
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania amesema kuwa,
zaidi ya dola za Kimarekani bilioni 80 zinahitajika katika kukamilisha
ujenzi wa miundombinu kwa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).
Kassim Majaliwa amesema hayo jijini Dar es Salaam wakati akifungua
kikao cha tano cha Bunge la tatu la Jumuiya ya Afrika Mashariki
kitakachofanyika kwa muda wa wiki mbili. Majaliwa amebainisha kuwa, nchi
za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), zinahitaji dola za Kimarekani
bilioni 20 ili kufanikisha ujenzi wa barabara, pamoja na dola za
Kimarekani bilioni 30 ili kukamilisha ujenzi na ukarabati wa reli.
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ameongeza kuwa, dola za
Kimarekani bilioni 10 zinahitajika katika upanuzi wa bandari, na ujenzi
wa bandari mpya, na dola za Kimarekani bilioni tano zinahitajika kwa
ajili ya ufufuaji wa umeme na miradi mbalimbali ya kuzalishia nishati
hiyo.
Kuhusu ujenzi wa reli ya viwango vya kimataifa Waziri Mkuu wa
Tanzania amesema kuwa, ukarabati na upembuzi yakinifu kuhusu ujenzi wake
umeshaanza kwa baadhi ya nchi. Aidha katika kikao cha ufunguzi wa Bunge
la tatu la Afrika Mashariki hapo jana, Spika wa Bunge la EAC, Daniel
Kidega, alimwapisha mjumbe mpya wa bunge hilo, Balozi Augustine Mahiga
ambaye ni Waziri wa Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
Kikanda na Kimataifa wa Tanzania.
0 MAONI YAKO:
Post a Comment