March 28, 2016


Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Antony Mtaka
 
MKURUGENZI wa Halmashauri ya wilaya ya Itilima mkoani Simiyu, John Aloyce amesimamishwa kazi kutokana na tuhuma mbalimbali ikiwemo kushindwa kuisimamia halmashuari hiyo na kusababisha kuwepo kwa migogoro ya mara kwa mara kati ya madiwani na watendaji.

Uamuzi huo umechukuliwa na Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Antony Mtaka katika kikao cha dharura cha Baraza la Madiwani kilichofanyika jana mjini Langangabilili wilayani humo. 

Mbali na uamuzi huo, amefuta posho zote kwa wakuu wa idara na vitengo katika halmashauri zote zilizoko mkoani hapa wanaoingia katika vikao vya madiwani.

Vikao hivyo ni pamoja na Baraza na kamati za halmashauri kwa madai kuwa hazina tija yoyote, na kuelekeza fedha hizo zilizotengwa zifanye kazi nyingine za maendeleo kama vile utengenezaji wa madawati.

Alisema alipata malalamiko dhidi ya Mkurugenzi huyo kupitia wajumbe wa Kamati ya Fedha na Mipango wa halmashauri hiyo waliofika ofisini kwake, hivyo kuamua kuitisha kikao hicho cha dharura ili kuyasikiliza.

 Katika kikao hicho madiwani hao walisema serikali ilitoa Sh milioni 450 kwa ajili ya ujenzi wa nyumba za watumishi katika halmashauri hiyo lakini kazi hiyo haikufanyika, wanapohoji na kutoa uamuzi umekuwa haufanyi kazi.

“Wilaya yetu ni mpya na katika kuondoa tatizo la watumishi wa halmashauri hii kuishi mbali na makao makuu ya wilaya tuliamua kuanza ujenzi wa nyumba za watumishi na tukaletewa Sh milioni 450. Lakini kila tunapohoji matumizi ya fedha hizo hatupatiwi majibu na tunapomwagiza Mkurugenzi atuletee hakubaliani na maamuzi yetu,”alisema Kuzenza William (CCM), ambaye ni Diwani wa Kata ya Zagayu.

Walisema kuwa hata mapato ya ndani yanayopatikana hayafahamiki licha ya kuwepo kwa ushuru wa mazao mchanganyiko haulipwi na wafanyabiashara walio wengi, hivyo kusababisha shughuli nyingi za halmashauri kukwama na kuzua migogoro ya mara kati ya madiwani na ofisi ya Mkurugenzi.

“Mapato ya ndani hayafahamiki kabisa kuwa ni kiasi gani cha fedha kimepatikana, maana hatusomewi na inaonekana hata ushuru wa mazao mchanganyiko wafanyabiashara hawalipi hii timu ya mkurugenzi inayosimamia mapato sina imani nayo,” alisema Diwani Kata ya Lugulu, Robert Jongela. 

Mwenyekiti wa halmashauri hiyo, Daud Nyalamu alisema madiwani wa halmashauri hiyo wanaonekana hawana uamuzi kwani waliagiza kuwa vifaa vyenye thamani ya Sh milioni 320 vilivyokopwa na halmashauri hiyo kwa ajili ya ujenzi wa maabara 35 za shule za sekondari vifanye kazi, lakini hadi sasa hakuna kilichofanyika na vingi vimeharibika.

“Tulikopa benki Sh milioni 320 kwa ajili ya ujenzi wa maabara 35 zilizoko katika halmashauri yetu, vifaa vimenunuliwa lakini hadi sasa vimesambazwa maeneo mbalimbali havijafanyiwa kazi. Vimeharibika kwani saruji imeganda na mbao zimepinda na hazifai kwa ujenzi. Hii inatokana na uzembe wa Mkurugenzi wetu na kila kukicha halmashauri inadaiwa hadi madiwani hatulipwi stahili zetu,” alisema.

Akizungumzia tuhuma dhidi yake, Aloyce alisema tangu ateuliwe kuwa Mkurugenzi wa halmashauri hiyo miezi sita iliyopita alikuta Sh milioni 126 zilizokuwa zimebaki katika ujenzi wa nyumba za watumishi.

“Mimi wakati nafika katika halmashauri hii nilikuta kati ya Sh milioni 450 za ujenzi wa nyumba za watumishi zilikuwa zimebaki Sh milioni 126, tulikaa na wakuu wa idara tukaamua tuzikope na kujenga ukumbi ukizingatia ya kuwa tulikuwa tunaelekea uchaguzi mkuu hivyo tungeshindwa mahali pa kukusanyia matokeo ya kura,” alisema.

Alisema licha ya tuhuma mbalimbali dhidi ya halmashauri hiyo, iliundwa tume kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Simiyu kuzichunguza lakini hadi sasa hawajawaletea majibu, hivyo kuomba iundwe tume huru kutoka nje ya mkoa ili kuweza kuzichunguza tuhuma zilizotajwa na madiwani dhidi yake na ikibainika yuko tayari kuachia ngazi.

0 MAONI YAKO:

Post a Comment

Popular Posts

WADAU

BLOG ZINGINE