Naibu Katibu Mkuu wa CUF Bara, Magdalane Sakaya
Chama cha Wananchi (CUF), kimesema kinajiandaa kutoa tamko zito kuhusu hatima yake kisiasa visiwani Zanzibar.
Kufuatia hatua ya Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zaniabar (ZEC),
Jecha Salum Jecha kufuta Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25, mwaka jana, ambao
chama hicho kinaamini kuwa kilishinda, CUF iligomea uchaguzi wa marudio
wa Jumapili iliyopita.
Tangu hapo, Rais Dk. Ali Mohammed Shein alishaapishwa Alhamisi iliyopita kuongoza visiwa hivyo mpaka mwaka 2020.
CUF inaamini matokeo ya uchaguzi wa mwaka jana yangeonyesha kuwa mgombea wao, Maalim Seif Hamad, ameshinda kwa kishindo.
Aidha, Chama hicho kimesema hakitababaishwa na hatua ya serikali
kumwondolea walinzi Maalim Seif kwasababu chama hicho kina walinzi wa
kutosha kufanya kazi hiyo .
Akizungumza na Nipashe jana, Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho Bara,
Magdalane Sakaya, alisema CUF inafanya maandalizi ya vikao vya ngazi za
juu ambavyo ndivyo vitakavyotoa maamuzi kuhusu mustakabali wa kisiasa
visiwani humo, baada ya uchaguzi wa marudio.
Sakaya ambaye ni Mbunge wa Jimbo la Kaliua mkoani Tabora kwa tiketi ya
CUF, alisema ingawa shughuli za chama zinaendelea kama kawaida, vikao
hivyo ambavyo ni Kamati Tendaji na Baraza Kuu vitakaa ndani ya muda
mfupi ujao na vitajadili na kutoa msimamo wa chama kuhusu hatma ya
Zanzibar.
“Tunaendelea na maandalizi ya vikao hivyo na wiki ijayo vitakaa na kutoa
mwelekeo wa nini kinaendelea na nini msimamo wa chama kuhusu siasa za
Zanzibar, lakini tunaendelea kuamini kuwa mgombea wetu ndiye chaguo
sahihi la Wazanzibari katika uchaguzi wa Oktoba 25 mwaka jana,” alisema
Sakaya.
Aidha, Sakaya alisema CCM ilishapanga siku nyingi za kuhakikisha
wanashinda kwa hila kwenye uchaguzi huo ili wabadili Katiba ya Zanzibar
inayozungumzia Serikali ya Umoja wa Kitaifa na hatimaye waunde serikali
peke yao ambayo haitakuwa na vyama vya upinzani.
Kuhusu taarifa za Maalim Seif kupunguziwa walinzi, Sakaya alisema CUF
haiwezi kubababishwa na hilo kwasababu chama chao kina walinzi wa
kutosha ambao watamlinda wakati wote na aliongeza kuwa hatua ya CCM
kulazimisha kumwapisha Dk. Shein ni udikteta wa kupindukia.
Alielezea kushangazwa na idadi kubwa ya askari polisi na wa JWTZ wakati
wa uchaguzi wa marudio, hali ambayo iliwatisha wananchi na wengine
kuogopa kwenda kwenye shughuli zao za kila siku.
“Baadhi ya wanachama wa CUF bado wako mahabusu hadi leo na wanasheria
wetu wanaendelea na mchakato wa kuwatoa maana hawana kesi," alisema
Sakaya.
"Wengi walipigwa na kuteswa na kubambikiwa kesi kwasababu za kisiasa na
kwa kuwa wameshatimiza kile walichokuwa wanakitaka tunaamini
watawaachia.”
Mwenyekiti wa ZEC Jecha alimtangaza Dk. Ali Mohammed Shein kuwa Rais wa
Zanzibar Jumatatu kwa kupata asilimia 91.4 ya kura halali.
Kwa mujibu wa Jecha, Shein alipata kura 299,982 kati ya jumla ya wapiga
kura waliojitokeza 341, 865. Jumla ya Wazanzibari wlaiojiandikisha
walikuwa kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25, mwaka jana ambao
ulifuntwa na Jecha walikuwa 503,580.
Nafasi ya pili ilichukuliwa na mgombea urais wa ADC, Hamad Rashid
aliyepata kura 6,734 na Maalim Seif Sharif Hamad (CUF) alishika nafasi
ya tatu kwa kupata kura 6,076.
Ushindi wa Dk. Shein wa asilimia 91.4 una maana vyama vingine saba
vilivyoshiriki vilikosa asimilia 10, ambazo kisheria zingeliweza
kukifanya kuingia kwenye serikali ya umoja wa kitaifa.
Jecha aliufuta uchaguzi wa Oktoba 25 kwa madai ya kuwepo kasoro kubwa,
hatua ambayo ilipingwa vikali na CUF, ambacho aliyekuwa mgombea wake wa
urais, Maalim Seif Sharif Hamad, alisema alikuwa ameshinda kwa zaidi ya
52%.
Bado haijafahamika ikiwa Dk. Shein ataunda serikali nyengine yenye
muundo wa umoja wa kitaifa, kwasababu mbali na chama chake, hakuna
chama kingine kilichotangazwa na ZEC kufikia asilimia 10 ya kura za
jumla wala kupata wajumbe kwenye baraza la wawakilishi, masharti muhimu
kwa chama kujumuishwa kwenye uundaji wa serikali kwa mujibu wa katiba ya
visiwa hivyo.
CHANZO: NIPASHE
0 MAONI YAKO:
Post a Comment