Katika siku za hivi karibuni kumekuwa
na taarifa za kuwepo kwa Programu (Application) ya simu ikijulikana kama
SOFTBOX TANZANIA iliyosemekana iko kwenye Google PLAYSTORE.
Ilidaiwa kuwa program (Application)
hiyo ya SOFTBOX TANZANIA ilikuwa na uwezo wa kunasa au kuingilia
mazungumzo ya simu, ujumbe mfupi pamoja na mawasiliano ya WhatsApp
kutoka kwenye simu ya mtu binafsi.
Kwa yeyote aliyekuwa na nia hiyo ya
kunasa au kuingilia mazungumzo ya simu, ujumbe mfupi pamoja na
mawasiliano ya WhatsApp kutoka kwenye simu ya mtu mwingine alihitajika
kulipia fedha kiasi cha Tshs 35,000/= kupitia mitandao ya simu ili
kupata namba ya siri kwa ajili ya kuwezesha nia hiyo.
Mamlaka ya Mawasiliano imefanya
uchunguzi kubaini kuwepo kwa programu hiyo na ukweli kuhusu uwezo wake
wa kufanya kilichodaiwa, ikiwa ni pamoja na kuangalia madhara ya program
hiyo na sheria inasema nini kuhusu suala hili.
Baada ya kufanya uchunguzi wa kina,
Mamlaka ya Mawasiliano ilibaini na imejiridhisha kuwa program
(Application) hiyo haina uwezo huo wa kunasa au kuingilia mazungumzo ya
simu, ujumbe mfupi pamoja na mawasiliano ya WhatsApp kutoka kwenye simu
ya mtu binafsi kama ilivyodaiwa.
Aidha Mamlaka imebaini kuwa
watengenezaji (Developers) wa programu hiyo walikuwa na nia ya kutapeli
na kujipatia fedha hiyo kiasi cha Tshs 35,000/= kwa njia ya udanganyifu
wakitumia kivutio cha kunasa au kuingilia mazungumzo ya simu, ujumbe
mfupi pamoja na mawasiliano ya WhatsApp kutoka kwenye simu za watu
binafsi.
Programu (Application) nyingine ya aina hiyo iliibuka tena ikiitwa SIMNET Tanzania ikiwa na maelezo kama ya awali.
Wakati Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania
pamoja na Jeshi la Polisi wakiendelea na uchunguzi zaidi, tunapenda
kuuarifu umma wa Watanzania kuepuka kufanya mambo yafuatayo:
1. Kuvutiwa na matendo yaliyo kinyume
na sheria na maadili ya matumizi mazuri ya mawasiliano kama hili la
kunasa au kuingilia mazungumzo ya simu, ujumbe mfupi pamoja na
mawasiliano ya WhatsApp kutoka kwenye simu ya mtu binafsi.
Kitendo hiki ni kosa la jinai kwa
mujibu wa kifungu cha 6 na 10 cha Sheria ya Makosa ya Mtandao ya Mwaka
2015 na kifungu cha 123 cha Sheria ya Mawasiliano ya Kielektroniki na
Posta (EPOCA) ya Mwaka 2010.
Sheria katika vifungu hivyo inakataza
mtu yeyote kuingilia mawasiliano ya mtu mwingine. Adhabu kali ya makosa
haya ni faini isiyopungua shilingi milioni tano au kutumikia kifungo kwa
kipindi kisichopungua mwaka mmoja au vyote kwa pamoja.
2. Mamlaka inawatahadharisha watumiaji
wa huduma za mawasiliano kutokuwa wepesi na kudanganyika kufanya malipo
yoyote kwa njia ya mitandao kwa huduma wasiyokuwa na uhakika nayo au
bila kujiridhisha na uwepo wa huduma hiyo.
Ni vizuri kutoa taarifa kwa mtoa huduma wako au kuwasiliana na Mamlaka ya Mawasiliano kupitia barua pepe malalamiko@tcra.go.tz au kupiga simu namba 0784558270/1.
Imetolewa na:
Mkurugenzi Mkuu
Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania
04/12/2015.
0 MAONI YAKO:
Post a Comment