
Wizara ya Mambo ya Nje ya Kenya imetangaza kuwa, zoezi la kurejeshwa
nyumbani raia wa nchi hiyo kutoka Yemen, litaendelea. Kwa mujibu wa
wizara hiyo, hadi sasa serikali ya Nairobi imeshawarejesha nyumbani
makumi ya raia wake kutoka Yemen, kutokana na kushadidi mashambulizi ya
Saudia nchini humo. Imesema kuwa, hatua hiyo imekuja kufuatia ombi la
Wakenya waishio nchini Yemen kuitaka serikali yao kusaidia kuwatoa
nchini humo ili kuokoa maisha yao kutokana na mashambulizi mtawalia ya
ndege za kijeshi za Saudi Arabia na waitifaki wake zikiwemo Marekani na
Israel. Hii ni katika hali ambayo siku ya Alkhamisi Wizara ya Mambo ya
Nje ya Misri ilitangaza kuondolewa raia wake 1,150 nchini Yemen kutokana
na usalama kuwa mdogo nchini humo. China ni nchi nyengine ambayo
imeondoa wanadiplomasia wake nchini Yemen. Hadi sasa karibu watu 1000
wamekwishauawa tangu Saudia ilipoanzisha mashambulizi yake ya kichokozi
tarehe 26 Machi mwaka huu dhidi ya wananchi wa nchi hiyo jirani ya
Kiarabu. Wakati huo huo, malaki ya Wayemen jana walimiminika
mabarabarani mjini Sana'a na mikoa mingine ya nchi hiyo kulaani jinai za
Saudia katika kuwaua raia wasio na hatia na kubomoa miundombinu
sambamba na kutangaza kuiunga mkono Harakati ya Answarullah iliyosimama
kidete kuwakomboa wananchi wa Yemen.
0 MAONI YAKO:
Post a Comment