
Godwin Kunambi. PICHA NA RAMADHANI JUMA-OFISI YA MKURUGENZI
………..
NA RAMADHANI JUMA.OFISI YA MKURUGENZI
MANISPAA YA DODOMA
HALMASHAURI
ya Manispaa ya Dodoma inatarajia kuwapatia eneo wafanyabiashara zaidi
ya 550 waliovunjiwa vibanda vyao na kampuni hodhi ya Rasilimali za Reli
(RAHCO) katika stendi ya mabasi madogo ya Jamatini ili kupisha
utekelezaji wa mradi wa Reli ya kisasa, ili waendelee kufanya biashara
zao kama kawaida.
Mkurugenzi
wa Halmashauri ya Manispaa ya Dodoma Godwin Kunambi amewaeleza
wafanyabiashara hao kuwa, Manispaa iko katika hatua za mwisho kuandaa
eneo la Makole D-Center kwa kuweka miundombinu muhimu ikiwemo mfumo wa
maji safi na maji taka ili wafanyabiashara hao waanze kufanya shughuli
zao mara moja na katika mazingira rafiki na salama katika eneo hilo.
Aliyasema
hayo alipotembelea eneo la Jamatini na Stendi Kuu Novemba 6 mwaka huu,
akiambatana na Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi Vijana na Ajira
Anthony Mavunde ambaye ni Mbunge wa Jimbo la Dodoma, pamoja na Naibu
Meya wa Halmashauri ya Manispaa hiyo Jumanne Ngede kwa lengo la kuwapa
pole wafanyabiashara hao na kuwajulisha hatua zilizochukuliwa na
Viongozi mbalimbali katika kuhakikisha tatizo linalowakabili linapatiwa
ufumbuzi kwa wakati.
Aliwatoa
hofu ya kuwa eneo hilo halitakuwa na wateja wengi kama ilivyokuwa eneo
la stendi ya Jamatini, ambapo aliwaambia tayari Mkuu wa Mkoa wa Dodoma
Daktari Binilith Mahenge ametoa maelekezo kwa Manispaa na Sumatra
kuhakikisha daladala zinakuwa na ruti inayopita katika eneo hilo jipya
la biashara ambapo abiria watakuwa na kituo cha kupanda na kushuka na
hivyo kuongeza mzunguko wa wateja katika eneo hilo, na kwamba
utekelezaji wa maelekezo hayo umeshaanza kufanyiwa kazi na Sumatra.
Akizungumza
na wafanyabiashara ya usafiri wa mabasi katika Stendi Kuu ya mabasi ya
mikoani, Mkurugenzi Kunambi aliwaambia kuwa, Manispaa kwa kushauriana na
uongozi wa Mkoa na wadau kama Sumatra imepanga kuhamishia Stendi hiyo
katika eneo la Chaduru au kwenye eneo la viwanja vya Nanenane vilivyopo
Kata ya Nzuguni barabara kuu ya Dodoma-Dar es Salaam.
Alisema
Manispaa itazungumza na uongozi wa wasafirishaji ili kupata mapendekezo
yao juu ya eneo rafiki zaidi miongoni mwa maeneo hayo mawili.
Kwa
upande wake, Naibu Waziri Mavunde aliwataka wote walioathiriwa na zoezi
hilo la bomoabomoa wawe watulivu katika kipindi hiki kigumu wakati
Mamlaka na Viongozi wakifanya juhudi za makusudi kuwatafutia maeneo
rafiki kwa shughuli zao huku Naibu Meya Ngede akiwahakikishia kuwa
Baraza la Madiwani litasimamia kikamilifu suala la upatikaaji wa maeneo
hayo.
0 MAONI YAKO:
Post a Comment