Rais mteule wa Liberia George Weah.
Meneja wa Arsenal Arsene Wenger
ameambia BBC kwamba amepokea mwaliko kutoka kwa rais mteule wa Liberia
George Weah kuhudhuria sherehe ya kuapishwa kwake baadaye mwezi huu.
Wenger amesema: “Nimealikwa na George kwa siku hiyo ambapo ataapishwa kuwa Rais.”Meneja huyo wa Arsenal alikuwa meneja wa Weah katika klabu ya Monaco inayocheza Ligi Kuu ya Ufaransa miaka ya 1990 na amesema hakuwahi kufikiria kwamba wakati mmoja mchezaji huyo angekuwa rais.
“Maisha ya jamaa huyu kwa kweli ni kama filamu. Ni ya kushangaza. Yanaweza kuunda filamu nzuri sana,” amesema Wenger.
Meneja wa Arsenal Arsene Wenger.
Wenger amesema Weah kwa muda mrefu amekuwa anaipenda sana nchi yake na ana ukakamavu ambao umemfanya kuamini kwamba alikuwa na ndoto fulani maishani.
“Nilisafiri na George wakati huo kulipokuwa na vita nchini Liberia na nimeona jinsi alivyotatizika kutokana na taifa lake na hilo lilikuwa jambo moja ambalo lilikuwa linaendelea kwa muda taifa lake, upendo wake kwa taifa hilo na watu wake,” amesema Wenger.
“Leo hii nikitazama nyuma na kumuona akitokwa na machozi vita vilipokuwa vimechacha Liberia ni jambo la kufurahisha sana na natumai atakuwa rais wa furaha na ningependa kuona bwana huyu akiwa mfano mzuri kwa wachezaji wote wa soka wa sasa.”
Wenger amesema kwamba hataweza kusafiri Liberia kuhudhuria sherehe hiyo ya kuapishwa kwa Weah kutokana na shughuli nyingi Ligi ya Premia.
“Ninaamini nitakuwa na shughuli nyingi lakini iwapo nitapigwa marufuku basi nitapata muda wa kwenda,” Wenger, ambaye amefunguliwa mashtaka ya utovu wa nidhamu na Chama cha Soka England amesema.
0 MAONI YAKO:
Post a Comment