Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amefika
nyumbani kwake katika kijiji cha Mlimani, Wilaya ya Chato Mkoani Geita
kwa mara ya kwanza tangu achaguliwe kuwa Rais, ambapo akizungumza
na wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika uwanja wa
shule ya sekondari Chato, ametoa wito kwa kila mtanzania kuchapa kazi
kwa juhudi ili nchi iondokane na utegemezi wa misaada ya wafadhili
ambayo huambatana na masharti.
Dkt.
Magufuli amesema jukumu kubwa lililo mbele ya watanzania kwa sasa, ni
kushikamana na kujisimamia katika maendeleo ili kila mmoja ahakikishe
anaongeza uzalishaji na utendaji kazi mahali pake pa kazi.
"Kwa
hiyo ni lazima tujisimamie sisi wenyewe, na tukijisimama sisi wenyewe
kwa kila mmoja kuwajibika mahali alipo, kama ni mfanyakazi afanye kazi
kwelikweli, kama ni mkulima afanye ukulima wake kwelikweli, kama ni
mfanyabiashara afanye biashara kwelikweli, kama ni mfugaji afuge
kwelikweli, kama ni mvuvi avue kwelikweli, Tanzania hii tutavuka" Amesema Rais Magufuli.
Aidha,
Rais Magufuli amesema serikali yake imeamua kuchukua hatua kudhibiti
nidhamu serikalini, kwa kuhakikisha inawachukulia hatua watumishi wa
umma wanaolisababishia taifa upotevu mkubwa wa fedha, na ameahidi kuwa
hatua hizo maarufu kwa jina la "Kutumbua Majipu" zitaendelea kuchukuliwa
hadi tatizo hilo likomeshwe.
Dkt.
Magufuli pia amekumbusha viongozi wote wakiwemo Wakuu wa Mikoa, Wakuu
wa Wilaya, Makatibu Tawala na Wakurugenzi, kutekeleza wajibu wao
ipasavyo na ameweka bayana kuwa mahali popote ambapo hapatakuwa na
ufanisi, kiongozi husika atakuwa amedhihirisha kuwa hatoshi kuendelea na
wadhifa aliopewa.
Rais
Magufuli amewapongeza walimu kote nchini kwa kufanya kazi nzuri ya
kufundisha, licha ya changamoto ya ongezeko kubwa la wanafunzi
waliojiunga darasa la kwanza mwaka huu, lakini ametaka Wazazi na kamati
za shule kushirikiana na walimu kuwasimamia wanafunzi ili waweze kufanya
vizuri katika masomo yao.
"Niziombe
kamati za shule zote Tanzania nzima, kama haziwezi kusimamia nidhamu ya
wanafunzi shuleni, zile kamati za shule zijiuzulu. Lakini pia kama wewe
ni Mwalimu Mkuu, shule yako kila siku inatoa divisheni ziro nyingi kila
mwaka, sioni sababu ya wewe kuendelea kuwa Mwalimu Mkuu" Alisisitiza Dkt. Magufuli.
Kuhusu
tatizo la wafanyakazi hewa, Rais Magufuli amesema uhakiki mdogo
uliofanywa hivi karibuni, umebaini wafanyakazi hewa 1,680 waliokuwa
wakilipwa shilingi bilioni 1 na milioni 800, na kwamba ni matarajio kuwa
uhakiki unaofanywa nchi nzima utaisaidia serikali kubaini wafanyakazi
hewa wengi zaidi na kunusuru fedha nyingi zaidi za watanzania.
Ametolea
mfano wa mfanyakazi mmoja wa Mamlaka ya Mapato Nchini (TRA) ambaye
alikuwa akilipwa mishahara ya watu 17, na kueleza kuwa mfanyakazi huyo
atafikishwa mahakamani.
Pia
Rais Magufuli amesema serikali yake imejiandaa kuboresha maslahi ya
wafanyakazi kwa kupunguza kodi kutoka asilimia 11 ya sasa hadi asilimia
10 au 9 kuanzia bajeti ijayo, lakini amesema kwa wale wanaolipwa
mishahara mikubwa ambayo inafikia hadi shilingi milioni 40, itapunguzwa
na kuweka kima cha juu cha mshahara usiozidi shilingi milioni 15.
0 MAONI YAKO:
Post a Comment