CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimeanza harakati za kuwatema makada wake wanaotuhumiwa kujihusisha na vitendo vya rushwa kwa madai ya kuonesha taswira hasi kwa wananchi
Shaka Hamudu Shaka, Katibu Mkuu wa Umoja wa Vijana wa CCM-Taifa (UVCCM) amesema kuwa, wabunge wa chama hicho wanaotuhumiwa pia wengine wanaojihusisha na vitendo vya rushwa wanapaswa kutimliwa ndani ya chama hicho.
Kauli ya Shaka inakuja ikiwa ni siku chache baada ya wabunge wanne wa CCM kupandishwa kizimbani wakituhumiwa kuomba rushwa ya Sh. 30 milioni kutoka kwa Mbwana Magotta, Mkurugenzi wa Halmashauli ya Gairo.
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) imewapandisha kizimbani Kangi Lugola, Mbune wa Mwibara; Ahmed Sadiki, Mbunge wa Mvomelo; Victor Mwambalaswa, Mbunge wa Lupa na Richard Ndasa, Mbune wa Sumve kutokana na tuhuma hizo.
Akizungumza katika mkutano wa hadhara jana, uliofanyika katika Uwanja wa Magomeni, Kata ya Kirumba Wilaya ya Ilemela, mwanza, Shaka amesema kuwa wabunge na watumishi wa umma wanaojihusisha na rushwa wanapaswa kuchukulia hatua.
Shaka amesema kuwa wabunge wa chama hicho tawala wanaotuhumiwa kuomba na kupokea rushwa, wanapaswa kuchukuliwa hatua ikiwemo kuvuliwa madaraka na pia isiishie kupandishwa kizimbani pekee.
“Wabunge ambao wameshindwa kuwatumikia wananchi waliowapa ridhaa hiyo na wameanza kupokea rushwa wanapaswa kutokuonewa aibu, inapaswa wachukuliwe hatua zaidi ya kupelekwa mahakamani ili iwe fundisho kwa wengine.
“Tunapaswa kuheshimu sheria za nchi na Katiba ya nchi yetu, mtu ambaye atabainika kujihusisha na sheria anapaswa kuchukuliwa hatua, sisi ndani ya chama chetu (CCM) hatuungi mkono wabunge wanaojihusisha na rushwa,” amesema Shaka.
Licha ya kutowataja kwa majina Shaka aliwagusa wabunge hao kwenye maelezo yake kwa kuwa ndio waliopandishwa kizimbani kuanzia Aprili 1 mwaka huu katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam.
Miraj Mtaturu, Katibu wa CCM Mkoa wa Mwanza ameunga mkono kauli ya Shaka “CCm hatuungi mkono wabunge ambao wanapokea rushwa, viongozi wote wanaojihusisha na vitendo hivyo wanapaswa kuchukuliwa hatua, wao wanapaswa kuwatumikia Watanzania na sio kuomba rushwa.”
0 MAONI YAKO:
Post a Comment