Mahakama ya kikatiba nchini Madagascar imefutilia mbali uamuzi wa bunge kumfuta kazi rais Hery Rajaonarimampianina.
Mahakama hiyo ilitamka kwa kinywa kipana kuwa hakukuwa na ushahidi wowote kuwa Rais
Rajaonarimampianina alikuwa ''amekaribia hata kwa nia tu'' kukiuka sheria zozote za Madagascar.
Wanasiasa wanaompinga wametaja uamuzi huo wa mahakama kuwa wa kutamausha.
Bwana Rajaonarimampianina
alikwenda mahakamani kupinga kufurushwa kwake kutoka madarakani akisema
kuwa asilimia kubwa ya wabunge wanaodaiwa kupiga kura hiyo iliyomuondoa
madarakani hawakuwa bungeni wakati wa kura hiyo.
Rajaonarimampianina anadaiwa kuhujumu uchumi wa taifa hilo na pia
kushindwa kutekeleza ahadi alizowapa wapiga kura wakati wa kampeini za
uchaguzi mkuu.
Rajaonarimampianina alikuwa ameliongoza kisiwa
hicho kwa kipindi cha miezi 16 pekee na alikuwa anatazamiwa kuleta
utulivu katika taifa hilo lililokuwa katika hatari ya kurejea katika
misukosuko ya kisiasa na unga'nga'niaji madaraka kati ya vyama vya
kisiasa na viongozi wao.
Mwakilishi wa chama cha rais
huyo cha HVM , Rivo Rakotovao, ameunga mkono uamuzi huo wa mapema leo
huku msemaji wa chama cha upinzani Pierre Houleder akiutaja kuwa wa
''kushangaza mno.''
Wandani wa maswala ya Madagascar wanasema kuwa
rais Rajaonarimampianina anapigwa vita baridi na kiongozi wa zamani
Andry Rajoelina na pia rais mwengine wa zamani Marc Ravalomanana.
Viongozi
hao japo maarufu walilazimishwa na wahisani wa kimataifa kutoshiriki
uchaguzi wa pamoja wa urais uliofanyika mwaka wa 2013 kama sehemu ya
makubaliano ya kuleta suluhu ya mgogoro wa kisiasa uliotokana na
aliyekuwa rais wa taifa hilo bwana Rajoelina kumn'goa madarakani rais
wakati huo (2009)bwana Ravalomanana.
0 MAONI YAKO:
Post a Comment