Msemaji wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ameeleza kuwa, ugaidi
haufungamani na dini au madhehebu fulani na kusisitiza kwamba viongozi
wote wa dini ulimwenguni wanalaani na wanapinga kwa nguvu zao zote
vitendo vya kigaidi na vya kufurutu mipaka. Farhan Haq, Msemaji wa Ban
Ki moon ameelezea nafasi ya viongozi wa kidini katika kuzuia kusambaa na
kuongezeka makundi yenye misimamo ya kufurutu mipaka na ya kigaidi
yanayojinasibisha na dini ya Kiislamu na kusisitiza kwamba, ugaidi kamwe
haufungamani na dini maalumu na kwamba wafuasi wa makundi yenye
kufurutu mipaka kutoka dini yoyote ile wanaweza kutekeleza vitendo vya
kigaidi. Farhan Haq amebainisha kuwa, walimwengu wanapaswa kuelewa
kwamba vitendo vya kigaidi vinavyofanywa na baadhi ya wafuasi wa dini
fulani, havimaanisihi kwamba dini hiyo inahubiri na kuwashajiisha
wafuasi wake kutekeleza vitendo hivyo visivyo vya kibinadamu. Msemaji wa
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amesema kuwa, hadi sasa umoja huo
umefanya mazungumzo na viongozi wengi wa kidini duniani na kusisitiza
kwamba viongozi hao wote wamelaani vikali ugaidi unaofanywa kwa namna
yoyote ile. Farhan Haq ameeleza kwamba, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa
daima amekuwa akiwataka wafuasi wa dini mbalimbali kuwavumilia wafuasi
wa dini nyingine ili kupatikane amani na utulivu duniani.
0 MAONI YAKO:
Post a Comment