
Alfonce Mawazo enzi za Uhai wake
Viongozi wa Kitaifa wa Vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi
(Ukawa), leo wamewaongoza mamia ya wakazi wa mkoa wa Mwanza kutoa
heshima za mwisho, za kuuaga mwili wa aliyekuwa Mwenyekiti wa Chama cha
Demokrasia na Maendeleo (Chadema) mkoa wa Geita Marehemu Alphonce
Mawazo.
Katika shughuli hiyo baba mdogo wa Marehemu Alphonce Mawazo, Charles
Lugiko na mtoto mkubwa wa Marehemu Prescious Mawazo wakatoa ujumbe
mzito, huku mwanaye anayesoma darasa la nne akiahidi kuwa siku moja
atarithi mikoba ya baba yake katika ulingo wa Siasa.

Aliyekuwa Mgombea Urais wa CHADEMA na kupeperusha bendera ya UKAWA, Mhe. Edward Lowassa akitoa salamu zake za mwisho kwa aliyekuwa M/kiti CHADEMA moa wa Geita Alphonce Mawazo aliyeuwawa kikatili kwa kukatwakatwa mapanga
Safari ya kuusindikiza Mwili wa Marehemu Alphonce Mawazo, imeanzia hapa
katika Hospitali ya Rufaa ya Bugando Jijini Mwanza, ambapo mwili wake
ulihifadhiwa kwa kipindi cha siku takribani kumi na nne, tangu mahuti
hayo yalipomkuta Novemba 14 mwaka huu.
Kituo cha kwanza cha safari hii kikawa nyumbani kwa baba yake mdogo
kata ya Luchelele Nyegezi eneo la Sweya, ambapo taratibu mbalimbali za
kifamilia zimefanyika, kabla ya kuanza safari ya kuupeleka mwili wake
katika viwanja vya Furahisha kwa ajili ya kuagwa.

Mwenyekiti CHADEMA Taifa, Freeman Mbowe akitoa salamu za mwisho kwa aliyekuwa Mwenyekiti wa Mkoa wa Geita kamanda Alphonce Mawazo ambaye ameagwa kitaifa katika Viwanja vya Furahisha jijini Mwanza
Taratibu hizo zilipokamilika safari ya kuelekea katika viwanja vya
Furahisha Jijini Mwanza ikawadia, ambapo katika viwanja hivyo viongozi
wa Kitaifa wa (Chadema) wakaungana na mamia ya wakazi wa mkoa wa Mwanza
kutoa heshima za mwisho.
Baada ya shughuli hiyo wafuasi wa Chama hicho wakaungana katika safari
ya kuusindikiza mwili wa Marehemu Alphonce Mawazo, hadi mkoani Geita
ambako utahifadhiwa katika Hospitali ya wilaya hiyo, kwa ajili ya kuagwa
siku ya Jumapili katika viwanja vya Magereza.
Shughuli hiyo itakapokamilika Mwili wake utapelekwa katika mji mdogo wa
katoro, ambako aligombea Ubunge wa Jimbo hilo kwa ajili ya kuagwa,
kabla ya safari ya kuelekea Kijijini kwao kata ya Chikobe, ambako
mazishi yatafanyika siku ya Jumatatu majira ya saa nne asubuhi.

Familia ya Marehemu Alphonce Mawazo wakiendeshwa na mchungaji kwa ibaa fupi iliyofanyika nyumbani kwa baba Mdogo wa Marehemu.

Mwili wa marehemu Alphonce Mawazo ikiwasili nyumbani kwa baba mdogo (Charles Lugiko) Nyegezi jijini Mwanza ukitokea Hospital ya Bungando kwaajili ya ibada fupi


0 MAONI YAKO:
Post a Comment