JINA la aliyekuwa mgombea urais kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Edward Lowassa, limeibuka ndani ya vikao vya wabunge wa CCM vilivyofanyika mjini Dodoma kati ya juzi na jana, Raia Mwema linaweza kuripoti.
Lowassa ambaye pia alikuwa akiungwa mkono na vyama vilivyomo ndani ya Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), alihama CCM mwezi Agosti mwaka jana lakini anaonekana bado anazua mjadala ndani ya chama hicho.
Wakati wa Mkutano huo wa wabunge wa CCM, baadhi ya wabunge wanaofahamika kama maswahiba wa Lowassa, walilazimika kujitetea mbele ya wenzao na kueleza kuwa hawana uhusiano tena na kiongozi huyo na kwamba wao si wasaliti.
Mmoja wa wabunge hao, Peter Serukamba, ambaye ni Mbunge wa Jimbo la Kigoma Kaskazini (CCM), alisema uhusiano wake na Lowassa ulimalizika siku ambayo kiongozi huyo alihamia Chadema.
Haya mambo kwamba kuna wasaliti humu ndani ya chama chetu yanatakiwa kupuuzwa. Kila mtu aliingia kwenye chama kwa siku yake na ni lazima awe na watu au kundi alilokuwa nalo karibu.
“Ukiniuliza mimi, nitakwambia kwamba wakati wa mchakato wa kuwania urais kupitia CCM, zilikuwapo kambi nyingi. Kwa mfano, ilikuwapo kambi ya waziri mkuu, Mizengo Pinda, ilikuwapo kambi ya aliyekuwa waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe na ilikuwepo ya Lowassa.
“Cha ajabu ni kwamba, watu waliokuwa kambi za Pinda, Membe na wengine hawaonekani kuwa ni tatizo lakini sisi tuliokuwa kwenye kambi ya Lowassa inaonekana tuna matatizo. Hii si sahihi hata kidogo,” alisema Serukamba kwa hisia kali.
Akitoa mifano na maelezo mengine, Serukamba alisema katika Jimbo lake la uchaguzi, aliyekuwa mgombea urais wa CCM, John Magufuli, alipata kura nyingi kuliko Lowassa, dalili kwamba yeye alifanya kampeni zake kwa mgombea wa chama chake.
Alisema pia kwamba katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010, CCM ilipoteza jumla ya kata tano ambazo imefanikiwa kuzirejesha katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana.
Kauli hiyo ya Serukamba iliungwa mkono na Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake wa CCM, Sofia Simba, aliyesema kama wangekuwa bado ni watu wa Lowassa, wangehama naye wakati alipoondoka na kuhamia Chadema.
Taarifa kutoka ndani ya kikao hicho kilichofanyika katika Ukumbi wa Pius Msekwa kwenye eneo la Bunge mjini Dodoma, zinaeleza kuwa Sofia ambaye kwa muda mrefu amekuwa mtetezi wa Lowassa kwenye vikao vya chama hicho alieleza namna alivyojitahidi kumshawishi Lowassa asihame bila mafanikio.
“ Mimi mnavyoniona, nilifanya kazi kubwa sana ya kujaribu kumshawishi Lowassa asihame CCM kwenda Chadema. Niliifanya kazi hiyo kwa mapenzi yangu kwa chama. Iliposhindikana, sikuhama. Nimebaki humu hadi leo,” alisema Sofia.
Kwa zaidi ya miaka minane sasa, Sofia amefahamika kama mmoja wa watetezi wakuu wa Lowassa ndani ya CCM; na matukio mawili katika suala hilo yalimpambanua zaidi.
Mosi ni tukio la yeye, na wajumbe wawili wa Kamati Kuu ya CCM; Dk. Emmanuel Nchimbi na Adam Kimbisa, kuzungumza na waandishi wa habari kupinga maamuzi yaliyofanyika ya kukata jina la Lowassa miongoni mwa wagombea urais.
Tukio jingine lilitokea takribani miaka mitano iliyopita, wakati bado suala la kashfa ya Richmond likiwa la moto, ambapo Simba alizungumza ndani ya vikao vya chama hicho kuwa “Hakuna Mwanamume kama Lowassa” ndani ya chama hicho.
Kwa upande wake, Mbunge wa Busega, Dk. Raphael Chegeni, ambaye naye alikuwa akifahamika kama mwana mtandao wa Lowassa , alizungumza kwenye mkutano huo kwa hisia pia na kueleza kuwa yaliyopita si ndwele.
Alisema yeye ni muumini wa dini ya Kikristo anayeamini kwenye suala la kuzaliwa kwa mara ya pili.
“Mimi ni muumini wa dini ya Kikristo. Kwenye dini yetu, sasa sina hakika sana kwa wenzetu Waislamu kwao hali ikoje, tunasema mtu akizaliwa mara ya pili mambo yote ya nyuma yanafutika. Mimi nadhani haya mambo na hizi dhana ziishe na tusonge mbele,” alisema Chegeni.
Kinana aongoza kikao
Mkutano huo wa wabunge uliongozwa na Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana, kutokana na kutokuwapo kwa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, ambaye kwa mujibu wa taratibu za chama hicho, ndiye huwa mwenyekiti wa vikao rasmi vya wabunge wa chama hicho.
Mbali ya Kinana, Mkutano huo ulihudhuriwa pia na Makamu Mwenyekiti wa CCM, Philip Mangula, na mmoja wa watoa mada alikuwa ni Makamu Mwenyekiti mstaafu wa chama hicho, Pius Msekwa, ambaye amewahi pia kuwa Spika wa Bunge.
Hoja za akina Serukamba zinaonekana kuchagizwa na hotuba ya ufunguzi wa mkutano huo iliyotolewa na Mangula, ambaye alizungumzia changamoto mbalimbali zilizojitokeza ndani ya CCM wakati wa Uchaguzi Mkuu.
Kwa mara ya kwanza tangu kumalizika kwa uchaguzi huo, Mangula alisema yeye hana tatizo na wana CCM walioamua kuhama chama hicho na kujiunga na vile vya Upinzani kwa sababu ya kutoridhishwa na uamuzi wa kukata wagombea au kutotendewa haki.
“ Mimi nawapongeza wana CCM waliohama chama wakati wa uchaguzi kwa sababu ya kutoridhika na maamuzi yetu au kuona kwamba hawakutendewa haki ndani ya chama. Hawa waliona kuwa kama wangebaki, wangetuumiza.
“ Tatizo tulilokuwa nalo wakati wa uchaguzi ni kuhusu wana CCM ambao hawakuhama lakini wakabaki na kuamua kutufanyia hujuma za ndani kwa ndani. Hawa kwa kweli walituumiza,” alisema Mangula.
Mmoja wa wabunge waliohudhuria mkutano huo alisema ni jambo la heri kwamba Mangula alizungumza mambo hayo kwenye kikao hicho cha wabunge kwa vile kimetoa fursa ya watu kutoa ya moyoni.
“ Unajua hali haikuwa nzuri sana na wabunge tunakwenda kwenye Bunge gumu na litakalokuwa na upinzani mkali. Sasa kama sisi wenyewe ndani ya CCM hatujasafisha mioyo yetu, hatuwezi kuwa wamoja bungeni. Hivyo Mangula katusaidia sana,” alisema mmoja wa wabunge maarufu wa CCM kutoka mikoa ya Kanda ya Ziwa aliyezungumza na gazeti hili kwa masharti ya kutotajwa majina
Source:RAIA Mwema
0 MAONI YAKO:
Post a Comment